Mar 12, 2021 15:46 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (21)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni katika sehemu nyingine mfululizo huu wa Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambao huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.

Vipindi vyetu viwili vilivyotangulia vilimzungumzia Khajeh Nasir al-Din Tusi mmoja wa wanazuoni na wasomi wakubwa na mashuhuri wa Kishia katika karne ya 7 Hijria ambaye alibobea katika falsafa, teolojia, fikihi, hisabati na nujumu. Nasir al-Din Tusi ndiye mwasisi wa kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kuangalilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maraghe. Tulibainisha pia jinsi tadibiri na mipango yake, ilivyoweza mara chungu nzima kuziokoa na umauti roho za watu na Maulamaa wengi wakati wa utawala wa Mongolia. Sehemu ya 21 ya kipindi chetu juma hili itazungumzia maisha ya Allama Hili pamoja na mchango na athari zake za kielimu.  Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Sheikh Jamal al-Din Hassan bin Yusuf Hilli mashuhuri kwa lakabu ya "Allama Hilli" fakihi na mwanateolojia wa Kishia aliishi katika karne ya Nane Hijria na ameandika zaidi ya vitabu 120 katika taaluma mbalimbali za elimu ya dini. Baadhi ya athari na vitabu vyake ni mitaala ya masomo katika Vyuo Vikuu vya Kiislamu (Hawza).  Allama Hilli alihesabiwa kuwa mtu aliyekuwa na kipaji kikubwa cha elimu katika zama zake na aliyekuwa akifanya hima kubwa ya kubainisha misingi ya kiitikadi ya Kishia kwa kutegemea misingi ya kiakili. Mamujtahidi na wasomi wapatao 500 wamehitimu katika masomo na vikao vya elimu vya Allamah Hilli. Msomi huyu alikuwa na mchango mkubwa katika kueneza madhehebu ya Shia pamoja na maarifa na mafundisho ya Ahlul-Biti (AS) na anaweza kutajwa kama ni mhuishaji wa athari za Kishia. Alifanya midahalo na mijadala mingi mno na Maulamaa wa Kisuni ambapo vitabu vyake vingi vinavyobainisha misingi ya Ushia na majibu yenye hoja na mantiki kwa wapinzani wa Ushia katika kipindi chote cha maisha yake ni ushahidi wa wazi wa jambo hili.

Allama Hilli

 

Allama Hilli alizaliwa usiku wa tarehe 29 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 648 Hijria katika familia ya kielimu na iliyosifika kwa maadili mema. Mama yake alitokana na familia ya elimu na iliyotambulika kwa wema na tabia njema na alikuwa ni dada yake Muhaqiq Hilli mwanazuoni mwingine mashuhuri wa Kishia. Baba yake naye alikuwa mmoja wa wasomi na wanazuoni wa fikihi waliokuwa mahiri katika zake katika mji wa Hillah. Allamah Hilli alikipitisha kipindi cha utoto wake akiwa chini ya malezi na mafundisho ya wazazi wake sambamba na mjomba wake aliyekuwa msomi stadi pia yaani Muhaqiq Hilli. Akili na kipaji kikubwa cha kufahamu mambo alichokuwa nacho pamoja na hima na juhudi kubwa katika masomo, viliwashangaza wengi ambapo akiwa katika rika la ujana na kuinukia, alikuwa tayari na ufahamu mkubwa katika elimu na taaluma nyingi.

 

Kipindi cha utoto cha Jamaluddin Hassan kilisadifiana na zama za hujuma na mashambulio ya kinyama ya watawala wa Mongolia dhidi ya ardhi za Kiislamu. Iran ilikuwa katika lindi la moto wa vita vya Mongolia na wananchi Wairaqi nao kutokana na hofu ya kukabiliwa na mashambulio ya Mongolia walikuwa  wakihama miji yao na kuiacha mitupu na kukimbilia majangwani. Mashia wa Iraq huko Najaf, na Kadhmein na wa miji mingine ya Iraq walikuwa wakimbilia hifadhi katika haram za Maimamu watoharifu AS.

