Apr 16, 2021 03:33 UTC
  • Ijumaa tarehe 16 Aprili 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 3 Ramadhani 1442 Hijria sawa na Aprili 16 mwaka 2021.

Katika siku kama ya leo miaka 1029 ilyopita inayosadifiana na tarehe 3 Ramadhani 413 Hijria, alifariki dunia Muhammad bin Nu'uman maarufu kwa lakabu ya Sheikh Mufiid, faqihi, mtaalamu wa elimu ya hadithi, Qurani Tukufu na historia ya Kiislamu. Sheikh Mufid alikuwa hodari na mwanafikra aliyepevuka, kwani aliweza kujibu masuala ya kifiqihi kwenye midahalo kulingana na madhehebu yoyote aliyotakiwa kufanya hivyo. Kutokana na uhodari wake huo, maulamaa wengi wa Kiislamu katika zama hizo walimpa lakabu ya Mufiid. Sheikh Mufiid ameandika vitabu vingi miongoni mwa hivyo, ni al Kalaam Fii Dalaailil Quran', al Arkaan' na˜Kashful Saraair'.

Siku kama ya leo miaka 177 iliyopita, alizaliwa mjini Paris Anatole France, mwandishi na malenga wa Kifaransa. Tangu akiwa kijana alivutiwa na elimu ya fasihi na uandishi ambapo kutokana na kipawa alichokuwanacho akatokea kupata umashuhuri katika uga wa mashairi na fasihi. Anatole France ameacha athari mbalimbali kikiwemo kitabu kinachoitwa 'Mfalme wa Sabai.' Mwaka 1914 Anatole France alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na kuandika kitabu alichokipa jina la 'Uasi wa Malaika' huku akifariki dunia mwaka 1924.

Anatole France

Miaka 132 iliyopita, Charles Spencer Chaplin mcheza filamu na msanii mashuhuri wa tasnia ya filamu alizaliwa katika viunga vya mji wa London, Uingereza. Alipokuwa mdogo, alianza na michezo ya kuigiza na kupata umashuhuri hatua kwa hatua. Mwanzoni mwa ujana wake, Chaplin alielekea nchini Marekani kwa lengo la kutengeneza filamu. Lakini kutokana na kutengeneza filamu ya ukosoaji na yenye kuonyesha mshikamano wake na matabaka ya kimasikini katika jamii ya Marekani, serikali ya nchi hiyo ilitoa amri ya kubaidishwa kwake mnamo mwaka 1952. Chaplin alikumbana na mazingira magumu ya kufanya shughuli zake nchini Marekani na hivyo akahamia nchini Uswisi pamoja na mkewe. Msanii huyo katika tasnia ya filamu alifariki dunia mwaka 1977.

Charles Spencer Chaplin

Miaka 73 iliyopita katika siku kama ya leo Wazayuni waliokuwa na silaha walishambulia kambi ya zamani wa askari wa Uingereza huko Palestina na kuua Wapalestina 90 na kujeruhi wengine wengi. Kwa upande mmoja, maafa hayo yalitokea wakati askari wa Uingereza walipokuwa wakiondoka katika kambi hiyo na kurejea nchini kwao; na kwa upande wa pili, Wazayuni walikuwa wameshadidisha mauaji hayo ya Wapalestina wasio na hatia kwa lengo la kuasisi dola haramu la Israel. Matokeo ya mauaji hayo yaliyofanyika kwa uratibu wa Uingereza, ilikuwa kuuawa idadi kubwa zaidi ya Waislamu wa Palestina na kutangazwa dola bandia la Israel mwezi mmoja baadaye.

Jinai za Wazayuni huko Palestina

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita ulitokea mlipuko mkubwa ulisababishwa na mtungi wa gesi na kusambaza moto kwenye mahema ya Mahujaji huko Mina kilomita 10 kutoka katika mji wa mtakatifu wa Makka. Mahujaji wasiopungua 343 walifariki dunia na wengine 1,290 kujeruhiwa katika tukio hilo. Aidha mahema yasiyopungua elfu sabini yaliteketea kwa moto huo. Hilo linahesabiwa kuwa tukio kubwa la pili la janga la moto kutokea wakati wa msimu wa Hija. Mnamo mwaka 1975, ulitokea moto mkubwa huko Mina nchini Saudi Arabia uliosababisha vifo vya maelfu ya Mahujaji na wengine wengi kujeruhiwa. Kutokana na matukio hayo, Saudi Arabia ililazimika kuweka katika eneo la Mina, mahema yasiyoshika moto ili kuepusha ajali za moto.

Mahema ya mahujaji huko Mina

 

Tags