Dec 11, 2021 02:43 UTC
  • Jumamosi, 11 Disemba, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 6 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1443 Hijria sawa na tarehe 11 Disemba 2021.

Siku kama ya leo miaka 1029 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Abu Said Muhammad bin Abdul-Jalil Sistani mwanahisabati mahiri na mashuhuri wa Kiislamu. Alibobea katika nyuga za hisabati, jiometri na nujumu na alihesabiwa kuwa mwalimu hodari wa taaluma hizo. Abu Said Sistani alikuwa akialifu kitabu katika kila taaluma aliyokuwa akiikosomea. Kitabu cha Jamiu Shahi katika hisabati ni miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu wa Kiislamu. ***

Abu Said Muhammad bin Abdul-Jalil Sistani

 

Katika siku kama ya leo miaka 211 iliyopita Alfred Louis Charles de Musset-Pathay malenga na mwandishi mwashuhuri wa Ufaransa alizaliwa katika familia ya wasomi mjini Paris, Ufaransa. Musset aliandika diwani yake ya kwanza ya mashairi kwa jina la Simulizi za Uhispania na Italia akiwa na umri wa miaka 19 na hivyo kupata umashuhuri mkubwa kutokana na mbinu yake mpya ya uandishi. Akiwa na umri wa miaka 22 aliandika  tamthilia yake ya kwanza iliyoibua utata kutokana na masuala ya kiroho na kimaadili. Fikra zake huru zilimfanya awe miongoni mwa waandishi watajika katika nusu ya kwanza ya karne ya 19. Alfred de Musset aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 47  hapo mwaka 1857. ***

Alfred Louis Charles de Musset-Pathay

 

Miaka 178 iliyopita katika tareke kama ya leo yaani tarehe 11 Disemba mwaka 1843 Miladia alizaliwa daktari na mtaalamu wa vividudu maradhi wa Kijerumani aliyevumbua ugonjwa wa kifua kikuu,  Robert Koch. Baada ya kukamilisha masomo katika taaluma ya tiba, Robert Koch alijishughulisha na kutibu wagonjwa katika miji mbalimbali ya Ujerumani sambamba na kufanya uhakiki kuhusu maradhi tofauti. Tarehe 24 Machi mwaka 1882 alifanikiwa kuvumbua ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Katika safari zake nyingi barani Afrika, tabibu huyo wa Kijerumani pia alibaini kuwa ugonjwa wa malale uliokuwa ukisababisha vifo vya Waafrika wengi ulikuwa ukisababishwa na mdudu anayeitwa mbung'o. ***

Robert Koch.

 

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) uliasisiwa baada ya kupasishwa suala hilo kwa wingi wa kura na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Kwa utaratibu huo, taasisi hiyo ikaanza rasmi shughuli zake chini ya Baraza la Masuala ya Kijamii la Umoja wa Mataifa. Awali Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), ulikuwa na jukumu la kuwahudumia watoto waliojeruhiwa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Hata hivyo baadaye asasi hiyo muhimu ikapanua zaidi shughuli zake na kuanza kuandaa mahitaji ya kimsingi maishani kama chakula, elimu na malezi kwa watoto waliokosa haki hizo za kimsingi. Makao makuu ya UNICEF yapo mjini New York, Marekani. ***

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF)

 

Na tarehe 11 Disemba mwaka 1958 Burkina Faso ilitangazwa kuwa Jamhuri. Tangu mwanzoni mwa karne ya 19 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala na ukoloni wa Ufaransa. Burkina Faso ambayo hapo kabla ilikuwa ikiitwa Upper Volta, mnamo mwaka 1958 ilijitangazia utawala wa ndani wa jamhuri. Hata hivyo iliendelea kuwa sehemu ya Ufaransa. Miaka miwili baadaye yaani tarehe 5 Agosti 1960, Burkina Faso ilijipatia uhuru kamili sambamba na kukubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Mwaka 1984 jina la nchi hiyo lilibadilishwa rasmi kutoka Upper Volta na kuwa Burkina Faso. Nchi ya Burkina Faso ina ukubwa wa karibu kilomita mraba 274,000 na inapatikana Magharibi mwa Afrika ikipakana na nchi za Mali, Ivory Coast, Ghana, Togo, Benin na Niger. ***

Bendera ya Burkina Faso

 

Tags