Dec 28, 2020 08:27 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Disemba 28

Hujambo mpenzi mwanaspoti wa na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.

Iran yaibuka ya 3 mashindano ya dunia ya chesi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya tatu katika Mashindano ya Kimataifa ya Mabingwa wa Sataranji ya Vijana yaliyofanyika Georgia kwa njia ya intaneti. Fainali ya mashindano hayo ya dunia ilifanyika Jumanne iliyopita ya Disemba 22. Wanasataranji saba wa Kiirani wakiongozwa na kocha Mehrdad Ardeshi walimaliza katika nafasi ya tatu katika mashindano hayo yaliyowavutia wachezaji chesi zaidi ya 1,300 kutoka nchi 114 duniani.

Mchezo wa chesi (sataranji)

 

Marekani imetwaa nafasi ya kwanza huku India ikimaliza ya pili katika mashindano hayo yanayofahamika kwa Kimombo kama World Junior Chess Championship. Muirani Sina Movahedan ametwaa medali ya dhahabu katika mashindano hayo, huku mwenzake Amir Reza Pour-Agha Bala akitia kibindoni medali ya fedha.

Soka: Iran U-16 yaicharaza Tajikistan

Timu ya taifa ya soka ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 16 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeicharaza Tajikistan bao 1-0 katika mchuano wa kirafiki Jumamosi. Katika mchuano huo uliopigwa katika mji wa Dushanbe, mabarobaro hao wa Iran walipata ushindi huo hafifu licha ya kuupigia ugenini. Balozi wa Iran mjini Dushanbe, Mohammad-Taqi Saberi alishuhudia mchuano huo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Tajikistan.

Kabla ya mchuano huo, Iran ilikuwa imeibanjua Tajikistan mabao 4-1 katika mchuano wao wa kwanza wa kirafiki. Licha ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA kufuta fainali za Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17 na 20, mwaka ujao 2021, lakini Iran inashiriki mechi hizi za kirafiki kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi zijazo za kimataifa.

Fainali Cecafa ya Vijana U-17

Timu ya taifa ya soka ya Uganda ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 17 ndio mabingwa wa kandanda katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati. Hii ni baada ya kuichachafya mahasimu wao wa Tanzania mnamo Disemba 22 katika mchezo wa fainali ya michuano ya kieneo ya Cecafa iliyoanza kufanyika tangu Disemba 12 nchini Rwanda. Tanzania iligaragazwa na The Cubs ya Uganda inayonolewa na Hamza Lutalo mabao 3-1 katika fainali hiyo iliyopigwa Jumanne ya wiki iliyopita. Tanzania ilitinga hatua ya fainali baada ya kupata ushindi kwa penalti wa mabao 4-3 dhidi ya Ethiopia, mchezo uliochezwa Disemba 20 nchini Rwanda.

Mashirikisho ya Soka ya nchi wanachama wa CECAFA

 

Waganda hao walianza vyema mashindano hayo ya kikanda kwa kuicharaza Kenya mabao 5-0 kabla ya kuitia skulini Ethiopia kwa kuichapa mabao 3-0 katika michuano ya makundi. Licha ya kupoteza mchezo huo, lakini timu ya taifa ya Tanzania U 17  imejikatia tiketi ya kushiriki mechi za Afcon 2021 nchini Morroco. Licha ya kuwa mwenyeji, lakini Rwanda imevuta mkia katika Kundi A, nyuma ya Tanzania na Djibouti. Inaelekea kuwa Uganda ni moto wa kuotea mbali katika soka la kieneo, kwa kuzingatia kuwa, wamewahi kutwaa mataji ya CECAFA U-15 ya wavulana, CECAFA U-17 ya wasichana, CECAFA U-17 wavulana, CECAFA U-20 wavulana na CECAFA Senior Challenge Cup (Kombe la Chelenji), huku klabu ya KCCA FC ya nchi hiyo ikitamalaki CECAFA Kagame Cup.

Mechi za Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho

Klabu ya Simba ya Tanzania ilikuta ijikiwaa kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya timu hiyo kufungwa bao 1-0 na FC Platinum ya Zimbabwe kwenye mechi iliyochezwa katika uwanja wa taifa wa Zimbabwe. Licha ya Simba kujitahidi kupambana, goli lililofungwa na Perfect Likwende katika dakika ya 17 kutokana na mabeki wa Simba kuzidiwa ujanja, lilifanya mechi hiyo ikamilike kwa Simba kupoteza mchezo wao wa kwanza. Simba sasa wana kibarua kigumu kwenye mchezo wa marudiano unaotarajiwa kuchezwa Januari 5 katika uwanja wa Mkapa, na inatakiwa kushinda kwa magoli zaidi ya mawili, la sivyo safari yake itakuwa imefika mwisho. Simba ilitinga hatua hii ya kwanza baada ya kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya Plateau FC ya Nigeria katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa New Jos Nigeria. Katika mchezo wa pili Uwanja wa Mkapa, Simba iliweza kulinda ushindi wake na kufanya dakika 90 kukamilika kwa sare ya bila kufungana.

Kogalo ilipocheza na Zamalek huko nyuma

 

Mbali na hayo, magoli yaliyofungwa na Sixtus Sabilo katika dakika ya 14, na Stephen Sey katika dakika ya 31 yaliipa Namungo FC ya Tanzania ushindi wa 2-0 dhidi ya Al Hilal Obayed ya Sudan, kwenye mchezo wa kwanza Raundi ya Pili Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa kwenye uwanja wa Chamanzi jiji Dar es salaam. Ushindi huo umeiweka timu hiyo katika nafasi nzuri, kwani sasa inahitaji sare ugenini au kufungwa si kwa zaidi ya tofauti ya bao moja ili kusonga mbele, ambako watamenyana na moja ya timu zitakazotolewa Ligi ya Mabingwa kuwania kucheza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho. Kama ilivyo katika Ligi ya Mabingwa, Hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho huhusisha pia timu 16 zinazogawanywa kwenye makundi manne.

Huku hayo yakiarifiwa, klabu ya Gor Mahia ya Kenya ilidhalilishwa kwa kuchabangwa mabao 6-0 iliposhuka dimbani kuvaana na klabu ya CR Belouizdad ya Algeria siku ya Jumamosi. Gor walilishwa kichapo hicho cha mbwa wakiwa ugenini katika Uwanja wa  Stade du 5 Juillet 1962, katika mchezo wa hatua ya makundi ya CAF Champions League. Kiungo wa kati wa Waarabu hao, Amir Sayoud alipaicha wavuni mabao 3 ya hatrick likiwemo la penati. Mabao mengine matatu yaliyoungwa na Hamza Bellahouel, Larbi Tabti na Maecky Ngombo yalilizamisha kikamilifu jahazi la Kogalo ambao hawakupata japo goli la kufutia machozi.

Mabingwa hao wa Kenya ambao wanafahamika kwa jina la utani kama Sirkal wamejiweka katika mazingira magumu, watakapokutana tena na Waarabu hao wa Algeria katika mchuano wa mkondo wa pili katika Uwanja wa Taifa wa Nyayo jijini Nairobi mnamo Januari 6. Iwapo watazabwa tena, basi hawatakuwa na budi kushushwa kwenye Kombe la Shirikisho la CAF.

Mabingwa wa soka Afrika, TP Mazembe

 

Katika matokeo mengine, klabu ya Al-Ahly ya Misri wameanza vizuri kampeni za kutwaa ubingwa wa mashindano haya ya kikanda, baada ya kuifyatua AS Sondiep ya Niger bao 1-0 Jumatano, wakati ambapo mabingwa mara tano, TP Mazembe ya Kongo DR, ilikuwa inaipepeta Bouenguidi ya Gabon 2-1. Hata hivyo mchuano uliowawacha wengi vinywa wazi ni ule kati ya Stade Malien ya Mali na Waydad Athletic ya Morocco, ambapo Waarabu walikubali kichapo cha bao 1-0. Kadhalika Al Ahly Benghazi ya Libya iliwashangaza wengi ilipoilazimisha sare tasa mabingwa mara nne wa taji hili la kibara, Esperence ya Tunisia katika mji mkuu wa Misri, Cairo. Wakati huohuo, Al-Hilal Omdurman ya Sudan iliiaibisha Asante Kotoko ya Ghana kwa kuibamiza goli 1-0, huku hatrick ya  Saifeldin Bakhit wa Al-Merreikh ya Sudan ikitosha kuzima mchecheto wa Enyimba ya Nigeria iliyochachawizwa mabao 3-0.

……………………TAMATI…………………