Dec 23, 2020 11:04 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia (16)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.

 

Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia  Sheikh Fadhlu bin Hassan Tabarsi mwandishi wa tafsiri mashuhuri ya Qur’ani ya Majmaa al-Bayan. Tulieleza kwamba, Fadhl bin Hassan Tabarsi aliyezaliwa mwaka 468 Hijria na kufariki dunia mwaka 548 alikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa wa Kishia na mfasiri wa Qur’ani Tukufu katika karne ya tano na ya sita Hijria. Sehemu ya 16 ya kipindi hiki juma hili itamzungumzi Said bin Abdallah Ravandi Kashani mashuhuri kwa jina la Qutub al-Ravandi msomi, alimu, mpokezi wa hadithi, mwanateolojia, fakihi, mwanafalsafa na mwanahistoria mkubwa wa Kishia katika karne ya sita Hijria. Karibuni kujiunga nami hadi mwisho wa dakika chache za kipindi hiki.

 

Karne ya Sita Hijria kilikuwa kipindi cha utawala wa koo mbili kubwa za kifalme za Iran yyaani Saljukiyan na Khawarazmshahiyan. Katika zama hizo hususan katika kipindi cha utawala wa Saljukiyan, fikra za dini na muelekeo wa Sunna uliishinda mielekeo ya akili, na akthari ya vitabu vya akili na falsafa vilichomwa moto. Watawala wa Saljukiyan hususan waziri wake mashuhuri aliyejulikana kwa jina la Khoja Nidhamul Mulk walikuwa watu wenye kufuata mielekeo ya viongozi waliokuwa wakipinga utumiaji akili na nafasi ya akili.

Kuibuka vita vya msalaba na hujuma pamoja na mashambulio ya watu wa Ulaya dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu kulikuwa na matokeo mabaya kama kuporwa hazina na dafina za kielimu za Waislamu. Licha ya licha ya matukio hayo yote, lakini karne ya 6 Hijria iliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la karne ya elimu na maarifa. Hii ni kutokana na kuwa, wasomi na wanazuoni wengi walichomoka na kuibuka katika zama hizo ambapo kwa hima na idili yao ya kielimu isiyo na kikomo waliweza kutoa huduma kubwa kwa Uislamu.

Qutub al-Ravandi

 

Miongoni mwa wanazuoni hao waliokuwa na hima kubwa, ni msomi aliyekuwa na daraja ya juu, fakihi na mpokezi mashuhuri wa hadithi aliyejulikana kwa jina la Said bin Hibatullah Ravandi ambaye ni mashuhuri zaidi kwa jina la Qutub Ravandi.

Said bin Hibatullah Ravandi Kashani, mashuhuri kwa jina la Qutub Ravandi alikuwa mpokezi wa hadithi, mfasiri, mwanateolojia, fakihi, mwanafalsafa na mwanahistoria mkubwa katika karne ya Sita Hijria. Alimu na msomi huyu alikuwa mmoja wa wanafunzi hodari na maalumu wa Sheikh Tabarsi ambaye ni mwandishi wa Tafsiri ya Qur’ani ya Majmaul-Bayan. Wanazuoni wakubwa wa dini wanamtaja Qutub al-Ravandi kama mpokezi mkubwa zaidi wa hadithi wa Kishia na aliyekuwa na kipaji kikubwa katika elimu za Kiislamu ambaye hakutambuliwa daraja na thamani yake kama inavyotakiwa.

 

Allama Qutub al-Ravandi alizaliwa katika kijiji cha Ravand jirani na mji wa kihistoria wa Kashan nchini Iran. Hata hivyo inasikitisha kuwa, hakuna taarifa na maelezo mengi kuhusiana na kipindi cha utoto wake. Kama ambavyo hakuna taarifa za uhakika kuhusiana na mwaka aliozaliwa. Hata hivyo inaelezwa kuwa, aliaga dunia tarehe 14 Mfunguo Mosi Shawwal 573 Hijria.

Kinachojulikana kuhusiana na kipindi cha utoto wa Qutub al-Ravandi pamoja na familia yake ni kuwa, baba na babu yake walikuwa miongoni mwa Maulamaa wakubwa katika zama zao, ambapo Said alisoma masomo ya msingi kwa baba yake. Baada ya hapo akaanza kuhudhuria darsa na masomo ya walimu wakubwa katika zama hizo kama Abu Ali Tabarsi, Imaduddin Tabari na Sayyid Murtadha Razi. Baadaye alifanya safari na kuelekea katika mji wa Qum akiwa na lengo la kwenda kujiendeleza zaidi kielimu. Katika zama hizo mji wa Qum ulikuwa kitovu cha makao makuu ya fikihi ya Kishia na sehemu ya masomo na vikao vya elimu vya walimu watajika. Bidii na hima kubwa ya masomo aliyokuwa ilimfanya Qutub al-Ravandi kwa kipindi kifupi tu kuchomoza na kuwa shakhsia mashuhuri katika ulimwengu wa Kishia.