Kufuatia mashambulio hayo, mji wa Baghdad ambao katika zama hizo ulikuwa kitovu na makao makuu ya utamaduni wa Kiislamu na Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) ulisambaratishwa. Hata hivyo, Maulamaa na wanazuoni wa dini hawakukaa bure mkabala na hatari zilizokuwa zikiikabili jamii ya Kiislamu; kwani walifanya hima kubwa kuzuia kuendelea umwagaji damu. Walifanya mazungumzo na makamanda na watawala wa Kimongolia. Kwa busara, hekima na maarifa ya mafakihi wa Kishia akiwemo baba wa Allamah Hilli yaani Sheikh Yusuf, amani na usalama vikarejea katika miji na hatua kwa hatua mji wa Hillah ukawa kimbilio la wasomi na wanazuoni.

Allama Hilli

 

Kipindi cha utoto cha Allamah Hilli kilikumbumbana na matatizo kama haya. Hata hivyo, mazingira hayo hayakuwa kizingiti kwake cha kustawi na kuchanua kielimu. Alianza kujifunza Qur’ani na masomo ya msingi kwa baba na mjomba wake aliyejulikana kama Muhaqiq Hilli. Kisha baadaye akajifunza elimu za teolojia, mantiki na falsafa kwa walimu wakubwa na watajika wa zama hizo hususan Khajeh Nassirddin Tusi.

Hima yake masomoni ilifanya akiwa katika rika la ubarobaro na hata kabla ya kufikia umri wa kubaleghe aweze kufikia daraja ya juu ya kielimu ya Ijtihad. Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana watu wa karibu na waliokuwa wakimzunguka walimpa lakabu ya Jamaluddin kwa maana ya sababu ya umaridadi na ujamali wa dini.

Akiwa na umri wa miaka 28, Allamah Hilli aliteuliwa kuwa kiongozi wa madhehebu ya Shia Imamiya, katika hali ambayo, katika zama hizo kulikuwa  na Maulamaa na mamujitahidi 400 waliokuwa wakiishi katika mji wa Hillah. Hii ilionyesha ni kwa jinsi gani Allamah Hilli alikuwa na itibari ya usomi na elimu baina ya wanazuoni wa zama hizo.

 

Allama Hilli alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kukurubisha madhehebu za Kiislamu. Tabia, mwenendo na kifua kipana alichokuwa nacho alimu huyu katika kupokea na kuheshimu mitazamo ya wengine vilimpelekea aandae vikao vya mijadala na midahalo ya kielimu katika anga isiyo na chuki wala uadui na hivyo kupatikana fursa ya kukosoa na kufanya uchunguzi. Katika chuo ambacho alikuwa amekianzisha Allama Hilli, walihudhuria hapo Maulamaa wa madhehebu mbalimbali ambapo licha ya kuweko hitilafu za kiitikadi baina yao walikuwa wakifundisha katika chuo hicho bila ya kuweko mizozo na mivutano. Licha ya kuwa Allama Hilli alikuwa akitangaza bayana na kutetea kikamilifu itikadi za Kishia, lakini alikuwa akisifiwa na kupongezwa na Maulamaa hata wasiokuwa Mashia. Hii inaonyesha ni kwa kiwango gani, alikuwa akiheshimiwa kutokana na daraja yake ya kielimu.

Kaburi la Allama Hilli

 

Kwa mfano Ibn Hajar al-Asqalani, msomi na mwanazuoni wa elimu ya fikihi na hadithi wa Kishafii anamtaja Allama Hilli kama "ishara za haki katika akili na maarifa" na anasifu hatua yake ya kuamiliana kwa ukarimu na Ibn Taymiyah, mmoja wa wanazuoni wa Kisuni aliyekuwa na misimamo ya kufurutu mpaka. Ibn Taymiyah alikuwa na mitazamo na fikra za kuchupa mipaka na za kitakfiri na akthari ya  Maulamaa wa Kiislamu Masuni kwa Mashia, walikuwa wakizitambua itikadi zake kuwa ni mbaya, zisizo faa na zilizo nje ya dini. 

Allama Hilli ameandika vitabu vingi sambamba na juhudi zake kubwa za kueneza utamaduni wa Kiislamu na kufundisha. Mwanazuoni huyo alifahamika pia kwa uchaji Mungu na kuipa mgongo dunia.

Mwanazuoni huyu aliaga dunia mwezi Muharram mwaka 726 Hijria katika mji wa Hillah. Mazishi yake yalihudhuriwa na umati mkubwa wa watu. Allama Hilli amezikwa katika mji wa Najaf Iraq jirani na Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib as.

Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umalizika, hivyo sina budi kukomea hapa kwa leo. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.

Ahsanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini

 

 

Tags