Nov 27, 2020 02:26 UTC
  • Ijumaa, Novemba 27, 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 11 Mfunguo Saba Rabiuthani 1442 Hijria sawa na Novemba 27 mwaka 2020 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 834 iliyopita, alizawa mjini Mosul, moja ya miji mashuhuri ya Iraq, Ebn-e Xallakan, kadhi, mwanahistoria na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu. Akiwa kijana alisoma elimu za awali katika mji alikozaliwa na kisha kufanya safari mbalimbali na kukutana na wanasheria wa Kiislamu na wanahistoria wakubwa sanjari na kustafidi na elimu kutoka kwao. Kwa muda mrefu Ebn-e Xallakan alikuwa kadhi mjini Damascus, Syria ya leo huku akiwa mtaalamu pia katika elimu za Historia, fasihi ya Kiarabu na mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwezi wa Rajab mwaka 681 Hijiria baada ya kuugua na kuzikwa chini ya mlima Qasioun ulio Damascus ambako pia wamezikwa wasomi wengi.

Siku kama ya leo miaka 319 iliyopita, sawa na tarehe 27 Novemba mwaka 1701, Anders Celsius mwanafizikia na mtafiti wa Sweden alizaliwa katika mji wa Uppsala, uliokuwa makao makuu ya utamaduni ya nchi hiyo. Familia yake ilikuwa ya wasomi na baba na babu yake walikuwa wanahisabati. Celsius alivutiwa sana na elimu ya nujumu na mwaka 1730 alifanikiwa kuwa mwalimu wa nujumu katika chuo kikuu cha Uppsala. Mwaka 1742 alipendekeza kutumika daraja ya kipima joto kwa mujibu wa Celsius, iliyoitwa kwa jina lake. Mpangilio huo ulikubaliwa rasmi na kuanza kutumika duniani mwaka 1945, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kufariki dunia mwanafizikia huyo.

Tarehe 27 Novemba miaka 100 iliyopita iliainishwa mipaka mipya ya nchi za Ulaya na Mashariki ya Kati baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia. Baada ya kumalizika vita hivyo na kutiwa saini mkataba wa amani wa Versay, kulisainiwa mikataba mingine kadhaa ya kuainisha mustakbali wa tawala za Austria na Hungari na utawala wa Othmania na nchi ya Bulgaria ambayo kila mmoja ulikuwa na masharti mazito na kutoa fidia nchi hizo kwa zile zilizopata ushindi. Kuainishwa kwa mipaka mipya ya nchi za Ulaya na Mashariki ya Kati katika mkutano wa Paris kulibadili kabisa ramani ya dunia.

Na katika siku kama ya leo 40 iliyopita, vikosi vya majini vya Iran vilifanya ooperesheni katika maji ya Ghuba ya Uajemi na kufanikiwa kuvisambaratisha vikosi vya majini vya Iraq. Tukio hilo lilitokea takribani miezi miwili tu baada ya kuanza vita vya kichokozi vya Iraq dhidi ya Iran. Operesheni hiyo ilipelekea kutokea mapigano makali kati ya meli za kivita za pande mbili na meli nyingi za kivita za Iraq ziliteketezwa. Kutokana na ushujaa wa wapiganaji wa vikosi vya majini katika operesheni hiyo, siku hii inajulikana hapa nchini kwa jina la “Siku ya Jeshi la Majini”.