Kaburi la Allamah Qutub al-Ravandi katika haramu ya Bibi Maasuma AS

 

Kwa upande wa kifikra, Qutub al-Ravandi alikuwa mfuasi wa wasomi na waazuoni ambao harufu nzuri ya matunda yao ilisikika kwa wanadamu kwa miaka mingi. Fikra za shakhsia wakubwa wa Kiislamu kama Sheikh Saduq, Sayyid Murtadha, Sayyid Radhii na Sheikh Tusi zilikuwa na nafasi katika fikra na mitazamo yake. Qutub al-Ravandi alisikia na kunukuu hadithi na riwaya kutoka kwa wasomi wakubwa wa hadithi katika miji ya Isfahan, Khorasan na Hamadan na hilo linaweza kuonekana wazi katika safari za kielimu alizozifanya katika miji na maeneo mbalimbali. Kwa kuzingatia suhula chache zilizokuwa katika zama zile, kufanya safari mbalimbali za kielimu kwa ajili ya kwenda kustafidi kwa karibu kwa wanazuoni wakubwa na kupata vyanzo vya kielimu kwa wasomi lilikuwa jambo la dharura na la lazima.

 

Wapenzi wasikilizaji, moja ya mambo yanayomtofautisha Qutub al-Ravandi na wasomi wengine ni ukosoaji wake mzuri na wa mahala pake kwa mitazamo na nadharia za wanazuoni na maktaba nyingine za kifikra. Fikra yake ya ukosoaji sio tu kwamba, ilikuwa ikisaidia kukua kwa elimu, bali kwa ukosoaji huo alikuwa akibainisha nukta tata na kuondoa udhaifu katika nadharia hizo jambo lililokuwa likisaidia kukua kwa elimu.

Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali. Moja ya vitabu vyake ni Tahaafatul Falasifah ambapo ndani yake ameleta mitazamo na migongano ya baadhi ya wanafalsafa. Kitabu kingine cha Qutub al-Ravandi ni Tafsirul-Qur’ani wa Taawil al-Ayaat. Katika kitabu kitabu hiki, mwanazuoni huyu anabainisha Sabab al-Nuzul yaani sababu za kushuka Aya za Qur’ani.

Kkaburi la Qutub al-Ravandi

 

Kitabu chake kingine ni Kharaij Wa Jaraih ambapo ndani ya kitabu hiki Qutub al-Ravandi anabainisha masuala mbalimbali ya teolojia na fikihi na sehemu muhimu ya kitabu hiki inabainisha miujiza ya Mtume Muhammad. Mwanazuoni huyo aliweza kulea na kutoa wanafunzi wengi ambao waliondokea kuwa wanazuoni wa kutegemewa na Umma wa Kiislamu. Miongoni mwa wanafunzi wake mahiri ni mwanawe Hussein bin Said Hibatullah Ravandi. Aidha Ibn  Shahar Ashoub Mazandarani ni mwanafunzi mwingine mkubwa wa Qutub al-Ravandi ambaye aliondokea kuwa mwanazuoni mahiri wa elimu ya Fikihi na Tafsiri wa Kishia katika karne ya Sita Hijria ambaye tutamzungumzia katika kipindi chetu kijacho.

Hatimaye Allama Qutub al-Ravandi aliaga dunia tarehe 14 Mfunguo Mosi Shawwal 573 Hijria baada ya kuishi umri uliojaa fadhila na juhudi kubwa na mtawalia za kueneza elimu. Mwanazuoni huyu amezikwa jirani na Haram ya Bibi Fatma Maasumah mjini Qum. Baada ya karne 8 wakati Haram ya Fatma Maasuma (AS) ilipokuwa ikifanyiwa marekebisho kaburi la Allama Qutub al-Ravandi lilifukuliwa kwa bahati mbaya. Waliokuweko walipatwa na mshangao mkubwa baada ya kupata mwili wa mwanazuoni huyu ukiwa mzima kabisa baada ya miaka 800. Maulama na watu wa kawaida wakatoa ushahidi wakisema kwamba, mwili wake umebakia kama vilivyobakia vitabu na athari zake.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umekomea hapa ambapo tumezungumzia kwa mukhtasari maisha, athari na mchango wa Said bin Hibatullah al-Ravandi Kashani, mashuhuri kwa Qutub al-Ravandi. Tukutane tena wiki ijayo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags