Apr 15, 2021 02:25 UTC
  • Alkhamisi tarehe 15 Aprili 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe Pili Ramadhani mwaka 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 15 Aprili

Siku kama ya leo miaka 1102 iliyopita alifariki dunia Abdur Rahman Zujaji Nahavandi aliyekuwa mwanafasihi, mtaalamu wa lugha na faqihi wa karne ya 4 Hijria katika mji wa Damascus. Alipata elimu kwa wanazuoni wakubwa na mashuhuri wa zama zake kama Ibn Dorayd na akafanikiwa kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa katika elimu hizo. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo wa Kiislamu ni "al Idhah".

Siku kama ya leo miaka 569 iliyopita, alizaliwa mchoraji na msanii mashuhuri wa kutengeneza vinyago wa Italia Leonardo da Vinci. Alionesha kipaji kikubwa cha kuchora akiwa bado mtoto mdogo na alikweya daraja za juu katika fani hiyo haraka mno. Mwaka 1506 Miladia da Vinci alichaguliwa kuwa mchoraji wa Mfalme Luis wa 12 kisha akawa mchoraji wa Mfalme Francis wa Kwanza.

Mbali na uhodari wake katika kuchora na kutengeneza vinyago, Leonardo da Vinci pia alisomea fizikia na hisabati. Miongoni mwa kazi zake mashuhuri ni michoro ya kanisa kuu la mji wa Milan, mchoro wa picha ya "Tabasamu la Jugund," picha ya Mona Lisa na ya Karamu ya Mwisho ya Issa Masih (as). Leonardo da Vinci alifariki dunia mwaka 1519 akiwa na umri wa miaka 67.

Leonardo da Vinci

Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita meli kubwa ya abiria ya Titanic ambayo ilitambuliwa kuwa nembo ya mafanikio makubwa ya viwanda vya meli vya wakati huo iligonga mwamba wa theluji na kughariki katika Bahari ya Atlantic, katika safari yake ya kwanza kutoka bandari ya Southampon nchini Uingereza ikielekea New York, Marekani. Zama hizo Titanic ilitambuliwa kuwa meli kubwa zaidi na ya kifahari kuliko zote duniani. Watengenezaji wa meli hiyo walikuwa akisema kuwa haiyumkini kughariki na kuzama. Wasafiri 705 tu kati ya abiria wake wote 2207 ndio waliookoa katika ajali hiyo. Ajali hiyo inatambuliwa kuwa mbaya zaidi ya baharini na iliyosababisha idadi kubwa ya vifo duniani.

Meli ya abiria ya Titanic

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Taqee Bafqi, alimu mkubwa na faqihi wa ulimwengu wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1292 Hijiria katika eneo la Bafq, mjini Yazd nchini Iran. Baada ya kuhitimu masomo ya awali ya dini ya Kiislamu alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Allamah Akhund Khorasani, Sayyid Mohammed Kazem Yazdi na Sayyid Ahmad Karbalai. Baada ya Ayatullah Taqee Bafqi kuishi mjini Najaf kwa kipindi cha miaka 19 alielekea Qum, Iran na kujikita katika kazi ya ufundishaji. Msomi huyo alikuwa miongoni mwa watu waliofanya maandalizi ya kumuhamishia Qum Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Haeri Yazdi na hatimaye kuasisi kituo kikubwa cha ya elimu. Ayatullah Sheikh Muhammad Taqee Bafqi hakuogopa chochote katika kuzuia machafu na ufuska wa utawala wa Shah hususan katika kupinga vikali tukio la kuingia wanawake wa ufalme huo katika Haram ya Bibi Fatimat Ma'asumah wakiwa katika mazingira machafu na bila ya vazi la hijabu. Kufuatia suala hilo tarehe Pili mwezi wa kwanza 1306 msomi huyo alikamatwa na maafisa wa utawala huo na kuteswa na kisha akabaidishwa Ray. Alirejea Qum baada ya mfalme Shah kukimbia nchi na alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 72. Ayatullah bafqi alizikwa katika Haram ya Bibi Fatimat Ma'asumah (as).

Ayatullah Sheikh Muhammad Taqee Bafqi

Tarehe 15 Aprili 1988, shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD lilimuua shahidi Khalil al Wazir maarufu kwa jina la Abu Jihad mwasisi na shakhsia nambari mbili wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina PLO huko Tunis, Tunisia. Abu Jihad aliongozana na wenzake nchini Misri, na huko wakaamua kuanzisha harakati ya mapambano dhidi ya Wazayuni, na kuipatia jina la Harakati ya Ukombozi ya Palestina PLO.

Khalil al Wazir

Na siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa kuanzisha Shirika la Biashara Duniani (WTO) nchini Morocco. Utangulizi wa kuasisiwa shirika hilo ulifanywa na Marekani na Uingereza wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kwa msingi huo, mwaka 1947 nchi 23 zilizoendelea zilitia saini makubaliano ya kuanzisha GATT. Makubaliano hayo yalisisitiza juu ya kufanyika mazungumzo ya kupunguza ushuru wa forodha, vipingamizi vya biashara na kuondoa vizuizi vya biashara huru. Baadaye jumuiya ya GATT ilibadilishwa jina na kuwa WTO na hati yake ilianza kutekelezwa Januari mwaka 1995. Hata hivyo Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimeliteka shirika hilo la kibiashara duniani na kulitumia kwa faida na maslahi yao wenyewe.

 

Tags