Jul 26, 2021 08:02 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Julai 26

Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu yaliyojiri viwanjani ndani ya siku zilizopita, ndani na nje ya Iran, hususan Michezo ya Olimpiki ya Tokyo, Japan.

Iran yaanza vizuri Michezo ya Olimpiki

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanza vizuri Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 iliyofungua pazia lake Ijumaa ya Julai 23 nchini Japan. Hii ni baada ya mlengaji shabaha stadi wa Iran kutwaa medali ya dhahabu katika mchezo wa kupiga shabaha kwa bastola umbali wa mita 10 kwa upande wa wanaume. Javad Foroughi mbali na kutwaa dhahabu, lakini ameweka rekodi mpya ya Olimpiki baada ya kuzoa pointi 244.8, alama 6.9 mbele ya Msabia Damir Mikec aliyeibuka wa pili na kuzawadiwa medali ya fedha. Raia wa China Panga Wei ambaye alitwaa medali ya dhahabu mwaka 2008, hakuwa na budi kuridhika na nafasi ya tatu na kutia kibindoni shaba. Wananchi wa Iran walimiminika mabarabarani kwa shangwe na vifijo kufurahia ushindi huo wa aina yake.

Foroughi alipopiga sijda ya kushukuru baada ya kuibuka kidedea Tokyo

 

Foroughi mwenye umri wa miaka 41 anakuwa mwanamichezo wa Kiirani mwenye umri mkubwa zaidi kutwaa medali katika michezo ya Olimpiki, akimpiku mnyanyua uzani Mahmoud Namjou ambaye alikuwa na miaka 38 alipotwaa medali ya shaba katika Michezo ya Olimpiki ya Melbourne mwaka 1956. Rais mteule wa Iran, Ebrahim Raisi amemnyooshea mkono wa tahania mlengaji shabaha huyo stadi wa Iran kwa kuiweka Jamhuri ya Kiislamu katika ramani ya dunia na kuvunja rekodi ya olimpiki. Raisi amesema anatumai kuwa wanariadha wengine wa Iran wataibuka washindi na kulipa fakhari taifa hili. Makumi ya wanariadha wa Iran wanashiriki katika michjezo mbalimbali jiji Tokyo, kuanzia mieleka, voliboli na unyanyuaji uzani. Wanariadha 25 kati ya 66 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walioko Japan walishiriki katika hafla ya ufunguzi wa mashindano hayo siku ya Ijumaa, ambapo walipiga gwaride kwa fakhari wakiwa wamenyanyua bendera ya nchi hii. Wanamichezo kutoka nchi 200 duniani wanashiriki mashindano hayo yaliyoakhirishwa kwa mwaka mzima kutokana na janga la Corona, na yatakayomalizika Agosti 8. Iran ilimaliza katika nafasi ya 25 katika Michezo ya Olimpiki ya Rio de Janeiro mwaka 2016, baada ya kuzoa medali 3 za dhahabu, moja ya fedha na 4 ya shaba.

Dondoo za Olimpiki

Mwanamichezo wa mchezo wa Judo wa Algeria ameamua kujitoa kwenye michezo ya Olimpiki ya 2020 Tokyo inayofunguliwa rasmi leo katika mji mkuu huo wa Japan, ikiwa ni harakati ya kutangaza mshikamano na Palestina na kupinga kuanzishwa uhusiano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, Fat-hi Nurin, mwanamichezo wa Judo kutoka Algeria alitangaza kujiondoa kwenye michuano ya Olimpiki baada ya kura ya duru ya pili ya utangulizi wa mashindano hayo katika uzito wa chini ya kilo 73 kumwangukia apambane na mshindani kutoka Israel. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Nurin, ambaye ni bingwa wa uzito huo nchini Algeria amechukua uamuzi huo wa kishujaa wa kukubali kukosa kushiriki mashindano makubwa zaidi ya michezo duniani ili kulalamikia hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni na vilevile kuonyesha mshikamano na wananchi madhulumu wa Palestina kama anavyosema.  

Judoka wa Kialgeria aliyekataa kupigana na Mzayuni

 

Algeria, kinyume na jirani yake Morocco, ni nchi inayopinga kuanzisha uhusiano wa aina yoyote na utawala haramu wa Israel na kuendelea kushikilia kila mara msimamo wake thabiti wa kuliunga mkono taifa la Palestina. Katika miezi ya karibuni, nchi za Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco zimechukua hatua ya kutangaza hadharani uamuzi wao wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, uamuzi ambao umekabiliwa na malalamiko makubwa na upinzani mkali wa makundi ya muqawama ya Palestina.

