Nov 30, 2021 04:38 UTC
  • Jumanne tarehe 30 Novemba 2021

Leo ni Jumanne tarehe 24 Rabiuthani 1443 Hijria sawa na Novemba 30 mwaka 2021.

Miaka 354 iliyopita katika siku kama ya leo, Jonathan Swift mwandishi mashuhuri wa Ireland alizaliwa huko Dublin mji mkuu wa nchi hiyo. Swift alishiriki pakubwa katika harakati za ukombozi wa Ireland. Baadaye, Jonathan Swift alianza kujishughulisha na kazi ya uandishi. Swift alifariki dunia akiwa na miaka 78. 

Jonathan Swift

Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, alizaliwa Theodor Mommsen mwanahistoria na mtafiti wa Ujerumani. Baada ya kumaliza masomo, Mommsen alijishughulisha na utafiti kuhusiana na vitabu tofauti na athari za tamaduni za zamani. Miongoni mwa vitabu vyake maarufu zaidi ni kitababu kinachoitwa 'Historia ya Roma ya Kale' ambacho ndiyo kitabu kamili cha historia ya mji wa Roma. Mwanahistoria huyo wa Ujerumani alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi hapo mwaka 1902 na alifariki dunia mwaka mmoja baadaye, akiwa na umri wa miaka 86.

Theodor Mommsen

Miaka 186 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Mark Twain mwandishi mashuhuri wa Kimarekani. Twain alikipitisha kipindi cha utoto na ubarobaro wake na matukio yasiyo ya kawaida ambayo baadaye yalikuja kuwa maudhui kuu ya vitabu vyake. Mark Twain alikuwa mwandishi mwenye utani na mzaha. Aliandika visa na simulizi nyingi kwa ajili ya watoto na vijana wadogo ambapo tunaweza kuashiria hapa vitabu vyake viwili vya The Andventures of Tom Sawyer na (Matukio Yasiyo ya Kawaida ya Tom Sawyer) The Prince and The Pauper (Mrithi wa Kiti cha Ufalme na Ombaomba). Mwishoni mwa umri wake Mark Twain alikumbwa na ukata na umasikini mkubwa na hatimaye akaaga dunia mwaka 1910 baada ya kuugua.  

Mark Twain

Miaka 121 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Oscar Wilde, mwandishi na malenga mahiri wa Ireland. Wilde alizaliwa mwaka 1854 katika familia iliyokuwa na mapenzi maalumu na masuala ya kiutamaduni na Sanaa. Baada ya kukamilisha masomo yake ya sekondari alijiunga na Chuo Kikuu. Oscar Wilde alianza kujihusisha na taaluma ya uandishi akiwa katika rika la ujana na katika kipindi kifupi cha umri wake alifanikiwa kuandika vitabu mbalimbali vilivyokuwa na madhumuni ya riwaya, mashairi na maigizo. Baadhi ya vitabu vya Oscar Wilde ni The Model Millionaire, The Soul of Man Under Socialism na The Canterville Ghost. 

Oscar Wilde

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, aliaga dunia Ustadh Abdul-Basit Abdul-Samad katika mji wa Cairo nchini Misri. Abdul Basit alikuwa mmoja wa waalimu na maqarii wakubwa wa Qur'ani Tukufu. Alianza kujifunza Qurani Tukufu akiwa mdogo na alipofikia umri wa miaka 12 akafanikiwa kupata tuzo ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani. Katika maisha yake Ustadh Abdul-Basit alijishughulisha na usomaji wa Qurani Tukufu na kutunukiwa zawadi na tunzo muhimu katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani tukufu kwenye nchi mbalimbali za Kiislamu, sambamba na kuwavutia Waislamu wengi kwenye kusoma maneno hayo ya Mwenyezi Mungu. Abdul Basit ameacha kanda nyingi za sauti yake nzuri ya qiraa ya Qur'ani Tukufu.

 

Tags