Jun 25, 2021 03:27 UTC
  • Ijumaa tarehe 25 Jun 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 14 Dhulqaada 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 25 Juni mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 199 iliyopita kundi la watumwa wa Marekani wenye asili ya Afrika ambao waliachiwa huru na wamiliki wao wazungu wa nchi hiyo, walirejea Afrika na kuanzisha makazi katika ardhi ambayo leo hii inajulikana kama Liberia. Raia hao weusi wa Marekani walianzisha harakati ya ukombozi mwanzoni mwa karne ya 19 kwa lengo la kujiondoa utumwani na kuunda nchi yao. Kwa sababu hiyo kundi la Wamarekani weusi wenye asili ya Afrika lilihamia Magharibi mwa Afrika na kuasisi nchi ya Liberia kwa kusaidiwa na taasisi ya wahamiaji, baada ya kuwa utumwani kwa miaka mingi huko Marekani. Awali Liberia ilikuwa ikiendeshwa kama moja ya majimbo ya Marekani, lakini mwaka 1847 nchi hiyo iliasisi mfumo wa jamhuri na rais wake wa kwanza akawa Joseph Roberts, mtumwa kutoka jimbo la Virginia.

Bendera ya Liberia

Tarehe 4 Tir miaka 58 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini alihamishiwa katika kambi ya kijeshi ya Ushratabad baada ya kukamatwa na Shirika la Usalama la Shah maarufu kwa jina la Savak. Siku 40 baada ya kushikiliwa katika kambi hiyo, Imam Khomeini kwanza alipelekwa uhamishoni nchini Uturuki na mwaka mmoja baadaye akapelekwa Iraq. Katika kipindi chote cha miaka 13 ya kubaidishiwa nje ya nchi, Imam aliongoza harakati zake za mapinduzi kupitia wanafunzi wake waliokuwa wakiwasilisha ujumbe zake kwa wananchi ndani ya Iran. Februari mwaka 1979 Imam Ruhullah Khomeini alirejea nchini na kupokewa na watu milioni tano. Siku 10 baadaye Imam alifanikiwa kuuangusha utawala wa kifalme ulioiongoza Iran kwa kipindi cha miaka 2500. 

Imam Ruhullah Khomeini

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, yaani tarehe 25 Juni mwaka 1975, Msumbiji ilipata uhuru. Mwishoni mwa karne ya 15 kundi moja la mabaharia wa Kireno likiongozwa na mvumbuzi mashuhuri Vasco da Gama lilifika Msumbiji na kuanzia hapo mabaharia hao wakaanza kuikoloni nchi hiyo, ukoloni ambao uliendelea kwa karne tano. Wareno walianza kupora maliasili na utajiri wa Msumbiji na makumi ya maelfu ya wananchi wapigania ukombozi wa Msumbiji waliuawa wakitetea nchi yao.

Bendera ya Msumbiji

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita yaani tarehe 4 Tir 1367 Hijria Shamsia, ndege za utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq, kwa mara nyingine tena ziliwashambulia kwa mabomu ya kemikali wapiganaji wa Kiirani waliokuwa katika visiwa vya Majnun. Mamia ya wanajeshi wa Iran waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Saddam. Utawala wa zamani wa Iraq ulitumia silaha za maangamizi ya umati za kemikali tangu mwanzoni mwa vita vyake dhidi ya Iran mwaka 1359 Hijria Shamsiya, na kuzidisha matumizi ya silaha hizo sambamba na ushindi wa wapiganaji wa Iran.

Shambulizi la silaha za kemikali

 

Tags