Jan 23, 2022 02:35 UTC
  • Jumapili, 23 Januari, 2022

Leo ni Jumapili tarehe 20 Mfunguo Tisa Jamadithani 1443 Hijria sawa na tarehe 23 Januari 2022.

Siku kama ya leo miaka 1451 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Bibi Fatima Zahra, binti mtukufu wa Mtume Muhammad (saw). Bibi Fatima Zahra alilelewa katika nyumba ya wahyi na chini ya malezi bora na mwongozo wa baba yake Mtume Muhammad (saw) na hivyo kuweza kufikia daraja za juu za ukamilifu. Bibi Fatima (as) alikuwa na nafasi kubwa katika kukabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikimkabili baba yake kutoka kwa washirikina. Mwaka wa pili Hijiria, Bibi Fatima Zahra alifunga ndoa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) ambaye ni dhihirisho la haki, uadilifu na uchaji-Mungu katika sherehe ndogo iliyosimamiwa na Mtukufu Mtume Muhammad (saw). Vilevile Bibi Fatima akiwa na Imam Ali alifanikiwa kulea shakhsia adhimu kama Hassan, Hussein na Bibi Zainab (as). Mbali na majukumu ya kulea familia, Bibi Fatima Zahra, alijishughulisha pia na malezi ya jamii. *** 

 

Miaka 190 iliyopita katika siku kama ya leo Edouard Manet mchoraji mahiri wa Kifaransa alizaliwa. Awali Edouard alikuwa na mapenzi makubwa na ubaharia. Hata hivyo baadaye alianza kujihusisha na uchoraji na kuonyesha kipaji kikubwa katika sanaa hiyo. Kazi zake ziliwavutia wengi. Edouard Manet aliaga dunia 1883. ***

Edouard Manet

 

Katika siku kama ya leo miaka 124 iliyopita alizaliwa Sergei Mikhailovich Eisenstein mwananadharia na muongozaji wa filamu wa nchini Russia.  Aliongoza na kutengeneza filamu yake ya kwanza mwaka 1925 iliyojulikana kwa jina la Strike yaani mgomo. Filamu ya pili ya Sergei Mikhailovich Eisenstein iliyojulikana kwa jina la Battleship Potemkin ilileta mageuzi makubwa katika Sanaa ya filamu na sinema ulimwenguni. Miongoni mwa athari nyingine za Mikhailovich ni Seed of Freedom, Ten Days that Shook the World na Time in the sun. Mwongozaji filamu huyo aliaga dunia 1948.***

Sergei Mikhailovich Eisenstein

 

Miaka 123 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alizaliwa huko Khomein Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ruhullah al-Musawi Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul-Karim Hairi na Muhammad  Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa zaidi za kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa. Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha karibu miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.***

Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ruhullah al-Musawi Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 

Katika siku kama ya leo miaka 103 iliyopita yaani tarehe 23 Januari 1919, Chama cha Kifashisti cha Italia kiliasisiwa na Benito Mussolini. Wanachama wa chama hicho walikuwa wakivaa mashati meusi kama sare zao. Sare hiyo ilipelekea wafuasi wa chama hicho kujulikana kwa jina la watu wa " Mashati Meusi'.'' Fikra za Kifashisti zilikuwa zimejengeka juu ya misingi ya kuunda dola moja kubwa la kidikteta na fikra hizo zilikuwa zikipingana na aina yoyote ya uhuru. Oktoba mwaka 1922, Benito Mussolini na wafuasi wake waliuteka mji wa Roma na yeye mwenyewe akashika hatamu za uongozi akiwa Waziri Mkuu. Kuanzia hapo kiongozi huyo alianza kutekeleza malengo na sera za Chama cha Kifashisti. Hata hivyo mwaka 1945, mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia Benito Mussolini alitiwa mbaroni na wazalendo na kisha akanyongwa. ***

Benito Mussolini

 

Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo, Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) liliutangaza mji wa Baitul Muqaddas ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu, kuwa mji mkuu wa utawala huo badala ya Tel Aviv. Uamuzi huo uliofikiwa na Bunge hilo miaka miwili tu baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Wapalestina, uliwakasirisha mno Waarabu na Waislamu. Njama hiyo ya Israel iliyolenga kupata ridhaa ya nchi nyingine ili ziutambue rasmi mji huo kama mji mkuu wake na hivyo zihamishie balozi zao katika mji huo, haikuwa na natija, kwani hadi leo mji wa Tel Aviv ungali unatambuliwa kama mji mkuu wa utawala huo vamizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. ***

Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset)

 

Na siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Bahman 1357 Hijria Shamsia, baada ya kupatikana uhakika kuhusiana na uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea Iran akitokea uhamishoni Ufaransa, kuliundwa kamati ya mapokezi ya Imam Khomeini. Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 50,000 ikiwa na mjumuisho mkubwa wa wawakilishi kutoka vyama na makundi mbalimbali ya mapinduzi. Jukumu kuu la kamati hiyo lilikuwa ni kumpokea Imam Khomeini, kumlinda, kuweka nidhamu, kulinda usalama na kudhamini mambo ya lazima kwa ajili ya kurejea Imam Khomeini. ***

Mapokezi  ya Imam Khomeini

 

Tags