Mar 28, 2021 05:27 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (23)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Kwa moyo mkunjufu kabisa ninakukaribisheni kutegea sikio sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambao huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.

Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Muhammad bin Makki mashuhuri kwa lakabu ya al-Shahid al-Awwal aliyezaliwa mwaka 734 Hijria katia eneo la Jabal Amil nchini Lebanon. Jabal Amil ni eneo lenye milima na mandhari nzuri nchini Lebanon ambapo licha ya kuwa na masafa na kilomoita mrada ndogo, lakini liliondokea kuwa kitovu cha Maulamaa wengi wakubwa ambapo inanukuliwa kwamba, katika marasimu moja ya kidini zaidi ya Mamujitahidi sabini walikuwa wakihudhuria.

Tuliashiria kuwa, kitabu chake mashuhuri zaidi ni Lum’a Dimishqiah ambacho kimeeleza kwa mapana na marefu hukumu za ibada na amali (za kivitendo) katika Uislamu. Karibuni kutegea sikio kipindi chetu cha juma hili ambacho kitatupia jicho kwa mukhtasari historia, maisha pamoja na mchango wa kielimu wa Sayyid Haidar Amoli, arifu mkubwa wa Kishia na mfasiri mahiri wa Qur’ani Tukufu wa Kiirani, hii ikiwa ni sehemu ya 23 ya mfululizo huu.

Sayyid Haidar Amoli, ni msomi na arifu mkubwa wa Kishia, mfasiri mahiri wa Qur’ani Tukufu, mtambuzi wa hadithi na fakihi mtajika ambaye aliishi katika karne ya 8 Hijria. Alikuwa fakihi na mwanateolojia wa kwanza aliyeleta mfungamano mkubwa baina ya Ushia na Usufi. Alimu huyu licha ya kuwa na uwezo na taathira katika uga wa Irfani ya Kishia, hakufahamika sana miongoni mwa watu na hata baina ya wasomi. Henry Corbin mwanafalsafa Mwislamu wa Kifaransa na Profesa Othman Yahya ambao wote wawili walikuwa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Sorbonne cha Ufaransa, katika miongo kadhaa iliyopita walichapisha athari na vitabu kadhaa vya mwanazuoni huyu.

Kaburi la Sayyid Haidar Amoli katika mji wa Mazandar, Iran

 

Baada ya hapo, tabaka la wasomi na vyuo vikuu vya ulimwengu vikafahamu na kuelewa fikra na shakhsia ya Sayyid Haidar alizaliwa katika mji wa Amol ulioko Mazandar nchini Iran. Hiyo ilikuwa mwaka 720 Hijria. Sayyid Haidar alizaliwa katika familia ya kisharifu. Alifanikiwa kuzisoma vyema elimu rasmi katika zama hizo akiwa katika rika na ujana.

Kutokana na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa kile, kilichojulikana kama Irfani ya Kishia ya Maimamu 12, kando ya elimu rasmi alisoma pia na kujiendeleza kwa bidii katika uga wa misingi ya irfani. Akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu, alielekea katika miji ya Iran ya Isfahan na Khorasan ambayo katika zama hizo ilihesabiwa kuwa na vyuo muhimu zaidi vya kidini. Miaka mitano baadaye Sayyid Haidar Amoli akiwa tayari ametimiza miaka 25 na kutambuliwa kama alimu na mwanazuuoni mkubwa, alirejea mahala alipozaliwa. Umashuuhuri wa elimu yake ulimfikia gavana wa Tabaristan ambaye aliamua kumuita kijana huyu mwenye uwezo wa kielimu na kumpa heshima zote baada ya kumpa wadhifa wa uwaziri.

Katika zama hizo Sayyid Haidar Amoli mbali na kusifika kwa elimu na maadili mema, alikuwa na nafasi muhimu ya kijami na maisha mazuri na alikuwa akiishi maisha mazuri yenye kila kitu kimaada. Hata hivyo licha ya kuwa na hayo yote hakuthamini mambo hayo ya kidunia na badala yake aliona kama ni maisha machungu na yasiyo na maana yoyote.

Kwa msingi huo aliamua kuachana na yote hayo, kuanzia mali, utajiri, cheo na kadhalika na kuvaa vazi lenye thamani ndogo kabisa na kufunga safari ya kuelekea katika nyumba ya Mwenyezi Mungu yaani al-Kaaba. Aidha alifanya ziara katika maeneo na Haram za Ahlul-Baiti (as) na maeneo mengine matakatifu  huko Iraq, Palestina, Makka na Madina na kisha kuanza kipindi kipya cha maisha.

