Dec 03, 2021 03:09 UTC
  • Ijumaa tarehe 3 Disemba 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 27 Rabiuthani 1443 Hijria sana na tarehe 3 Disemba 2021.

Miaka 137 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Dakta Rajendra Prasad, mwanasiasa na mwanafilosofia wa India huko katika mojawapo ya vijiji vya jimbo la Bihar. Rajendra Prasad aliweza kuendelea na masomo na kufikia daraja ya udaktari, licha ya hali duni ya kifedha ya familia yake. Aidha alishiriki na wananchi wa India katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yao. Prasad vilevile alishirikiana bega kwa bega na Mahatma Gandhi katika mapambano ya kisiasa dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na kwa mara kadhaa aliteuliwa kuongoza chama cha Congress ya Kitaifa ya India. Rajendra Prasad aliteuliwa kuwa Rais wa kwanza wa India baada ya uhuru wa nchi hiyo na kuasisiwa mfumo wa jamhuri nchini humo mwaka 1950.

Dakta Rajendra Prasad

Miaka 42 iliyopita katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipasishwa kwa wingi wa kura za wananchi. Katiba hiyo inasisitiza juu ya kuzingatiwa thamani za Kiislamu, uadilifu wa kijamii na kuheshimiwa haki za binadamu. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, katika mwaka 1368 Hijria Shamsiya, kipengee cha ziada kiliongezwa kwenye katiba hiyo, baada ya kupasishwa na Baraza la Wataalamu linalomteuwa Kiongozi Mkuu wa Iran na kuidhinishwa pia na wananchi. Kwa mujibu wa kipengee hicho cha nyongeza, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ina vipengee 14 na vifungu 177. 

 

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na umri wa miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Alishirikiana bega kwa bega na wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala muovu wa Shah. Msomi huyo amelea ma lufunza wasomi wakubwa kama Ayatullah Murtadha Mutahhari, Imam Musa Sadr na Sayyid Ridha Sadr. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Ameandika vitabu vingi katika taaluma za sheria na teolojia ya Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari

Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 3 mwezi Disemba mwaka 1984, kulitokea janga kubwa la kuvuja gesi ya kemikali katika kiwanda kimoja cha Marekani katika mji wa Bhopal huko katikati mwa India. Kiwanda hicho kilikuwa kikimilikiwa na kampuni ya Kimarekani iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Union Carbide. Uzembe wa maafisa wa kiwanda hicho na kutozingatiwa viwango vya usalama kulipelekea kuvuja kwa gesi ya sumu ya sianidi (cyanide) kutoka katika kiwanda hicho na kuenea katika hewa. Wakazi wasio na hatia wa mji wa Bhopal wasiopungua 2500 walipoteza maisha yao na mamia ya wengine pia kujeruhiwa katika janga hilo.

Janga la Union Carbide

Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo, kombora la kwanza la balestiki lililotengenezwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilifanyiwa majaribio kwa mafanikio wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi hicho ambapo Iran ilikuwa chini ya vikwazo vikali vya nchi za Magharibi huku ikipigana na adui kulinda ardhi yake, awamu ya kwanza ya majaribio ya kombora hilo ilifanyika kwa mafanikio na uzalishaji wake ukaanza wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. 

 

Tags