Feb 09, 2021 18:39 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (20)

Nina wingi wa matumaini kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni katika sehemu nyingine mfululizo huu wa Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambao huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.

 

Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Khajeh Nasir al-Din Tusi mmoja wa wanazuoni na wasomi wakubwa na mashuhuri wa Kishia katika karne ya 7 Hijria. Tulieleza kwamba, Nasir al-Din Tusi, alikuwa mwanafalsafa, mwanateolojia, fakihi, mwanahisabati na mnajimu mkubwa wa Kiirani wa karne ya 7 Hijria na ndiye aliyeasisi kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kuangalilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maraghe. Tulibainisha pia kwamba, msomi huyo ameacha athari nyingi za kielimu hususan katika nyanja za hisabati na nujumu. Sehemu ya 20 ya kipindi chetu hiki juma hili, itaendelea kumzungumzia msomi na mwanazuoni huyu. Endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki. ***

 

Mbali na nafasi muhimu na mchango mkubwa wa Khajeh Nassir al-Din Tusi katika ulimwengu wa elimu na fikra katika karne ya saba Hijria, nafasi ya mwanazuoni huyu katika uga wa siasa hasa juhudi zake za kulinda maisha ya Waislamu katika zama za uvamizi na udhibiti wa Mongolia, ni jambo la kupigiwa mfano na la kuzingatiwa mno.

Khajeh Nassir al-Din Tusi

 

Mchango na mbinu ya Nasir al-Din Tusi katika zama za utawala wa Mongolia uliofanya mauaji na uharibifu mkubwa, ilikuwa nuru ya matumaini katika nyoyo zilizokuwa na giza totoro. Uwepo wa msomi na mwanazuoni huyo kwa hakika ulikuwa na nafasi muhimu mno. Hiyo ilitokana na kuwa, Nasir al-Din Tusi alikuwa mfuasi wa viongozi Maasumina AS kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume SAW, ambapo akitumia elimu yake, tadibiri na maarifa aligeuka na kuwa mlinzi imara wa jamii ya Kiislamu pamoja na athari za Kiislamu. Katika mazingira kama haya ambapo jamii ilikuwa katika kilele cha kukata tamaa, mwili wa Umma wa Kiislamu ukapata roho na matumaini mapya hususan ulimwengu wa Kishia.  Mbinu aliyokuwa akiitumia Khaje Nasir al-Din Tusi haikuwa na manufaa makubwa wakati huo tu, bali hata baadaye; kwani akitumia upeo wa hali ya juu wa kifikra aliokuwa nao baina ya viongozi na watawala wa Kimongolia aliweza kulinda na kuhifadhi maslahi ya Waislamu. Tadibiri na mipango yake, iliweza mara chungu nzima kuziokoa na mauti roho za watu na maulamaa wengi. Aidha wananchi na maulamaa wengi walifanikiwa kuachiliwa kutoka gerezani.

Baada ya mashambulio mawili ya Mongolia dhidi ya Iran na kuharibiwa miji sambamba na kuuawa kwa umati wananchi wasio na hatia, Khajeh Nasir al-Din Tusi alihamia katika ngome za Waismailia kwa ajili ya kuokoa maisha yake. Ngome hizo kutokana na kuwa imara na madhubuti, yalikuwa maeneo salama na amani kulingaanisha na miji mingine.

 

Wakati utawala wa Mongolia uliposhambulia ngome hizo, Khajeh Nasir al-Din Tusi ambaye alikuwa ameushuhudia uharibifu na ukatili wa askari hao huko Neishabour na Khorasan, alifahamu kwamba, kukabiliana na askari kama hao wamwagaji damu ni jambo lisilowezekana. Hivyo basi ndio maana alikuwa akiamini kwamba, njia pekee ya kuokoka ni kujisalimisha na kuwa pamoja nao. Ni kutokana na ukweli huo ndio maana alikuwa akiwataka raia na viongozi kufanya hivyo hivyo na kwa utaratibu huo akawa akifanya juhudi za kupunguza maafa na uharibifu zaidi. Kama ilivyotokea katika shambulio la Hulagu Khan mtawala wa Mongolia dhidi ya maeneo ya Waismailia, mtawala wa mwisho wa ngome za Ismailia alikubaliana na pendekezo la Khaje Nasir aal-Din Tusi ambapo alijisalimisha pamoja na mwanazuoni huyo na kwa utaratibu huo wakafanikiwa kuokoa maisha yao.

