Oct 25, 2021 02:30 UTC
  • Jumatatu tarehe 25 Oktoba 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 18 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1443 Hjria sawa na Oktoba 25 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1442 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, ilianza kazi ya ujenzi wa Msikiti wa Mtume mjini Madina ambao ni msikiti wa pili kwa utukufu duniani baada ya Masjidul Haram. Mtume (SAW) alitoa amri ya kujengwa msikiti wa Madina baada tu ya kuhamia mjini humo na yeye mwenyewe alishiriki katika ujenzi wake. Kandokando ya msikiti huo kulijengwa vyumba vya Mtume na baadhi ya maswahaba zake. Mtume hakuutumia msikiti kwa ajili ya ibada tu, bali alitumia pia sehemu hiyo kwa ajili ya masuala kama kutoa hukumu baina ya watu, vikao vya mashauriano, mafunzo ya kivita na utatuzi wa masuala mbalimbali ya Waislamu.

Msikiti wa Mtume mjini Madina

Siku kama ya leo miaka 310 iliyopita, mwanakijiji mmoja aligundua alama za awali za mabaki ya miji miwili ya kihistoria ya Pompeii na Herculaneum nchini Italia. Mji wa Pompeii ulijengwa na kaumu ya Oscan mwanzoni mwa karne ya 6 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih (as) na ulikuwa na bandari maarufu na yenye ustawi mkubwa hadi karne ya kwanza baada ya kuzaliwa Nabii Issa (as). Mji huo na ule wa Herculaneum ilizikwa na kufunikwa kikamilifu na volcano ya Mlima Vesuvius mwaka 79 Miladia.

Siku kama ya leo, miaka 210 iliyopita, alizaliwa Évariste Galois, mtaalamu wa hesabati wa nchini Ufaransa, karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Paris. Kufikia umri wa miaka 12, Galois hakufunzwa na mtu yeyote isipokuwa mama yake na alianza kusoma vitabu vya jiometri na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo. Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa.  Galois aliuawa  akiwa na umri wa miaka 21 hapo tarehe 29 mwezi Mei mwaka 1832 baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa. Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani.

Évariste Galois

Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita, alizaliwa Pablo Picasso mchoraji mashuhuri wa Kihispania. Picasso alikuwa mwasisi wa harakati ya Cubist ambayo ilienea kwa kasi kubwa miongoni mwa wachoraji wa Ufaransa. Pablo Picasso alichora picha nyingi na daima alikuwa akifanya juhudi za kuendeleza harakati hiyo. Mchoro wa 'The Girls of Avignon' wa mchoraji huyo ndio uliokuwa mwanzo wa mtindo wa Cubism na kazi kubwa zaidi ya Picasso katika mtindo huo ni 'Guernica'. Katika mchoro huo Pablo Picasso anaonesha hofu iliyompata kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na ndege za kivita za Ujerumani na Italia dhidi ya mji wa Guernica. Picasso alifariki dunia Aprili mwaka 1973.

Pablo Picasso

Na katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita aliaga dunia Abul Qassim Halat mshairi, mchekeshaji na mtarjumi wa zama hizi wa Kiirani. Alianza kutunga mashairi akiwa na umri wa miaka 16 na akaondokea kubobea katika mashairi ya vichekesho. Malengo huyo alikuwa akizifahamu vyema lugha za Kifarsi, Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu. Miongoni mwa athari zake muhimu ni tarjama ya maneno yenye thamani kubwa ya Bwana Mtume (saw) na Imam Ali bin Abi Talib (as). Abul Qassim Halat ameacha athari nyingi zenye thamani kubwa katika uga wa maishairi.

Abul Qassim Halat

 

Tags