Sep 13, 2021 02:26 UTC
  • Jumatatu tarehe 13 Septemba 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 6 Safar 1443 Hujria sawa na Septemba 13 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1394 iliyopita, vilimalizika vita vya miaka 24 baina ya mfalme wa Iran na Roma. Khosrow Parvēz, mfalme wa Kisasani kwa kutekeleza mashambulizi mtawalia, aliweza kudhibiti maeneo ya Mesopotamia, Syria, Palestina, Misri na Asia Ndogo, na hivyo akawa ameweza kupanua wigo wa ushindi wake hadi kufikia Istanbul ya leo. Mwaka 591 Miladia, hatimaye amani ilifikiwa kufuatia kutiwa saini makubaliano baina ya mfalme Khosrow Parvēz na mfalme wa Roma. Hata hivyo tarehe Tano Juni mwaka 603 Miladia, kuliibuka tena vita vilivyodumu kwa muda wa miaka 24 baina ya nchi hizo mbili. Katika vita hivyo, jeshi la Iran lilipata ushindi mtawalia katika ardhi ya Roma kiasi cha kudhibiti karibu eneo zima la Roma ya Mashariki. Baadaye jeshi la mfalme Khosrow lilidhoofika na kumfanya mfalme huyo kukimbilia eneo la Ctesiphon, moja ya tawala za Sasania, huku akikataa pendekezo la usuluhishi. Aidha kutokana na Mfalme Khosrow Parvēz kuchana barua ya Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kulaaniwa na mtukufu huyo, utawala wa mfalame huyo ulidhoofika na hatimaye kushindwa na Waroma. Baadaye raia wa Iran kwa kushirikiana na jeshi la taifa walimuengua Khosrow kwenye utawala na kumtia jela kabla ya kuuawa kwake. 

Katika siku kama ya leo miaka 809 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa, mnajimu na tabibu mashuhuri wa Kiislamu Qutbuddin Mahmoud Shirazi katika mji wa Shiraz nchini Iran. Alianza kujifunza tiba akiwa bado mdogo na alianza kutibu wagonjwa katika moja ya hospitali za Shiraz baada ya kufariki dunia baba yake. Katika kipindi cha miaka kumi ya kazi ya utabibu, Qutbuddin Shirazi alitalii vitabi mbalimbali vya tabibu mwingine wa Kiislamu Bin Sina na vitabu vingine vya tiba na falfasa.Baada ya kuasisiwa kituo cha utafiti wa elimu ya nujumu katika eneo la Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran, Qutbuddin Shirazi aliishi kipindi kirefu na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi na kupata elimu ya nujumu.Katika kipindi chote cha umri wake, tabibu huyo wa Kiislamu alitembelea miji na nchi mbalimbali na kukutana na wasomi na maulamaa wa maeneo hayo. Ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha Jaamiul Usul.Alifariki dunia mwaka 710 Hijria.

Qutbuddin Mahmoud Shirazi

Siku kama ya leo miaka 771 iliyopita, vilianza vita vya Mansuriya katika silsila ya Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu. Vita hivyo vya kihistoria vilianzishwa katika eneo lililojulikana kwa jina hilo huko Misri na mfalme Saint Louis wa Ufaransa ambaye alikuwa na lengo la kuidhibiti Misri. Katika vita vya Mansuriya Jeshi la Msalaba lilipigwa vibaya na wapiganaji wa Kiislamu wa Misri waliokuwa wakiongozwa na Sallahuddin Ayyubi. Hatimaye Saint Louis alikamatwa mateka na Waislamu na kufungwa jela katika ikulu ya Loken ambayo hii leo inatumika kama jumba la makumbusho.

Miaka 241 iliyopita lifti au elevator kwa kimombo ilivumbuliwa. Mvumbuzi wa lifti hiyo ya kwanza alikuwa raia wa Marekani kwa jina la John Bikbart. Lifti hiyo ilifanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza huko katika mji wa Chicago nchini Marekani. Katika majaribio hayo, watu kadhaa waliingia ndani ya lifti hiyo na kwenda juu na chini katika masafa marefu. Lifti ya kwanza ya umeme ilitengenezwa mwaka 1889 na ile ya otomatiki mwaka 1915. 

Mfano wa lifti ya amani

Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Septemba 1885, alizaliwa Aquilino Ribeiro mwandishi na mwanamapinduzi wa Ureno. Baada ya kumaliza masomo yake, Ribeiro alitumbukia kwenye uwanja wa kisiasa na kufungwa jela kwa miaka kadhaa. Mnamo mwaka 1961, Aquilino Ribeiro alifanikiwa kupokea tuzo ya Nobel katika taaluma ya fasihi, na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1963 akafariki dunia.

Aquilino Ribeiro

Miaka 101 iliyopita katika siku kama hii ya leo inayosadifiana na tarehe 21 Shahrivar 1299 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Sheikh Muhammad Khiyabani, mwanamapambano katika kipindi cha kupigania katiba, na kukandamizwa harakati ya msomi huyo na wafuasi wake katika mji wa Tabriz, ulioko kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kujipatia elimu kwa maulamaa wakubwa, Sheikh Khiyabani alianza harakati za kupinga dhulma na ukandamizaji zilizokuwa zikifanywa na tawala za silsila ya Qajar hapa nchini. Baada ya kuusambaratisha udikteta wa Muhammad Ali Shah Qajar na kumlazimisha mtawala huyo kukimbia mwaka 1287 Hijria Shamsia, wananchi wa Tabriz walimchagua Sheikh Muhammad Khiyabani kuwa mwakilishi wao katika Bunge la Taifa la Iran. Hata hivyo katika siku kama ya leo Sheikh Khiyabani alikamatwa na kuuawa shahidi, wakati alipokuwa akipambana na vikosi vya serikali ya kifalme.

Shahidi Sheikh Muhammad Khiyabani

Na Siku kama hii ya leo miaka 28 iliyopita, mwafaka na tarehe 13 Septemba 1993 Yasir Arafat, kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na Yitzhak Rabin waziri mkuu wa wakati huo wa utawala haramu wa Israel walisaini mkataba wa mapatano kwa jina la "Makubaliano ya Ghaza-Jericho" huko Washington, Marekani. Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na utawala wa Kizayuni zilitambuana rasmi katika makubaliano hayo yaliyosainiwa miaka miwili baada ya kuanza mazungumzo eti ya amani kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni.

 

Tags