Jan 22, 2022 02:35 UTC
  • Jumamosi, 22 Januari, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 19 Mfunguo Tisa Jamadithani 1443 Hijria mwafaka tarehe 22 Januari 2022.

Siku kama ya leo miaka 461 iliyopita inayosadifiana na tarehe 22 Januari 1561 alizaliwa mwanafalsafa na mtaalamu wa hesabati wa Uingereza Francis Bacon. Awali, Bacon alijishughulisha na masuala ya kisiasa na baadaye alikamatwa na kufungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kula rushwa. Kipindi cha kufungwa jela kilikuwa fursa mwafaka kwa Francis Bacon kudhihirisha kipawa chake. Mwanafalsafa huyo alitoa mchango mkubwa katika kueneza sayansi asili nchini Uingereza na kuhuisha sayansi na falsafa barani Ulaya. Bacon ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha New Atlantis. Msomi huyo wa Uingereza alifariki dunia mwaka 1626. ***

Francis Bacon

 

Siku kama ya leo miaka 247 iliyopita, alizaliwa Andre Marie Ampere, mtaalamu wa hisabati na fizikia wa Ufaransa. Akiwa kijana mdogo alipendelea sana fani ya hesabati. Akiwa Chuo Kikuu cha Polytechnique cha mjini Paris, aligundua mambo kadhaa katika uga wa fizikia. Moja ya mambo aliyoyagundua Andre Marie Ampere ni pamoja na simu ya upepo "Telegrafu." Mtaalamu huyo alifariki dunia mwaka 1836. ***

Andre Marie Ampere

 

Katika siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, alifariki dunia Alexandrina Victoria, malikia maarufu wa Uingereza akiwa na umri wa miaka 82. Victoria alizaliwa mjini London mwaka 1819 Miladia, huku akichukua nafasi ya William IV kiutawala ambapo alisalia katika madaraka kwa kipindi cha miaka 64. Katika utawala wa Alexandrina Victoria, kulishtadi ukandamizaji dhidi ya raia wa nchi hiyo. Kufariki dunia malikia huyo ilikuwa mwanzo wa kudhoofika utawala wa kifalme ambapo baada yake aliingia madarakani Edward VII. ***

Alexandrina Victoria,

 

Miaka 82 iliyopita katika siku kama ya leo Sayyid Nassir Hussein Musawi Hindi fakihi na mtaalamu wa elimu ya hadithi aliaga dunia. Msomi huyo aliyejulikana kwa lakabu ya Shamsul-Ulamaa ni mtoto wa Sayyid Hamid Hussein mmoja wa Maulamaa wakubwa wa India ambaye aliwahi pia kuwa Mufti. Sayyid Nassir Hussein Musawi Hindi alizaliwa tarehe 19 Jamadithani 1284 Hijria. Alisoma kwa baba yake na kwa Sayyid Muhammad Abbas na kufanikiwa kukwea daraja za kielimu. Msomi huyo hakuwa nyuma pia katika uandishi wa vitabu ambapo baadhi ya athhari zake ni Diwanul-Khutwab, al-Mawaidh, Diwanus-Shiir na Nafahatul-Azhar Fi Fadhail al-At'har. ***

Sayyid Nassir Hussein Musawi Hindi

 

Na miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo, katika kuendelea upinzani wa wananchi Waislamu wa Iran  dhidi ya utawala wa Shah watu wengi waliuawa na kujeruhiwa katika mapambano yao na wanajeshi. Wananchi wa Iran walikuwa wakisubiri kwa hamu na shauku kubwa kurejea  nchini Imam Khomeini kutoka uhamishoni ambapo kulikuwa kumefanyika maandalizi ya lazima kwa ajili ya mapokezi hayo makubwa ya kihistoria ya Imam Khomeini. Kwa mnasaba huo, kukaundwa kamati iliyojumuishwa viongozi wa dini na wawakilishi wa matabaka mbalimbali ya wananchi mjini Tehran kwa ajili ya shughuli ya mapokezi hayo. Wananchi wengi pia kutoka miji mbalimbali ya Iran walifunga safari na kuelekea Tehran ili washiriki katika shughuli ya kumpokea Imam Khhomeini. ***

 

Tags