Dec 21, 2020 09:29 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Dec 21

Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.

Persepolis ya Iran yaibuka ya 2 fainali AFC

Klabu ya Persepolis ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka mshindi wa pili katika Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia (AFC Champions League) mwaka huu 2020 iliyopigwa Jumapili hii ya Disemba 19 huko Doha, mji mkuu wa Qatar. Hii ni baada ya klabu hiyo kushindwa kufurukuta mbele ya klabu ya Ulsan Hyundai Motors ya Korea Kusini katika fainali ya Jumapili na mchuano huo uliopigwa katika Uwanja wa al-Junoub mjini Doha kuishia kwa Wekundu wa Tehran kuzabwa mabao 2-1.  Katika dakika za kwanza, Persepolis walitanda gozi na kumiliki vizuri mpira. Kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza, klabu hiyo ya Iran ilipata bao la aina yake lililotiwa wavuni na Mehdi Abdi. Hata hivyo Ulsan Hyundai ya Korea ilisawazisha mambo kupitia mkwaju wa penati lililofungwa na Mbrazil Junior Negrao. Klabu hiyo ya Korea ilifunga la pili na ushindi kupitia mkwaju mwingine wa penati baada ya Mehdi Shiri kuunawa mpira kwenye sanduku la hatari.

Wachezaji wa klabu ya Persepolis

 

The Reds ya Tehran ilipoteza nafasi nyingi za wazi za kusawazisha mambo n ahata kuibuka mshindi na hivyo kumalizi ligi hiyo ya kieneo katika nafasi ya pili kama walivyofanya mwaka 2018, waliposasambuliwa na Kashima ya Japan mabao 2-0. Klabu hiyo ya Korea ilitinga fainali baada ya kuizaba Vissel Kobe ya Japan mabao 2-1 katika mchuano wa nusu fainali ya pili uliochezwa Jumapili ya wiki iliyopita katika Uwanja wa Al Sadd mjini Doha. Persepolis ilitangulia kutinga fainali ya ligi hiyo ya kieneo baada ya kuigaragaza klabu hiyo ya al-Nassr ya Saudia mabao 5-3 kweye nusu fainali ya kwanza. Persepolis imepoteza fursa ya kumaliza ukame wa ubingwa wa miaka 27 kwa Iran na iwapo ingeliibuka mshindi, basi ingekuwa klabu ya kwanza ya Iran kutwaa taji hilo la kikanda tokea mwaka 1993, ambapo Pas ya Tehran iliibuka kidedea.

Tuzo za FIFA 2020

Mshambuliaji mahiri Robert Lewandowski wa Bayern Munich alitawazwa Mchezaji Bora wa Kiume wa Mwaka 2020 kwenye tuzo za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) zilizotolewa jijini Zurich, Uswisi mnamo Alkhamisi. Lewandowski alimpiku mshindi wa tuzo hiyo katika mwaka wa 2019 Lionel Messi pamoja na nyota wa Juventus na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo. Lewandowski ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Poland alifunga mabao 55 kutokana na mechi 47 za msimu uliopita wa 2019-20 na kusaidia Bayern kutia kapuni mataji matatu kwa mkupuo. Sogora huyo mwenye umri wa miaka 32 pia alikamilisha kampeni za msimu wa 2019-20 akiwa mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), mashindano ya kuwania makombe mbalimbali na gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Robert Lewandowski 

 

Beki Lucy Bronze wa Manchester City alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake. Washindi wa tuzo hizo waliamuliwa kupitia uteuzi uliofanywa na manahodha wa timu za taifa, makocha wa timu za taifa, kura za siri zilizopigwa na baadhi ya mashabiki na wawakilishi 200 wa vyombo vya habari. Hii ni mara ya kwanza kwa Lewandowski kutia kapuni taji hilo ambalo limekuwa likitamalakiwa na Lionel Messi wa Barcelona na Cristiano Ronaldo.

Kwa upande wa makocha, Jurgen Klopp alitawazwa Kocha Bora wa Mwaka kwa ufanisi wa kuwaongoza Liverpool kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 mnamo 2019-20. Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Klopp ambaye ni raia wa Ujerumani kupokezwa tuzo hiyo. Manuel Neuer wa Bayern alitawazwa Kipa Bora wa Mwaka baada ya kuwapiga kumbo Jan Oblak wa Atletico Madrid na Alisson Becker wa Liverpool.

Ligi ya EPL

Kocha Brendan Rodgers wa Leicester City amesisitiza kwamba wanasoka wake “hawatajinaki kupita kiasi na kujisahaulisha majukumu yaliyoko mbele yao” licha ya kuwaangusha majabali Tottenham Hotspur mnamo Jumapili na kupaa hadi nafasi ya pili kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Leicester walishuka dimbani kwa minajili ya mchuano huo wakishikilia nafasi ya nne jedwalini huku Spurs ya kocha Jose Mourinho ikishikilia nafasi ya tatu kwa alama 25. Jamie Vardy aliwafungia Leicester bao la kwanza kupitia penalti ya dakika ya 45 kabla ya Toby Alderweireld kujifunga katika dakika ya 59.

