Jan 24, 2022 02:39 UTC
  • Jumatatu tarehe 24 Januari 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 21 Jamadithani 1443 Hijria sawa na tarehe 24 Januari 2022.

Siku kama ya leo miaka 1059 iliyopita yaani sawa na tarehe 21 Jamaduth-Thani mwaka 384 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya kauli za kihistoria, alifariki dunia Muhsin Bin Ali Tanukhi, mtaalamu wa fasihi, malenga na mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu. Tanukhi alikuwa na kipawa katika uga wa kuhifadhi mashairi na fasihi ambapo ameacha turathi ya mashairi. Aidha kwa muda mfupi Muhsin Bin Ali Tanukhi alikwea hatua za kielimu na kidini katika zama zake na kisha akajishughulisha na kazi ya ukadhi. Kitabu cha ‘al Faraj Baada sh-Shiddat’ kinachozungumzia matukio ya kihistoria na kijamii ya zama zake, ni miongoni mwa athari zilizoandikwa na msomi huyo. Kitabu kingine cha msomi huyo ni ‘Al-Masaajid’ ambacho hekaya na masuala ya akhlaqi na maadili mema.

Siku kama ya leo miaka 355 iliyopita, mkataba wa Breda ulitiwa saini kati ya Uingereza na Uholanzi. Kwa mujibu wa mkataba huo, Uholanzi ambayo haikuwa na uwezo wa kulinda makoloni yake katika bara lililokuwa ndio kwanza limegunduliwa la Amerika, iliyakabidhi makoaloni yake hayo kwa Uingereza. Eneo muhimu ambalo Uingereza ilikabidhiwa ni New York, ambalo leo kijiografia linapatikana mashariki mwa Marekani.

Katika siku kama ya leo miaka 163 iliyopita, kisima cha kwanza kabisa cha mafuta katika historia kilichimbwa huko Pennsylvania nchini Marekani. Kisima hicho kilichimbwa na Edwin Laurentine Drake kikiwa na kina cha urefu wa mita 230. Uchimbaji wa kisima hicho uliendelea kwa kipindi cha mwaka mmoja. Vifaa vilivyotumika kuchimbia kisima hicho vimehifadhiwa hadi leo katika jumba moja la makumbusho nchini Marekani.

Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Winston Churchill, mwanasiasa maarufu wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 91. Churchill alizaliwa mwaka 1874 na mwaka 1895 alijiunga na jeshi la Uingereza na kushiriki katika vita vya kikoloni. Mwaka 1900 Winston Churchil aliingia katika Bunge la Uingereza akikiwakilisha chama cha Kihafidhina na mara kadhaa aliongoza wizara mbalimbali na kwa vipindi viwili alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.

Winston Churchill

Siku kama hii ya leo miaka 43 iliyopita sawa na tarehe 4 Bahman mwaka 1357 Hijria Shamsiya, Shapour Bakhtiar Waziri Mkuu wa utawala wa Shah ambaye alikuwa akielewa kuwa kurejea Imam Khomeini nchini kutoka uhamishoni Paris kungempokonya udhibiti wa hali ya mambo, alitoa amri ya kufungwa viwanja vyote vya ndege vya Iran ili kuzuia kurejea nchini Imam Khomeini. Shapour Bakhtiar alichukua hatua hiyo baada ya kuchapishwa habari ya kukaribia kuwasili hapa nchini Imam Khomeini kutoka uhamishoni huko Paris Ufaransa. Hatua hiyo ya serikali ya utawala wa Shah iliwakasirisha wananchi ambao walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa ujio huo wa Imam Ruhullah Khomeini nchini Iran.

Shapour Bakhtiar

 

Tags