Oct 05, 2021 02:18 UTC
  • Jumanne tarehe 5 Oktoba 2021

Leo ni Jumanne tarehe 28 Safar 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 5 Oktoba 2021.

Siku kama ya leo miaka 1432 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka 11 Hijria, alifariki dunia Mtume Mtukufu Muhammad (saw) akiwa na umri wa miaka 63. Kutokana na kuwa na tabia ya ukweli na uaminifu tangu alipokuwa na umri mdogo, Mtume Mtukufu (saw) alipata umashuhuri kwa jina la "Muhammad Mwaminifu". Akiwa na umri wa miaka 40 Mwenyezi Mungu SW alimteua kuwa Mtume Wake ili aweze kuwalingania watu ibada ya Mungu Mmoja na kuondoa ukabila, dhulma na ujinga. Watu wa dini, madhehebu na mirengo tofauti na hata wale wasiokuwa na dini kabisa wamesema mengi kuhusu shakhsia adhimu ya Nabii Muhammad (saw). Mwandishi wa Ulaya, Stanley Lane Poole ameandika kwamba, Mtume Muhammad alipendwa na watu wote na kila aliyemuona, na kwamba hajawahi kuona wala hatamuona tena mtu mithili yake.

Siku kama ya leo miaka 1393 iliyopita, yaani sawa na tarehe 28 Safar mwaka 50 Hijiria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia mjini Madina. Mtukufu huyo aliishi miaka saba ya mwanzo wa umri wake pamoja na babu yake Mtume Muhammad (saw) ambapo aliweza kunufaika na mafunzo na maarifa ya dini Tukufu ya Kiislamu. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as). Baada ya kufariki dunia Imam Ali (as) Waislamu walimpa baia Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza, ambapo hata hivyo baada tu ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo alikabiliwa na njama za Muawiyah bin Abi Sufiyan. Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi aliloachiwa na baba yake kwa ajili ya kumkabili Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah. Imam Hassan aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufyan.

Katika siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, alizaliwa Louis Jean Lumiere, mwanakemia mashuhuri wa Kifaransa. Mwaka 1895 akiwa pamoja na ndugu yake aliyejulikana kwa jina la Auguste Lumiere, walifanikiwa kutengeneza kifaa ambacho kiliwasaidia kuchukua picha mbalimbali na kusajili harakati. Mwaka huo huo Lumiere alifanikiwa kuonyesha filamu yake ya kwanza au Motion Picture katika majumba ya sinema.

Louis Jean Lumiere

Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo  Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliondoka Iraq na kuhamia Paris, Ufaransa. Imam Khomeini aliamua kufanya hijra hiyo ya kihistoria wakati utawala wa zamani wa Iraq ulipoanza kumzuia kufanya harakati za mapambano dhidi ya utawala wa Shah. Serikali ya wakati huo ya Iraq ambayo ilikuwa ikilinda uhusiano wake na utawala wa Shah nchini Iran, ilimtaka Imam Khomeini ajiepushe na harakati zozote za kisiasa na za kimapinduzi dhidi ya utawala huo wa Shah. Hata hivyo Imam aliiambia serikali hiyo kuwa hilo lilikuwa jukumu lake la kisheria ambalo aliwajibika kulitekeleza na kusisitiza juu ya kuendelezwa mapambano kwa kutoa hotuba na kutuma kanda za kimapinduzi nchini Iran. 

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, Slobodan Milosevic dikteta wa zamani wa Yugoslavia na mhusika mkuu wa vita vya umwagaji damu huko Balkan, alijiuzulu baada ya miezi kadhaa ya malalamiko ya ndani na vikwazo vya kimataifa. Milosevic alikuwa rais wa Serbia tangu mwaka 1990 hadi 1997 na baadaye akawa Rais wa Jamhuri ya Yugoslavia. Katika vita vya Bosnia, na kwa uungaji mkono wa kila upande wa Waserbia, Slobodan Milosevic alishiriki pakubwa katika kutekeleza mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa Bosnia Herzegovina. Milosevic alikuwa kiongozi wa kwanza mtenda jinai za kivita kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa kwa ajili ya kuhukumiwa. Hata hivyo mhalifu huyo katili alifariki dunia akiwa katika korokoro za mahakama hiyo huko The Hague nchini Uholanzi kutokana na mwendo wa kinyonga wa kushughulikia kesi yake.

Slobodan Milosevic

Na tarehe 5 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu. Siku hii ilitangazwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika tarehe 3 hadi 8 mwezi Septemba mwaka 1994 kwa ajili ya kuenzi mchango wa walimu na nafasi yao kubwa katika jamii ya mwanadamu.

 

Tags