Dec 01, 2021 02:39 UTC
  • Jumatano, tarehe Mosi Disemba, 2021

Leo ni Tarehe 25 Rabiuthani 1443 Hijria sawa na Disemba Mosi mwaka 2021.

Mwaka 288 Hijiria katika siku kama ya leo miaka 1155 iliyopita, alifariki dunia Thabit bin Qurrah Swabi, mtaalamu wa hesabati, nyota na tabibu katika kipindi cha utawala wa Bani Abbas. Alizaliwa mwaka 221 Hijiria, mjini Harran Mesopotamia nchini Iraq. Thabit bin Qurrah Swabi alikuwa akizungumza lugha za Kigiriki, Kiasyria na Kiarabu. Alisafiri kwenda mjini Baghdad Iraq kwa lengo la kusoma na kwa usimamizi wa Muhammad bin Musa aliyekuwa mtaalamu mkubwa Mwislamu wa hesabati na nyota kipindi hicho, Thabit bin Qurrah Swabi akaingia katika uwanja wa elimu hizo. Aliwasilisha nadharia mpya katika uwanja wa hesabati. Aidha katika utaalamu wa nyota yeye ni katika watu wa kwanza kurekebisha chombo cha Ptolemaic. Thabit bin Qurrah Swabi aliandika vitabu vingi katika uwanja wa tiba, hesabati na nyota, vilivyofasiriwa kutoka lugha ya Kigiriki kwenda Kiarabu, miongoni mwa vitabu hivyo ni pamoja na kitabu kiitwacho "Adh Dhakhiratu Fii Ilmi al Twib" na "Kitabul Mafrudhat."

Thabit bin Qurrah Swabi

Miaka 1075 iliyopita mwaka 368 Hijiria, alizaliwa mjini (Corduba, Qurtuba) Uhispania, faqih mtaalamu wa hadith, fasihi na mwanahistoria Abu Omar Yusuf bin Abdallah mashuhuri kwa jina la Abdul Birr. Alipata masomo ya msingi kutoka kwa baba yake na walimu wengine wakubwa wa kipindi hicho. Ibnu Abdul Birr aliupa umuhimu mkubwa utafiti, ambapo kwa kipindi cha muda mfupi alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa mjini Andalusia. Kufuatia kukosekana amani na usalama katika mji wa (Corduba, Qurtuba), Ibn Abdul Birr alilazimika kuhamia mji mwingine wa Daynah ambao kipindi hicho ulikuwa moja ya vituo muhimu vya elimu vya Andalusia, ambapo huko alifanikiwa kuandaa athari zake. Miongoni mwa athari za msomi huyu mashuhuri ni kitabu kiitwacho "Istiiab" ambacho kinahusu maisha ya masahaba wa Mtukufu Mtume Muhammad (saw).

Katika siku kama ya leo miaka 196 iliyopita, muungano wa kihistoria wa nchi za Ulaya uliojulikana kama Muungano Mtakatifu ulisambaratika baada ya kujiengua utawala wa Kikaitsar (Tsarist) wa Russia katika muungano huo. Baada ya kuanguka kwa utawala wa Napoleon, muungano huo ukaunda Congress ya Vienna, kati ya tawala za Russia, Austria na ufalme wa Pros na serikali hizo zikaafikiana kwamba nchi zilizo chini ya utawala wa muungano huo na katika uhusiano wa kimataifa zifuate misingi ya dini ya Kikristo.

Siku kama hii ya leo miaka 83 iliyopita Ayatullah Sayyid Hassan Mudarres, mwanazuoni mwanamapambano na mpigania ukombozi wa Kiirani aliuawa shahidi na vibaraka wa Reza Khan, mtawala dhalimu wa Iran wa wakati huo katika mji wa Kashmar kaskazini mashariki mwa Iran. Ayatullah Sayyid Hassan Mudarres aliamua kuanzisha mapambano dhidi ya utawala huo baada ya kujionea dhulma na ukandamizaji wa mtawala Reza Khan nchini Iran. Alifanya jitihada kubwa za kutekelezwa sheria za Kiislamu hapa nchini na kuiokoa Iran kutoka kwenye makucha na udhibiti wa wakoloni. Kwa msingi huo mtawala kibaraka wa wakati huo wa Iran, Reza Khan Pahlavi alimuona kuwa adui mkubwa na kuchukua uamuzi wa kumuua.

Ayatullah Sayyid Hassan Mudarres

Siku kama ya leo miaka 48  iliyopita David Ben-Gurion mmoja wa waasisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Waziri Mkuu wa kwanza wa utawala huo ghasibu aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87. Ben-Gurion alizaliwa tarehe 16 Oktoba 1886 katika mji wa Plonsk huko Uholanzi ambayo katika zama hizo ilikuwa sehemu ya ardhi ya ufalme wa Russia. Alielekea katika ardhi za Palestina mwaka 1906 akiwa na umri wa miaka 20 na kuasisisi harakati ya Kiyahudi. Katika Vita vya Kwanza vya Dunia David Ben-Gurion alikuwa na nafasi kubwa katika kuwahamisha taratibu Mayahudi kwenda ardhi za Palestina. Katika kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia harakati hiyo ilishika kasi chini ya uungaji mkono wa madola makubwa hususan Uingereza, kiasi kwamba mwaka 1948 Miladia sawa na tarehe 5 Mei na baada ya kupitishwa azimio na Umoja wa Mataifa la kuigawa Palestina katika pande mbili za Kiyahudi na Palestina, kulitangazwa rasmi kuanzishwa utawala haramu wa Kizayuni na wa kibaguzi wa Israel. Masaa machache baadaye, Marekani na Urusi ya zamani zikatangaza kuutambua utawala huo khabithi. 

David Ben-Gurion

Na tarehe Mosi Disemba kila mwaka, nchi mbalimbali duniani huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ukimwi. Ukimwi ni ugonjwa wa kuambukiza ambao unatokana na kurundikana kwa virusi vya HIV mwilini ambavyo huharibu mfumo wa ulinzi wa mwili na kutayarisha mazingira ya kushambuliwa na maradhi nyemelezi. Ugonjwa huu ulibainika kwa mara ya kwanza kabisa nchini Marekani mwazoni mwa miaka ya 1980. Wakati huo baadhi ya wanaume wanaofanya mapenzi kinyume na maumbile huko New York na California waligundulika kuwa na kansa ambazo hazikukubali tiba ya aina yo yote. Japokuwa wakati huo, haikujulikana sababu ya maambukizi ya ghafla ya magonjwa hayo lakini tukio hilo limetambuliwa kuwa ndiyo mwanzo wa kujitokeza maradhi ya Ukimwi. Ugonjwa huo ambao haukuwa na jina ulienea kwa kasi kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja na hatimaye mwaka 1982 ulipewa jina la Ukimwi.