Nov 01, 2021 10:37 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Nov 1

Hujambo mpenzi msikilizaji natumai u bukheri wa afya. Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio yaliyogonga vichwa vya habari katika ulimwengu wa michezo ndani ya siku saba zilizopita, ndani na nje ya nchi.

Soka: Iran U23 yatinga Kombe la Asia

Timu ya taifa ya soka ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 23 ya Iran imetinga michuano ya Kombe la Asia mwaka ujao 2022, baada ya kuzizaba Tajikistan, Lebanon na Nepal. Siku ya Jumapili, timu hiyo ilishuka dimbani kuvaana na mwenyeji wake Tajikistan, na kuvuna ushindi muhimu wa mabao 3-2. Katika mchuano huo uliopigwa katika Uwanja wa Central Republican jijini Dushambe, mchezaji Yasin Salmani alifanikiwa kufunga mabao matatu ya hatrick katika kipindi cha kwanza. Wenyeji walijizoazoa na kupata mabao mawili yaliyofungwa na Islom Zairov na Ehson Panshanbe. 

Wanakandanda wa Iran wakishangilia bao

 

Katika mchuano wa Alkhamisi, Iran ambayo ipokatika Kundi B iliichabanga Lebanon mabao 2-0. Mehdi Limouchi alipachika wavuni bao la kwanza dakika tano buda baada ya kupulizwa kipyenga cha kuanza ngoma, huku Mial Kor akiongeza la pili katika dakika za majeruhi. Kabla ya hapo, vijana hao wa Kiirani waliibamiza Nepal mabao 4-0 katika mchuano wa ufunguzi. Wanasoka hao wanaonolewa na mkufunzi Mehdi Mahdavikia wamejikatia tiketi za kushiriki fainali za michuano hiyo, na sasa watajiunga na timu nyingine 15 akiwemo mwenyeji Uzbekistan katika kivumbi cha Kombe la Asia 2022, kitakachoandaliwa na Shirikisho la Soka Asia (AFC).

Judo; Iran yazoa yaibuka ya 2 Ufaransa

Timu ya taifa ya judo kwa wachezaji wenye matatizo ya kusikia ya Iran imebuka ya pili katika mashindano ya Kombe la Dunia ya mchezo huo yaliyofanyika huko Ufaransa. Timu hiyo ya Iran imezawadiwa medali ya fedha kwa kufanya vyema kwenye mashindano hayo ya kimataifa yaliyoanza Alkhamisi katika mji wa Versailles, maili 12 magharibi mwa Paris, mji mkuu wa Ufaransa. Bahram Qasemi, Balozi wa Iran mjini Paris ameipongeza timu hiyo ya judo ya visiwi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kufanya vyema katika mashindano hayo ya dunia.

Katika ujumbe alitouma kwenye mtandano wa kijamii wa Twitter amesema: Ushindi wa thamani wa timu ya taifa ya judo ya viziwi ya Iran umeipa fakhari taifa la Iran kwa mara nyingine tena. Iran imeibuka ya pili ikitanguliwa na Korea Kusini, huku Uturuki ikimaliza katika nafasi ya tatu ya mashindano hayo ya mchezo wa judo ya visiwa mtindo wa kata.

Timu ya Raga ya Kenya yatwaa ubingwa 'Safari Sevens'

Timu ya taifa ya raga ya Kenya ya wachezaji saba kila upande ya Shujaa imetwaa ubingwa wa Safari Seven baada ya kuisasambua Ujerumani katika fainali ya aina yake iliyopigwa Jumapili katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi. Katika fainali hiyo ya duru ya 23 ya mashindano ya ubingwa ya Safari Sevens, Shujaa ya Kenya ilijituma na kucheza kwa kasi ya juu labda kutokana na motisha ya kuchezea nyumbani mbele ya mashabiki zake. Timu hiyo ilipata ushindi wa alama 12-5. Ulikuwa mwanzo mgumu kwa timu zote mbili, lakini hilo halikumfanya Levy Amunga ashindwe kufunga mikimbio 7 iliyowatoa kijasho vijana wa kijerumani wanaopikwa na Damian McGrathBaada ya mapumziko, timu ya Kenya inayotiwa makali na mkufunzi Innocent Simiyu ilipekwa mbio na Wajerumani ambao waliweza kufunga mizunguko kadhaa kwa mpigo. Kufuatia ushindi huo, taji hilo linasalia nchini Kenya kwani lilitwaliwa na Morans wa Kenya mwaka 2019.

Timu ya Kenya ya raga ya Kenya ilipotwaa ubingwa miaka 6 nyuma

 

Mwaka jana, mashindano hayo hayakuandaliwa kutokana na msambao wa virusi vya ugonjwa wa Covid-19. Wakati timu ya taifa ya raga ya Kenya kwa upande wa wanaume ilikuwa inatwaa taji hilo, ndugu zao wa kike pia walikuwa wanafanya kweli, kwani wametwaa ubingwa kwa upande wao baada ya kushinda mechi zao zote, ikiwemo ya fainali. Fainali hiyo ya raga ya wanawake ilipigwa Jumapili nchini Uganda, ambapo Lionesses 1 (Masimba jike) wa Kenya waliambulia ushindi mnono wa 26-0. Kenya Lionesses I ilinyakua taji la kinadada baada ya kupiga wapinzani wote – Titans kutoka Afrika, Kenya Lionesses II, Zimbabwe na Uganda. Lionesses I ilikamilisha kampeni yake kwa kulipua Uganda Lady Cranes 26-0 kupitia kwa miguso ya Janet Okello (miwili), Christabel Lindo na nahodha Philadelphia Olando na mikwaju ya Grace Adhiambo. Kenya Lionesses II iliridhika na nafasi ya pili nayo Uganda inakamata nambari tatu na kupokezwa tuzo hiyo na mshikilizi wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100, Ferdinand Omurwa Omanyala.

