Apr 17, 2021 13:03 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (24)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo hususan huko nyumbani Afrika Mashariki.

Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia na kutupia jicho kwa mukhtasari maisha ya Sayyid Haidar Amoli, msomi na arifu mkubwa wa Kishia, mfasiri mahiri wa Qur’ani Tukufu, mtambuzi wa hadithi na fakihi mtajika ambaye aliishi katika karne ya 8 Hijria.

Alikuwa fakihi na mwanateolojia wa kwanza aliyeleta mfungamano mkubwa baina ya Ushia na Usufi. Sayyid Haidar Amoli alikuwa akilalamikia na kukosoa baadhi ya misimamo ya uchupaji mipaka ya Masufi na akistafidi na mafundisho ya Ahlul-Baiti (as) alikuwa akibainisha na kuweka wazi misingi ya Irfani asili ya Kiislamu. Sehemu ya 24 juma hili na ijayo ya 25 juma lijalo zitatupia jicho kwa mukhtasari historia na maisha ya msomi mwingine wa Kishia ambaye si mwingine bali ni Ali bin Hassan Karaki mashuhuri zaidi kwa lakabu ya Muhaqqiq Thani au Muhaqqiq Karaki. Karibuni.

 

Ali bin Hassan Karaki alizaliwa mwaka 865 katika kijiji cha Karak moja ya vijiji na viunga vya Jabal Amil nchini Lebanon. Baba yake ambaye alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa Kishia, alimpatia mwanawe jina la Ali. Eneo la Jabal Amil linatambulika kama ardhi tukufu kutokana na sababu mbalimbali. Miongoni mwa sababu hizo ni uwepo wa haram za Mitume wengi, mawalii na shakhsia wakubwa waliozikwa katika eneo hilo.

Eneo la Jabal Amil nchini Lebanon

 

Ushia ulianza kuchomoza huko Jabal Amil katika nusu ya kwanza ya karne ya kwanza Hijria ambapo Mashia wenye ikhlasi kama Salman al-Farsi, Ammar Yassir na Abu Dharr al-Ghiffari walifanya hima kubwa ya kueneza mafundisho ya Ahlu Baiti (as) na Uislamu kwa ujumla katika eneo hilo. Yamkini uwepo wa Abu Dharr huko Jabal Amil katika kipindi cha kubaidishwa kwake ni jambo lililokuwa na taathira mno kwa wananchi. Miongoni wanazuoni mahiri wa Jabal Amil ni Sheikh Hurr Amili aliyeondokea kufahamika kwa uchaji Mungu na elimu katika ulimwengu wa Kishia.

Katika kitabu chake cha Amal al-Amal Fi Ulamaa Jabal Amil ametaja majina 100 ya wanazuoni na wasomi wa Kishia ambao asili yao ni Jabal Amil.

Ali bin Hassan Karaki mashuhuri kama Muhaqqiq Thani na Muhaqqiq Karaki, ni miongoni mwa Maulamaa wa Jabal Amil nchini Lebanon ambaye alikuja Iran kwa mwaliko wa mtawala wa wakati huo Shah Ismail Safavi na akawa na nafasi muhimu katika kueneza madhehebu ya Kishia.  Alimu huyo alilea wanafunzi wengi na akthari ya mafakihi na wanazuoni wa karne ya 10 Hijria walikuwa wanafunzi wake.

Chuo cha Kikuu cha Kiislamu cha Jabal Amil kinaweza kutajwa kama kituo cha kielimu kilichokuwa na taathira mno katika kuhuisha mafundisho ya Ahlu-Baiti (as). Kipindi kilichokuwa na harakati nyingi mno katika historia ya chuo hiki kinahusiana na karne ya nane mpaka ya 11 Hijria. Katika zama hizo, shakhsia wakubwa wa kielimu na wanazuoni wa fikihi wasio na mithili walichomoza na kudhihiri hapo ambapo miongoni mwao ni al-Shahid al-Awwal, al-Shahid al-Thani na Muhaqqiq Karaki. Aidha wanazuoni mahiri wa Jabil Amil walihajiri na kuja Iran na kuwa na nafasi muhimu na atharifu katika kueneza Ushia na mafundisho yake. Muhaqqiq Karaki alikuwa miongoni mwa wanazuoni hao.

Jamiul Maqasid fi Sherh al-Qawaid

 

 

Muhaqqiq Karaki au Muhaqqiq Thani alikipitisha kipindi cha utoto na kukua kwake katika familia ya kielimu. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi alijiunga na Chuo cha Karak na kuhudhuria masomo ya wanazuoni wakubwa wa zama hizo. Licha ya kuwa Karak kilikuwa kijiji lakini kilikuwa na chuo cha kielimu kilichokuwa na utajiri mkubwa wa elimu ambapo wanafunzi wa masomo ya dini walikusanyika hapo kutoka katika maeneo mbalimbali ya Lebanon.