Khajeh Nassir al-Din Tusi

 

Lengo la Khajeh Nasir al-Din Tusi la kujisalimisha lilikuwa ni kulinda roho za Waislamu na kuandaa fursa kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya hali hiyo iliyokuwa mbaya na isiyoridhisha. Jeshi la Khawarazmshahiyan na Ukhalifa wa Abbasiya walishindwa kusimama kidete na kukabiliana na mashambulio ya Mongolia, lakini kwa kutumia mbinu, fikra na tadibiri hiyo pamoja na uchaji Mungu waliokuwa nao walifanikiwa kuokoa roho nyingi za Waislamu sambamba na kuokoa utamaduni na elimu za Kiislamu zisiteketezwe na kuangamizwa.

Baada ya utawala wa Mongolia kushika hatamu za uongozi na kuanza kutawala badala ya utawala wa Khawarazmshahiyan, Nasir al-Din Tusi hakusitisha juhudi zake bali alifanya kila awezalo kupenya na kuwa na ushawishi baina ya watawala na viongozi wa Mongoliaa na kubadilisha fikra na mitazamo yao. Kiasi kwamba, aliweza mara nyingi kuokoa roho za wanazuoni, akapelekea kuachiliwa huru wafungwa wengi sambamba na kuzuia kuporwa mali za Waislamu.

 

Muamala na utendaji wa Nasir al-Din Tusi, kila siku ulipelekea hadhi, heshima na nafasi yake miongoni mwa watu iongezeke siku baada ya siku na kuondokea kupendwa mno. Katika upande mwingine, Hulagu Khan na Ilkhan Moghul walipofahamu na kudiriki elimu na maarifa makubwa aliokuwa nayo Nasir al-Din Tusi katika masuala ya jamii, hivyo walikuwa wakimtukuza na kumthamini mno, kiasi kwamba, ilifikia wakati hawakuwa tayari kufanya jambo pasi na kushauriana naye. Kipaji na maarifa aliyokuwa nayo katika uga wa siasa na masuala mbalimbali vilimfanya atumie elimu aliyokuwa nayo na hivyo kupenya katika moyo wa utawala wa Mongolia. Watawala wa Mongolia walikuwa na mapenzi makubwa na watabiri na wanajimu. Kwa msingi huo Nasir al-Din Tusi ambaye mwenyewe alikuwa amebobea na kutabahari katika elimu ya nujumu alitumia vyema fursa hiyo na kuweza kupenya katika akili na fikra za Hulagu Khan, kiasi kwamba, mtawala huyo hakuwa akipanda kipando chake kwa ajili ya kuelekea safarini bila ya idhini ya mwanazuoni huyo na alikuwa akitumia fedha mahala popote ambapo Nasir al-Din alikuwa akimtaka na kumueleza.

Khajeh Nassir al-Din Tusi

 

Baadaye Nasir al-Din alikubali kuchukua jukumu la uwaziri na mshauri wa watawala wa Mongolia sambamba na kukubali kuwa msimamizi wa Waqfu na mali za Waislamu. Kwa utaratibu huo akatumia nafasi na vyeo alivyokuwa navyo kwa ajili ya kueneza madhehebu ya Shia na kuimarisha elimu za maktaba hii.

Nasir al-Din Tusi alisifiwa na kuheshimiwa hata na wanazuoni wa Kisuni. Wanazuoni wakubwa wa Kisuni walikuwa wakimheshimu mno na kumtaja kama mtu aliyekuwa amebobea kielimu, mlinzi wa elimu, mnyenyekevu, mwenye kauli njema, anayeamiliana vyema na watu, mwanasiasa na mtu mwenye hadhi na daraja ya juu na nadharia katika masuala mbalimbali ya Kiislamu.

Hatimaye Khajeh Nasir al-Din baada ya kuishi umri uliojaa baraka, juhudi na idili isiyochoka aliaga dunia tarehe 18 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 672 Hijria katika mji wa Baghdad. Allama Hassanzadeh Amoli, msomi na fakihi mahiri wa zama hizi wa Kiirani ameandika hivi kuhusiana na Nasir al-Din Tusi: Mwandishi wa vitabu vyote hivi katika falasafa, hisabati, fikihi, Usul al-Fikih na mjenzi wa kituo cha kutazamia mwezi, jua na nyota cha Maraghe bila shaka ni mwalimu wa mwanadamu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo siku na wasaa kama wa leo. Ahsanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.

Tags