Jul 22, 2021 02:30 UTC
  • Alkhamisi tarehe 22 Julai mwaka 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe 11 Mfunguo Tatu Dhulhija 1442 Hijria sawa na Julai 22 mwaka 2021.

Miaka 106 iliyopita katika siku kama hii ya leo, kulitokea vita maarufu vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Isonzo. Vita hivyo vilitokea sambamba na kujiri Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Vita vya Isonzo vilitokea katika maeneo ya milimani yaliyojulikana kwa jina hilo hilo nchini Italia. Vita hivyo vilikuwa baina ya jeshi la Italia na Austria. Watu wapatao 70,000 wengi wao wakiwa ni Wataliano waliuliwa katika vita hivyo. Pamoja na hayo, jeshi la Italia lilipata ushindi dhidi ya jeshi la Austria.

Vita vya Isonzo

Miaka 98 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 11 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja alifariki dunia Ayatullah Mirza Jawad Malaki Tabrizi, ustadhi mkubwa wa akhlaqi, msomi na arif wa Kiislamu. Alizaliwa katika mji wa Tabriz moja ya miji ya Iran na baada ya kukamilisha masomo yake ya msingi na ya kati alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Akiwa huko alihudhuria darsa za maustadhi mahiri katika zama hizo kama Haji Agha Reza Hamedani, Akhund Khorasani, Muhaddith Nuri na Akhund Hamedani. Mwanazuoni huyo mbali na kufundisha na kulea wanafunzi wengi hakuwa nyuma pia katika taaluma ya uandishi wa vitabu. Asraru Salat, al-Muraqabaat na A'amalu al Sunna ni baadhi tu ya vitabu vya Ayatullah Mirza Jawad Maliki Tabrizi.

Ayatullah Mirza Jawad Malaki Tabrizi

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita Mahakama ya Kimataifa ya Hague ilitupilia mbali mashtaka ya serikali ya Uingereza dhidi ya Iran baada ya hatua ya Tehran kutaifisha sekta ya mafuta hapa nchini iliyokuwa chini ya udhibiti wa makampuni ya Kiingereza. Tarehe 29 mwezi Esfand mwaka 1329 (20 Machi 1951) Bunge la Taifa la Iran lilitangaza habari ya kutaifishwa sekta ya mafuta na kukata mikono ya Uingereza katika sekta hiyo nchini Iran. Uingereza ilikuwa ikipata fedha nyingi kutokana na kupora utajiri huo na hivyo iliamua kufungua mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Hague. Uamuzi uliotoewa na mahakama hiyo kwa maslahi ya Iran ulizikasirisha Uingereza na Marekani ambazo mwaka mmoja baadaye ziliongoza mapinduzi na kuiondoa madarakani serikali ya Muhammad Musaddiq nchini Iran kwa shabaha ya kutwaa tena sekta hiyo ya mafuta ya Iran.

Mahakama ya Kimataifa ya Hague

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 22 Julai 1961, yalianza mapigano makali kati ya majeshi ya Ufaransa na Tunisia, baada ya vikosi vya Ufaransa kuishambulia bandari maarufu ya Bizerte iliyoko kaskazini mashariki mwa Tunisia. Mara baada ya Tunisia kujitawala kutoka kwa mkoloni Mfaransa mwaka 1956, mkoloni huyo aliendelea kuikalia kwa mabavu bandari ya Bizerte, na kuifanya kuwa kambi ya jeshi la anga la nchi hiyo. Hata hivyo majeshi ya Tunisia yalifanikiwa kuikomboa bandari hiyo kwenye mapigano hayo makali yaliyopelekea Watunisia 750 kuuawa. 

Bizerte

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 22 Julai 2003, waliuawa Uday na Qusay watoto wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq pambizoni mwa mji wa Mosul, kaskazini mwa Iraq. Uday na Qusay wakiwa wamefuatana na maafisa wa ngazi za juu wa Iraq walitoroka mjini Baghdad baada ya majeshi ya Marekani na Uingereza kuishambulia nchi hiyo mwezi Aprili 2003. Majeshi ya Marekani yalishambulia nyumba walimokuwa wamejificha watoto hao wa Saddam Hussein na kuwauwa pamoja na wasaidizi wao.

Uday na Qusay

Tarehe 22 Julai 2002, ndege za kivita za utawala wa Israel zilishambulia eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina, na kuua watu 16 na wengine 150 kujeruhiwa. Shambulio hilo la kushtukiza lililofanyika usiku, liliua watoto 9 wasiokuwa na hatia yoyote. Hali kadhalika miongoni mwa waliouawa shahidi katika shambulizi hilo ni Sheikh Swalah Shahadah, mmoja wa makamanda wa Brigedi ya Izzuddin Qassam akiwa pamoja na mke na binti yake.

Sheikh Swalah Shahadah

 

Tags