Baada ya kukamilisha ziara hizo, alirejea Iraq akiwa na umri wa miaka 30 na kuamua kuishi huko. Akiwa huko alihudhuria masomo kwa wasomi na wanazuoni wakubwa kama Fakhrul-Muhaqiqin yaani mtoto wa Allama Hilli, na Maulana Nasiruddin Kashani Hilli.

Alimu huyo ambaye alisoma vizuri misingi ya maarifa ya Kiislamu, sasa akawa ameingia katika uga na medani ya amani na kufanikiwa kuzikwea vizuri saraja za malezi ya kinafsi. Ikhlasi na nia safi aliyokuwa nayo katika kujikuribisha kwa Mwenyezi Mungu sambamba na irada imara na madhubuti ya kuacha kile kinachomuweka mbali na dhikri na utajo wa Mwenyezi Mungu, ni mambo ambayo kwa hakika yalikuwa kama kufunguliwa mlango mmoja  baada ya mwingine wa uhakika na ukweli.

Sayyid Haidar alikuwa akiamini kwamba, usufi wa asili ni ule ambao uko mbali na fikra zilizo kengeuka, kuchupa mipaka au kupuuza sana mambo na ambao unaambatana na asili ya Shia ambao kimsingi ndio ile sira ya Bwana Mtume SAW na dhuria wake yaani Ahlul-Baiti wake (as). Ambapo yote haya ni maktaba moja. Ushia wa kweli ni usufi na usufi wa kweli ni Ushia, hata kama kidhahiri huenda iisiwe hivyo.

Kama walivyo wanazuoni wengine wakubwa, Sayyid Haidar Amoli pia, hakubakia nyuma katika fani ya utunzi na uandishi wa vitabu. Ameandika vitabu vingi vingine vikiwa na malengo ya kubainisha uwepo wa pamoja baina ya Ushia na Usufi. Alifanya utafiti mkubwa katika maudhui zote mbili.

Wakati itikadi ya Sayyid Haidar ya kueleza ukuruba wa Ushia na Usufi ilipofahamika na Maulamaa wakubwa wa Kishia wakati huo huko Iraq, walijitokeza na kupinga vikali. Hta hivyo katika kuwajibu Sayyid Hadar Amoli alisema: “ Mimi nifahamu msichokifahamu nyinyi, na na juu ya kila elimu kuna elimu nyingine.”

Irfani ni moja ya matawi ya elimu za Kiislamu ambayo imejengeka juu ya msingi ya maarifa ya Qur’ani na mafundisho ya Ahlul-Baiti (as). Sayyid Haidar Amoli alikuwa akiwalalamikia na kuwakosoa baadhi ya misimamo ya uchupaji mipaka ya Masufi na akistafidi na mafundisho ya Ahlul-Baiti (as) alikuwa akibainisha na kuweka wazi misingi ya Irfani asili ya Kiislamu. Aliweza kufungamanisha  misingi ya Irfani na Wilaya (uongozi).

Ili aweze kufiki lengo lake kubwa alilokuwa nalo, alialifu na kuandika vitabu mbalimbali. Kitabu cha Jamiul-Asrar ni kitabu muhimu zaidi cha Sayyid Haidar Amoli ambacho kinabainisha na kuweka wazi vyanzo vilivyotumika kuelezea fikra bna mitazamo yake. Katika kitabu hicho amebainisha na kuweka suala muhimu kabisa Khatmul- Wilaya yaani mwisho wa Utume na anamkosoa Ibn Arabi msufi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu.

Kaburi la Sayyid Haidar Amoli katika mji wa Mazandar, Iran

 

Hakuna taarifa za kuaminika kuhusiana na kipindi cha mwishoni mwa umri wake na hata tarehe hasa aliyoaga dunia. Baadhi wanasea kuwa hilo lilitokana na kuwa, katika kipindi cha mwishoni mwa umri wake Sayyid Haidar alijitenga kabisa na jamii na kuishi maisha ya Kisufi akilea nafsi. Inasemekana kuwa, aliaga dunia mwaka 792 Hijria huku kukiweko na hitilafu kuhusiana na mahala alipozikwa. Baadhi wanasema amezikwa katika mji wa Hillah Iraq huku wengine wakisema amezikwa mahala alipozaliwa yaani Amol nchini Iran.

Wapenzi wasikilizaji muda wetu kwa leo umefikia tamati, hivyo tunalazimika kukomea hapa kwa leo nikitaraji kwamba, mmenufaika na yale niliyokuandalieni kwa wiki, basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri maishani.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh

Tags