Apr 14, 2021 02:21 UTC
  • Jumatano, Aprili 14, 2021

Leo ni Jumatano tarehe Mosi Ramadhani 1442 Hijria sawa na tarehe 14 Aprili mwaka 2021.

Leo ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria; mwezi ambao ndani yake iliteremshwa Qurani Tukufu. Ni mwezi wa rehma na baraka za tele. Katika kubainisha utukufu wa mwezi huu, Mtume Mtukufu SAW amesema, siku za mwezi wa Ramadhani ndizo siku bora zaidi kuliko siku nyingine zote na kuwataka Waislamu wachume na wafaidike kutokana na fadhila na baraka za mwezi huu. Allah SWT anasema: (Hakika tumeiteremsha (Qurani) katika usiku wa heshima. Na nini kitakujulisha usiku huo wa heshima ni nini? Laylatul Qadr (usiku huo wa heshima) ni bora kuliko miezi elfu.) Tukio la kuhuzinisha moyo la kuuawa shahidi Imam Ali AS na kuzaliwa mjukuu wa Mtume SAW,  Imam Hassan AS,  ni katika matukio muhimu yaliyotimia katika mwezi huu. Tunamuomba Allah SW atupe baraka za mwezi huu na kutujaliiia kuwa miongoni mwa wale wanaofadika na baraka zake. 

Katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kiliteremshwa kitabu cha Suhf cha Nabii Ibrahim AS. Jina Ibrahim limetajwa mara 69 katika Qur'ani Tukufu kwa heshima na taadhima ambapo maisha yake yameashiriwa kwa njia mbalimbali kama ibra na ruwaza njema kwa waumini. Mwenyezi Mungu amemtaja kuwa ni mtu mwenye kumuabdudu Mungu Mmoja. Alikuwa Nabii mkweli kama tunavyosoma katika Surat Maryam aya ya 41. Aidha Mwenyezi Mungu alimpa yeye na familia yake neema na mamlaka na utawala mkubwa kama tunavyosoma katika Suratun Nisaa aya ya 54. Kuna vitabu kadhaa vya mbinguni ambavyo waliteremshiwa Mitume kama vile Suhuf cha Ibrahim AS na Nuh AS, Taurati ya Musa AS na Injili ya Issa AS, na kitabu kilicho kamilika kati ya vyote hivyo ni Qur'ani Tukufu.

Siku kama ya leo miaka 1014 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria,  iliyopita alifariki dunia Ibn Sina maarufu kwa jina la Sheikhur Rais, tabibu, mtaalamu wa hisabati, falsafa na mnajimu mkubwa wa Kiirani. Ibn Sina alifariki dunia katika mji wa Hamadan ulioko magharibi mwa Iran akiwa na umri wa miaka 58. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana na akapata kusoma elimu za mantiki, uhandisi na utaalamu wa nyota. Baada ya kumtibu Nuh bin Mansur, mmoja wa wafalme wa Kisamani akiwa kijana, Ibn Sina alipata idhini ya kutumia maktaba kubwa ya mfalme huyo. Katika maktaba hiyo, Ibn Sina alipata kusoma vitabu vingi vya elimu tofauti. Abu Ali Sina alitokea kuwa msomi, mwandishi na mtafiti mashuhuri. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha "Shifaa" kinachohusu elimu ya falsafa, "Qanun" kinachohusu tiba na "Daneshnameh Allai".

Ibn Sina

Katika siku kama ya leo miaka 710 iliyopita, alizaliwa Ibn Khaldun, mtaalamu wa masuala ya kijamii, mwanasiasa na mwanahistoria Mwislamu. Ibn Khaldun alizaliwa huko Tunisia. Maisha ya Ibn Khaldun yanaweza kugawanywa katika sehemu tatu na sehemu ya kwanza aliitumia katika kusoma elimu tofauti. Alitumia sehemu ya pili ya maisha yake katika siasa na kuhudumia nyadhifa tofauti za utendaji na alifungwa jela kutokana na njama za maadui zake. Baada ya kuachiliwa huru Ibn Khaldun alijitenga na siasa. Hapo ndipo ilipoanza duru ya tatu ya maisha yake ambapo alijishughulisha na utafiti na uandishi. Alimu na msomi huyo alifariki dunia mwaka 808 Hijiria. 

Ibn Khaldun

Na tarehe 25 Farvardin miaka 33 iliyopita serikali ya wakati huo ya Iraq ilikiri waziwazi kwamba ilitumia silaha za kemikali katika vita vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi chote cha miaka minane ya vita hivyo Iran iliwasilisha mashtaka katika jumuiya za kimataifa kwamba Iraq inatumia silaha za kemikali dhidi ya wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu. Wakati huo Iraq haikukiri wala kukadhibisha habari hiyo. Hata hivyo katika siku kama hii ya leo wakati vita vilipokuwa vimepamba moto, serikali ya Baghdad ilikiri kwamba inatumia silaha za kemikali zikiwemo za gesi ya sumu na hatari ya haradali dhidi ya malengo ya kijeshi na kiraia ya Iran.

Takwimu zimeonesha kwamba utawala wa Baath wa Iraq ulifanya mashambulizi 3,500 kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote cha vita hivyo.

Iraq ilikiri kuwa imetumia silaha za sumu dhidi ya Iran

 

Tags