Kipaji kikubwa cha kielimu pamoja na bidii isiyo na kifani aliyokuwa nayo alimu huyu, ni mambo ambayo yalimfanya achomoze na kuwa msomi mahiri katika kipindi cha rika la ujana. Alianza kufanya utafiti na uhakiki akiwa katika rika hilo katika taaluma za fikihi na hadithi, kiasi kwamba akapewa lakabu ya Muhaqqiq Thani yaani Mhakiki wa Pili. Mwanazuoni huyu anahesabiwa kuwa, msomi na mhakiki hodari na mahiri zaidi katika taaluma ya fikihi ya Ahlul-Baiti (as) baada ya Muhaqqiq Hili.

Mwanazuoni huyu ana vitabu 71 ambapo maarufu zaidi na ambacho kinahesabiwa kuwa dafina na Johari kubwa ni Sherh Kitab Qawaid Allamah Hilli ambacho kimeondokea kuwa mashuhuri zaidi kwa jina la Jamiul Maqasid fi Sherh al-Qawaid. Aidha Muhaqqiq Karaki anajulikana pia kwa jina la "Swahib Jamiul Maqaasid.

Kipindi fulani akiwa nchini Misri, msomi huyo aliweza kufahamu vyema fikra na mitazamo ya fikihi ya Kisuni. Baada ya kutoka Misri alielekea Iraq.

Muhaqqiq Karaki alikuja Iran katika kipindi ambacho haukuwa umepita muda mrefu tangu kutambuliwa rasmi madhehebu ya Kishia hapa nchini. Alipokuja Iran alichukua hatua kadhaa muhimu na athirifu zilizokuwa kwa maslahi ya Ushia hasa katika miji ya Khorasan, Isfahan na Qazvin.

Mwaka 929 Hijria, mwanazuoni huyo aliachana na nyadhifa rasmi katika utawala na kujishughulisha zaidi na ufundishaji katika Chuo Kikuu cha Kiislamu huko Najaf Iraq. Katika kipindi cha miaka sita cha kufundisha na kulea wanafunzi huko Najaf, alimu huyo aliweza kufunza na kulea wanafunzi mahiri ambao waliondokea baadaye na kuwa wasomi na wanazuoni watajika.

 

Moja ya mambo muhimu yaliyofanywa na Muhaqqiq Karaki nchini Iran ni kuimarisha vyuo vya kidini na kuvishughulikia kimaada na kimaanawi. Aidha alifanya marekebisho kuhusiana na upotofu kuhusu usufi ambao ulijitokeza katika zama hizo. Ni kwa fatuwa yake ambapo utawala wa Safavi ulichukua hatua ya kuvifunga vituo ambavyo vilikuwa vikifanya harakati zinazokinzana na sheria za Uislamu. Kuhuisha Swala ya Ijumaa na Swala za Jamaa nchini Iran ni miongoni mwa hatua nyingine zilizochukuliwa na msomi huyu. Alitoa amri ya kutumwa Masheikh katika miji na vijiji vyote kwa ajili ya kutoa majibu ya maswali ya kisheria ya wananchi na vilevile kuongoza Swala za Jamaa. Akiwa na lengo la kuhuisha nembo na madhihirisho ya Ushia na maktaba ya Ahlul-Baiti (as) katika jamii alifanya hima na juhudi kubwa ambapo baadhi yake ni kurejesha ibara za Ash'hadu anna Aliyan Waliyullah na Haiyalaa Kheiril Amal katika adhana na iqama ambazo zilikuwa zimeatolewa na kuachwa katika adhana na iqama kwa muda wa miaka 56 kuanzia kipindi cha utawala wa Tughril Bey Seljuki.

Shah Ismail Safavi

 

Nukta nyingine muhimu ya uwepo wa Muhaqqiq Karaki nchini Iran ni kuingia mwanazuoni huyu mkubwa wa kidini katika masuala ya kisiasa na kijamii. Alikuwa akiamini kwamba, kuendesha nchi na mambo ya wananchi kunapaswa kufanyika kwa mujibu wa dini na kwa uongozi wa fakihi aliyetimiza masharti. Mtazamo huu ndio ile nadharia ya Wilayatul-Faqih ambao unaaminiwa na wanazuoni wengi wa Kishia.

Wapaenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati. Msikose kipindi chetu cha juma lijalo ambapo tutabainisha nadharia na mitazamo ya mwanazuoni huyu.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Waabarakaatuh

Tags