Nov 28, 2020 03:26 UTC
  • Jumamosi, 28 Novemba, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 12 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1442 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 28 Novemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1310 iliyopita, yaani tarehe 12 Mfunguo Saba Rabiul Thani mwaka 132 Hijria, Abul Abbas Abdullah bin Muhammad maarufu kwa jina la 'Saffah' alikalia kiti cha uongozi akiwa khalifa wa kwanza wa kizazi cha Bani Abbas. Utawala huo wa Kiabbasi kwa kushirikiana na Abu Muslim Khorasani na majeshi yake, ulimuua Marwan wa Pili, mtawala wa mwisho wa ukoo wa Bani Umayyah na kuondoa madarakani utawala wao. Bani Abbas nao kama walivyokuwa watawala wa Bani Umayyah, waliwakandamiza raia na Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) na kufanya dhulma kubwa, na utawala wao uliendelea kushika madaraka katika ulimwengu wa Kiislamu hadi mwaka 656 Hijria. ***

Abul Abbas Abdullah bin Muhammad

 

Miaka 263 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa William Blake mshairi na mchoraji wa Kiingereza. Blake alikuwa na mapenzi na sanaa tangu akiwa mdogo na alipofikisha rika la ubarobaro alijihusisha na kusoma vitabu vya falsafa na mashairi. Athari za mshairi huyo zilikuwa zikipingana wazi na kanisa, hali ambayo iliwakasirisha mno viongozi wa dini ya Kikristo na watawala wa Uingereza. Hadi anaaga dunia mwaka 1827, msomi huyo wa Uingereza alikuwa ameandika vitabu 13. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni The Marriage of Heaven and Hell, The Tiger, The Chimney Sweeper na The Lamb. ***

William Blake

 

Tarehe 28 Novemba mwaka 1820 yaani miaka 200 iliyopita, alizaliwa mwanafalsafa mashuhuri wa Ujerumani Friedrich Engels. Alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa mwanafalsafa mwingine wa Ujerumani kwa jina la Karl Marx. Engels alifuatiliwa na kusakwa na vyombo vya dola kutokana na harakati zake za kisiasa na mwaka 1850 alikimbilia nchini Uingereza. Engels na Karl Marx walitayarisha Manifesto ya Ukomunisti iliyotangazwa na vyama vya kikomunisti katika mkutano wao wa kwanza hapo mwaka 1848. Baada ya  Karl Marx, Friedrich Engels alikuwa na nafasi muhimu katika kubuni nadharia za kikomunisti ambazo ziliugawa ulimwengu katika kambi mbili za kisoshalisti na kibepari. ***

Friedrich Engels.

 

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita Mauritania ilitangaza rasmi uhuru wa nchi hiyo. Mauritania ilikuwa ikikoloniwa na Ureno tangu karne ya 15 Miladia. Baadaye Uholanzi na Uingereza ziliivamia nchi hiyo na mwaka 1903 Mauritania ikawa koloni la Ufaransa. Katika nusu ya pili ya karne ya ishirini wananchi wa Mauritania walipiga kura ya maoni wakitaka kuasisiwa utawala wa jamhuri ya mamlaka ya ndani. Na hatimaye mwaka 1960 Mauritania ilipata uhuru kamili baada ya kusainiwa makubaliano kati yake na serikali ya Ufaransa. ***

Bendera ya Mauritania

 

Na miaka 49 iliyopita katika siku kama ya leo Iran ilidhibiti visiwa vitatu vya Tomb Kubwa, Tomb Ndogo na Bu Musa baada ya kuondoka vikosi vamizi vya Uingereza katika maeneo hayo. Uingereza iliondoka katika visiwa hivyo vitatu vya Iran vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi katika fremu ya mpango wa nchi hiyo wa kuondoa wanajeshi wake katika eneo la Bahari ya Mediterranean na Ghuba ya Uajemi kutokana na matatizo ya kisiasa na kiuchumi yaliyokuwa yakiisumbua nchi hiyo. ***

Visiwa vitatu vya Iran vya Tombu Kubwa, Tombu Ndogo na Bu Musa

 

Tags