Simba baada ya kuondolewa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika

Baada ya klabu ya Simba ya Tanzania kubanduliwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu baada ya kukubali kuzabwa mabao 3-1 na Jwaneng Galaxy ya Botswana, timu hiyo imeamua kufanya maamuzi magumu. Simba SC imetangaza rasmi kuachana na Kocha wake Mkuu Mfaransa Didier Gomes Da Rosa (52) pamoja na mtaalamu wa viungo Adel Zrane (Tunisia) na Kocha wa makipa Milton Nienov (Brazil). Mwanzo mbaya wa msimu, ikiwamo kutolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ni mambo yaliyochangia kuondoka kwa Gomes na mabosi wa klabu hiyo ya Msimbazi tayari wameingia mzigoni kuhakikisha wanampata kocha wa kurejesha tabasamu kwa mashabiki wao.

Wachezaji wa Simba uwanjani

 

Simba SC imetangaza uamuzi huo ikiwa ni siku mbili zimepita toka waondolewe katika michuano ya club Bingwa Afrika kwa kufungwa 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Gomes alijiunga na Simba SC 2021 akitokea Al Merreikh ya Sudan. Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa taarifa kuwa ameachana na club ya Simba SC, kocha Didier Gomes aliongea na waandishi wa habari akizungumzia jambo hilo. Aidha kikao chache na waandishi kimejiri siku chache baada ya baada ya Simba kufungwa 3-1 na Jwaneng Galaxy ya Botswa na kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika. Anasisitiza kuwa Simba ni timu imara ambayo ina nafasi ya kufanya vyema katika siku za usoni. Aidha amewashukuru mashabiki wa klabu hiyo kwa kusimama naye kipindi chote alipokuwa nchini Tanzania. Simba mpaka sasa ina orodha ya zaidi ya Makocha 100 waliotuma maombi ya kurithi mikoba ya Gomes.

Ligi ya EPL

Wilfred Zaha aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufungia Crystal Palace mabao 50 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kuongoza waajiri wake kuduwaza mabingwa watetezi Manchester City kwa kichapo cha 2-0 mnamo Jumamosi ugani Etihad. Zaha alifungulia Palace ukurasa wa mabao katika dakika ya sita baada ya kushirikiana vilivyo na Conor Gallagher aliyezamisha kabisa chombo cha Man-City ya kocha Pep Guardiola katika dakika ya 88. Ushindi wa Palace uliwashuhudia wakikomesha rekodi duni ya kusajili sare katika mechi nne mfululizo ligini. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Man-City kufungwa katika uwanja wao wa nyumbani msimu huu na mara ya nne katika kampeni zote za EPL. Huku hayo yakiarifiwa, REECE James alifunga mabao mawili na kusaidia Chelsea kufungua pengo la alama tatu kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kucharaza Newcastle United 3-0 uwanjani St James’s Park mnamo Jumamosi. James alijaza kimiani krosi aliyopokezwa na Callum Hudson-Odoi katika dakika ya 65 na kuweka Chelsea kifua mbele kabla ya beki huyo kumzidi maarifa kipa Karl Darlow kwa mara nyingine katika dakika ya 77 baada ya kushirikiana na Ruben Loftus-Cheek. Darlow alimkabili visivyo fowadi Kai Havertz mwishoni mwa kipindi cha pili na kusababisha penalti ambayo Chelsea walifungiwa na Jorginho. Matokeo hayo yaliendeleza masaibu ya Newcastle ambao hawajashinda mechi yoyote kufikia sasa ligini msimu huu. Chini ya kocha Thomas Tuchel, Chelsea walifungua mwanya huo wa pointi tatu baada ya wapinzani wao wakuu kwenye EPL msimu huu kujikwaa katika michuano yao. Liverpool ya kocha Jurgen Klopp iliambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Brighton ugani Anfield. Wakati huohuo, Kiungo Pierre-Emile Hojbjerg wa Tottenham Hotspur amesema matokeo ya timu yao katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowapa Manchester United jukwaa la kuwatandika 3-0 mbele ya mashabiki wa nyumbani wikendi “hayakubaliki kabisa”. Mabao matatu ambayo Man-United walifunga kupitia Cristiano Ronaldo, Edinson Cavani na Marcus Rashford yalikuwa kitulizo kikubwa kwa kocha Ole Gunnar Solskjaer aliyekuwa akikabiliwa na presha ya kupigwa kalamu ugani Old Trafford kwa sababu ya matokeo duni. Man-United walijitosa ulingoni wakiwa na kiu ya kujitoa topeni baada ya kupigwa na Leicester City (4-2) na Liverpool (5-0) ligini. Ushindi dhidi ya Spurs ulikuwa wao wa kwanza baada ya mechi tano za EPL na kwa sasa wanajivunia alama 17 sawa na Arsenal. Japo ufanisi huo ni afueni kwa ‘mashetani wekundu’ wa Man-United, mabingwa hao mara 20 wa EPL wangali na ratiba ngumu katika kipindi cha mwezi mmoja ujao. Na ARSENAL waliendeleza ufufuo wa makali yao msimu huu kwa kuzamisha Leicester City 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani King Power. Masogora wa kocha Mikel Arteta walichuma nafuu tele kutokana na utepetevu wa wenyeji wao katika kipindi cha kwanza na wakafunga mabao mawili ya haraka kupitia Gabriel Magalhaes na Emile Smith Rowe chini ya dakika 20 za mwanzo wa kipindi cha kwanza. Wabeba bunduki hao kwa sasa hawajashindwa katika mechi saba zilizopita za EPL na wanajivunia alama 17.

…………………TAMATI…………….

 

 

 

 

 

Tags