Mbali na hayo, ratiba ya michuano ya ndondi katika Michezo ya Olimpiki imetolewa huku mabondia wawili wa timu ya taifa Hit Squad ya Kenya, wakifuzu kiulaini kwa raundi ya pili. Mshindi wa medali ya dhahabu katika Mashindano ya Africa Zone 3 Championship nchini DRC Elly Ajowi na Elizabeth Akinyi wamefuzu hadi raundi ya pili bila jasho. Ajowi anayezichapa katika uzito wa heavy, ameratibiwa kupepetana na Cruiz Julio wa Cuba katika mzunguko wa pili siku ya Jumanne (Julai 27,2021). Siku hiyo ya Jumanne, Akinyi atakutana na Panguana Alcinda Helena wa Msumbiji kwa mara nyengine baada ya kukutana katika mashindano ya Africa Zone 3 Championship nchini DRC. Wakati huohuo, matumaini ya bondia Christine Ongare wa Kenya kunyanyua medali katika Michezo ya Olimpiki Tokyo Japan yaliyeyuka kama moshi baada ya kupoteza pigano lake. Ongare alishindwa na Magno Irish kutoka Ufilipino kwa alama 5-0 katika mrindimano ulioandaliwa katika ukumbi wa Kokugikan Arena. Matokeo haya yamezima kabisa ndoto ya Ongare kuwa mwanamke wa kwanza nchini kushinda medali katika Michezo ya Olimpiki. Kushindwa kwa Ongare ni pigo zaidi kwa kikosi cha Kenya, baada ya nahodha wake Nick Okoth kupoteza pigano lake pia alipovaana na Erdenebat Tsendbaatar wa Mongolia. Siku ya Jumamosi, kocha mkuu wa timu ya taifa ya ndondi Musa Benjamin alisema anaamini kuwa Okoth alishinda pigano lake dhidi ya rais huyo wa Mongolia. Kocha Benjamin amesema kunahitajika kuwa na semina kwa majaji kuhusu namna ya kutoa alama kwa sababu washiriki wanatoka katika mataifa mbali mbali yaliyo na mitindo yao ya kutoa alama.

Nembo ya Olimpiki Tokyo Japan

 

Hata hivyo, kocha Benjamin amesema hawana nia ya kukata rufaa dhidi ya matokeo haya hasa wakizingatia sheria na masharti ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kuhusu mashindano haya. Kwengineko, Ahmed Hafnaoui wa Tunisia aliduwaza wapinzani wake kwa kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya uogoleaji mtindo wa freestyle mita 400 kwenye Olimpiki katika ukumbi wa Aquatics Centre, Japan mnamo Jumapili. Mpiga mbizi huyo mwenye umri wa miaka 18 aliibuka mshindi licha ya kusajili muda wa chini zaidi kwenye hatua ya mchujo. Alimpiku muogoleaji nambari mbili Jack McLoughlin wa Australia kwa kuandikisha muda wa dakika 3:43.36. Kieran Smith wa Marekani aliridhika na nishani ya shaba. Ushindi huo ulizolea Tunisia medali ya tano ya dhahabu kwenye Olimpiki na ya tatu kutokana na mashindano ya uogeleaji. China kufikia sasa inaongoza kwa medali 6 za dhahabu, mbili za fedha na shaba 5, ikifuatiwa na Japan dhahabu 6, fedha moja na shaba moja, huku Marekani ikifunga orodha ya tatu bora kwa medali tano za dhahabu.

Simba bingwa Kombe la Azam

Klabu ya Simba ya Tanzania imetwaa ubingwa wa Kombe la Azam (ASFC) kwa msimu huu baada ya kuizaba Yanga bao 1-0 katika mechi ya fainali iliyopigwa jioni ya Jumapili ya Julai 25 kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma. Hii ni kwa mara ya pili mfululizo kwa Simba kubeba ubingwa huo kwani walifanya hivyo msimu uliopita kwa kuwafunga Namungo kwenye mchezo wa fainali iliyopigwa uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga. Hilo lijakuwa kombe la tatu kwa Simba msimu huu baada ya kubeba lile la Simba Super Cup, la Ligi Kuu Tanzania Bara na hili la ASFC. Kipindi cha kwanza kipimalizika kwa suluhu (0-0) huku Yanga wakiwa pungufu baada ya kiungo Tunombe Mukoko kuoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea faulo Nahodha wa Simba John Bocco.

Mnyama Simba akakabana na Yanga

 

Dakika ya 79 Taddeo Lwanga aliwafungia Simba bao la kwanza na la pekee katika mchezo huo baada ya kumalizia kwa kichwa kona iliyopigwa na Jose Miquissone na kuoneshwa kadi ya njano kwa kuvua flana wakati wa kushangilia. Muda huo jukwaa la Simba lilinyanyuka kwa shangwe huku lile la Yanga likipoa na katika jukwaa la pamoja linalotenganishwa na mlango wa kuingilia, mashabiki wa timu zote mbili walionekana wakirushiana chupa za maji. Pamoja na kufunga, pia kiungo wa Simba Lwanga ndiye aliibuka mchezaji bora wa mechi hiyo ya fainali.

……………………..TAMATI………..……

 

Tags