Nov 30, 2020 04:34 UTC
  • Jumatatu, 30 Novemba, 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 14 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1442 Hijria mwafaka na tarehe 30 Novemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1376 iliyopita Mukhtar bin Abi Ubaida al Thaqafi alianza mapambano ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali AS, mjukuu wa Mtume Muhammad SAW. Mwaka 61 Hijria Imam Hussein AS akiwa pamoja na wafuasi na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na jeshi la Yazid akiwa katika harakati za kuilinda dini tukufu ya Uislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake za mapambano katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilipigana na utawala wa Bani Umayyah, kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS. Mukhtar Thaqafi alitawala Kufa kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja na mwishowe alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa shahidi. ***

Kaburi la Mukhtar bin Abi Ubaida al Thaqafi

 

Miaka 353 iliyopita katika siku kama ya leo, Jonathan Swift mwandishi mashuhuri wa Ireland alizaliwa huko Dublin mji mkuu wa nchi hiyo. Swift alishiriki pakubwa katika harakati za ukombozi wa Ireland. Baadaye, Jonathan Swift alianza kujishughulisha na kazi ya uandishi. Swift alifariki dunia akiwa na miaka 78. ***

Jonathan Swift

 

Katika siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, alizaliwa Theodor Mommsen mwanahistoria na mtafiti wa Ujerumani. Baada ya kumaliza masomo, Mommsen alijishughulisha na utafiti kuhusiana na vitabu tofauti na athari zilizobakia za tamaduni za zamani. Miongoni mwa vitabu vyake maarufu zaidi ni kitabu kinachoitwa 'Historia ya Roma ya Kale' ambacho ni kitabu kamili cha historia kuhusiana na mji wa Roma. Mwanahistoria huyo wa Ujerumani alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi hapo mwaka 1902 Miladia na kufariki dunia mwaka mmoja baadaye, akiwa na umri wa miaka 86. ***

Theodor Mommsen

 

Miaka 185 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Mark Twain mwandishi mashuhuri wa Kimarekani. Twain alikipitisha kipindi cha utoto na ubarobaro wake na matukio yasiyo ya kawaida ambayo baadaye yalikuja kuwa maudhui kuu ya vitabu vyake. Mark Twain alikuwa mwandishi mwenye utani na mzaha. Aliandika visa na simulizi nyingi kwa ajili ya watoto na vijana wadogo ambapo tunaweza kuashiria hapa vitabu vyake viwili vya The Andventures of Tom Sawyer na (Matukio Yasiyo ya Kawaida ya Tom Sawyer) The Prince and The Pauper (Mrithi wa Kiti cha Ufalme na Ombaomba). Mwishoni mwa umri wake Mark Twain alikumbwa na ukata na umasikini mkubwa na hatimaye akaaga dunia mwaka 1910 baada ya kuugua.  ***

Mark Twain

 

Miaka 120 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Oscar Wilde, mwandishi na malenga mahiri wa Ireland. Wilde alizaliwa mwaka 1854 katika familia iliyokuwa na mapenzi maalumu na masuala ya kiutamaduni na Sanaa. Baada ya kukamilisha masomo yake ya sekondari alijiunga na Chuo Kikuu. Oscar Wilde alianza kujihusisha na taaluma ya uandishi akiwa katika rika la ujana na katika kipindi kifupi cha umri wake alifanikiwa kuandika vitabu mbalimbali vilivyokuwa na madhumuni ya riwaya, mashairi na maigizo. Baadhi ya vitabu vya Oscar Wilde ni The Model Millionaire, The Soul of Man Under Socialism na The Canterville Ghost. ***

Oscar Wilde

 

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, nchi ya Barbados ambayo kijiografi ipo Amerika ya Kati ilijikomboa na kupata uhuru. Siku ya leo ya Novemba 30 inajulikana nchini humo kama siku ya taifa. Barbados ambayo ni nchi ndogo ya Amerika ya Kati ilivumbuliwa na Uhispania katika karne ya 15 na kukaliwa kwa mabavu na nchi hiyo ya Ulaya. Karne moja baadaye Ureno ikadai mamlaka huko Barbados. Hadi kufikia karne ya 17 nchi mbili hizo za kikoloni yaani Ureno na Uhispania ziliwatimua nchini humo wakazi wa asili wa ardhi hiyo. Barbados ina ukubwa wa kilomita mraba 431 na ipo baina ya Bahari ya Caribbean na kaskazini mwa Amerika ya Kusini na mji mkuu wake ni Bridgetown. ***

Bendera ya nchi ya Barbados

 

Na katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, aliaga dunia katika mji wa Cairo Misri, Ustadh Abdul-Basit Abdul-Samad, mmoja wa waalimu na maqarii wakubwa wa Qur'ani Tukufu. Abdul-Basit alianza kujifunza Qurani Tukufu tangu akiwa mdogo na alipofikia umri wa miaka 12 akafanikiwa kupata tunzo ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani. Ustadh Abdul-Basit katika maisha yake alijishughulisha na usomaji wa Qurani Tukufu na kutunukiwa zawadi na tunzo muhimu katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu kwenye nchi mbalimbali za Kiislamu, sambamba na kuwavutia Waislamu wengi kwenye kusoma maneno hayo ya Mwenyezi Mungu. Abdul Basit ameacha kanda nyingi za sauti yake nzuri ya Qur'ani Tukufu. ***

Ustadh Abdul-Basit Abdul-Samad,

 

Tags