Ushindi huo wa Leicester uliwapaisha hadi nafasi ya pili kwa alama 27, nne pekee nyuma ya mabingwa watetezi Liverpool waliotua kileleni mnamo Jumamosi baada ya kutandika Crystal Palace 7-0 uwanjani Selhurst Park mnamo Disemba 19. Scott McTominay aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili chini ya dakika tatu za ufunguzi wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) alipowasaidia waajiri wake Manchester United kudhalilisha Leeds United 6-2 mnamo Jumapili ugani Old Trafford. Kiungo huyo aliwafungulia Man-United karamu ya mabao baada ya sekunde 67 pekee kabla ya kufunga goli la pili sekunde chache baadaye kwa kukamilisha krosi ya Anthony Martial. Bruno Fernandes na Victor Lindelof walitikisa pia nyavu za Leeds United katika dakika za 20 na 37 mtawalia kabla ya Liam Cooper kurejesha waajiri wake mchezoni kupitia bao la kichwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Daniel James alifungia Man-United bao la nne katika dakika ya 65 kabla ya Fernandes kuongeza goli lake la pili kupitia penalti iliyotokana na tukio la Martial kuchezewa visivyo na Pascal Struijk ndani ya kijisanduku. Stuart Dallas aliwapachikia Leeds United bao la pili kunako dakika ya 73 kwenye mchuano huo wa kusisimua ulioshuhudia jumla ya makombora 43 yakivurumishwa na wachezaji wa vikosi vyote viwili.

Baadhi ya wachezaji wa Man U

 

Ushindi kwa Man-United wanaotiwa makali na kocha Ole Gunnar Solskjaer uliwapaisha miamba hao wa soka ya Uingereza hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 26 sawa na Everton waliopepeta Arsenal 2-1 ugani Goodison Park mnamo Disemba 19. Kwengineko klabu ya Liverpool waliweka wazi azma ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kudhalilisha Crystal Palace 7-0 mnamo Disemba 19, 2020. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Liverpool kufunga jumla ya mabao saba tangu waipepete Derby County mnamo 1991. Liverpool walishambulia sana wenyeji wao baada ya kila dakika na wakasajili ushindi wa kwanza wa ligi ugenini tangu Septemba 2020. Minamino aliwafungulia Liverpool ukurasa wa mabao katika dakika ya tatu. Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa nyota huyo kufunga katika EPL baada ya miezi 12. Sadio Mane na Roberto Firmino walifunga mabao mengine ya Liverpool katika kipindi cha kwanza. Hata hivyo, Mane alionekana kukerwa na hatua ya kuondolewa kwake uwanjani katika kipindi cha kwanza na nafasi yake kutwaliwa na Salah katika dakika ya 57. Henderson alipachika wavuni goli la nne la Liverpool kabla ya Firmino kupachika wavuni la tano. Salah alicheka na nyavu za Palace kwa mara nyingine katika dakika za 81 na 84 na kuzamisha kabisa chombo cha wenyeji wao.

Ushindi kwa Liverpool uliwawezesha kufungua mwanya wa alama sita kileleni mwa jedwali la EPL. Na klabu ya Mchester City walijongea ndani ya mduara wa nne-bora kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Disemba 19, 2020, baada ya kuwapokeza Southampton kichapo cha 1-0 uwanjani St Mary’s. Bao hilo la pekee katika mechi hiyo lilipachikwa wavuni na fowadi Raheem Sterling aliyekamilisha kwa ustadi krosi ya kiungo Kevin de Bruyne baada ya dakika 16.

Na kwa kutamatisha klabu ya Celtic iliwagaragaza Hearts kichapo cha mabao 4-3 kupitia mikwaju ya penalti na kutwaa taji la Scottish Cup kwa mara ya 40 mnamo Jumapili ya Disemba 20. Mshindi wa mechi hiyo aliamuliwa kupitia penalti baada ya vikosi vyote kutoshana nguvu kwa sare ya 3-3 mwishoni mwa muda wa ziada. Kristoffer Ajer alifungia Celtic penalti ya mwisho na kusaidia waajiri wake kunyanyua taji lililoanza kuwaniwa na vikosi vya Scotland katika msimu wa 2019-20 kabla ya kukamilika baada ya miezi 16 kwa kuwa kivumbi hicho kiliahirishwa kwa sababu ya corona. Ryan Christie na Odsonne Edouard waliwaweka Celtic kifua mbele kwa mabao 2-0 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza kabla ya Liam Boyce na Stephen Kingsley kusawazishia Hearts na kufanya kivumbi hicho kuingia muda wa ziada. Japo Leigh Griffiths aliwarejesha Celtic uongoni katika dakika ya 105, jitihada zake zilifutwa na Josh Ginnelly aliyefanya mchuano kuingia kwenye penalti ndipo mshindi apatikane.

………………….TAMATI….….……….

 

 

Tags