Dec 04, 2021 02:40 UTC
  • Jumamosi, 4 Disemba 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 28 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1443 Hijria mwafaka na tarehe 4 Disemba 2021 Miladia.

Miaka 805 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia huko Damascus. Alizaliwa mwaka 560 Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka, Halab (Aleppo) na Baghdad, na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Ibn Arabi alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al-Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam". ***

Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi

 

Katika siku kama ya leo miaka 531 iliyopita, alizaliwa Mirza Sharaf Jihan Qazvini, mshairi mahiri wa Kiirani. Alizaliwa katika mji wa Qazvin moja ya miji ya Iran. Alisoma kwa Amir Ghiyath Din mwanazuoni mashuhuri wa zama hizo. Mirza Sharaf Jihan mbali na kubobea katika elimu za akili na nakili na kuzifundisha alikuwa mwalimu pia katika taaluma za fasihi na mashairi. ***

Mirza Sharaf Jihan Qazvini,

 

Miaka 122 iliyopita, kwa mara ya kwanza chanjo ya homa ya matumbo au Typhoid ilitumiwa kwa mwanadamu ili kukabiliana na maradhi hayo ambayo husababisha kuhara damu. Awali chanjo hiyo ilivumbuliwa na mtafiti mmoja wa Kifaransa na baadaye ilikamilishwa na tabibu wa Kiingereza kwa jina la Almroth Edward Wright. ***

Chanjo ya homa ya matumbo au Typhoid

 

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, mkutano wa pande tatu yaani Marekani, Uingereza na Ufaransa ulifanyika katika kisiwa cha Bermuda kaskazini mwa Amerika Kusini. Mbali na nchi hizo tatu kujadili uhusiano baina yao, zilichukua maamuzi muhimu na kuratibu namna ya kukabiliana na siasa za Shirikisho la Umoja wa Sovieti huko Berlin. Katika zama hizo sehemu ya magharibi ya mji wa Berlin, Ujerumani ilikuwa chini ya udhibiti wa Marekani, Uingereza na Ufaransa na sehemu ya mashariki ilikuwa chini ya udhibiti wa Umoja wa Sovieti. Kupamba moto hitilafu za namna ya kuuendesha mji huo, ndiko kulikopelekea kujengwa ukuta maarufu wa Berlin mnamo mwaka 1961. ***

Ujenzi wa ukuta wa Berlin

 

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, mkutano wa kwanza wa Kiislamu kuhusiana na Palestina ulifanyika hapa mjini Tehran. Mkutano huo ulifanyika katika fremu ya mfungamano wa walimwengu na mapambano ya Intifadha ya Palestina na kukabiliana na wimbi la kuhajiri Mayahudi kuelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa kuchunguza chanzo cha mapambano ya Intifadha ya wananchi Waislamu wa Palestina, Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi hao pamoja na taathira ya matukio ya Mashariki ya Kati kwa taifa la Palestina. ***

 

Na miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 9 Azar kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Murtadha Movahed Abtahi msomi na alimu mkubwa. Abtahi alizaliwa mwaka 1284 Hijria katika mji wa Isfahan, Iran. Akiwa katika rika la ujana alihudhuria darsa na kusoma kwa maustadhi na walimu mahiri wa zama hizo kama Jalal al-Din Hamai, Mirza Ahmad Shahidi na Sayyid Muhammad.  Msomi huyu alikuwa na hima kubwa pia katika kuandika vitabu na utunzi wa mashairi na ameacha athari zenye thamani katika uga wa elimu. Ayatullah Sayyid Murtadha Movahed Abtahi aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 90. ***

Ayatullah Sayyid Murtadha Movahed Abtahi

 

Tags