Jan 24, 2022 08:15 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Jan 24

Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia.

CAFA Futsal; Wanawake wa Iran wang'ara

Timu ya taifa ya futsal ya wanawake ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendelea kusajili matokeo mazuri katika Mashindano ya Ubingwa wa Bara Asia ya mwaka huu 2022. Akina dada hao wa Iran waliibamiza Tajikistan mabao 12-0 siku ya Jumamosi katika soka hiyo inayochezewa ukumbini. Mabao ya Iran katika mchezo huo yalifungwa na Fereshteh Karimi (3), Sara Shirbeigi (3), Sahar Papi (2), huku Mahsa Ali Madad, Fatemeh Papi, Nesa Ahmadi na Fereshteh Khosravi kila mmoja akifunga bao moja. Kabla ya mchuano huo wa Jumamosi, timu hiyo ya wanawake wa Kiirani ya futsal ilikuwa imeichabanga Uzbekistan mabao 5-2.

Timu ya taifa ya futsal ya wanawake ya Iran

 

Timu nne za Asia ya Kati ambazo ni Tajikistan, Iran, Uzbekistan na Kyrgyzstan zinachuana katika mashindano hayo yanayofanyika katika Ukumbi wa Spoti jijini Dushanbe nchini Tajikistan. Mashindano hayo ya kikanda yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Asia ya Kati (CAFA) yalianza Januari 21, na yanatazamiwa kufunga pazia lake Januari 28.

Kombe la Asia; China yailaza Iran

Wakati ambapo timu ya soka ya ukumbini ya Iran inaendelea kung'ara jijini Dushanbe, wenzao wa kandanda walikuwa wanaadhibiwa na China katika mechi za Kombe la Asia jijini Mumbai nchini India. Katika mchuano wa Jumapili, timu ya mpira wa miguu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali kutandikwa mabao 7-0 na China. Mabao ya China katika mchuano huo yalifungwa na Wang Shuang (2), Wang Shanshan (2), Xiao Yuyi, na Tang Jiali, huku beki Fatemeh Adelei wa Iran akijifunga mwenyewe, kunako dakika ya 83. Iran iliyaanza mashindano haya kwa sare tasa ilkipokabana koo na mwenyeji India, na intazamiwa kushuka dimbani Jumatano kuvaana na China Taipei katika mchuano mwingine wa Kundi A. Mashindano hayo ya kibara yanaadaliwa na Shirikisho la Soka Asia (AFC).

Handiboli; Iran yatamba

Timu ya taifa ya mpira wa mikono ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Jumamosi ilikipata ushindi wa nne mfululizo baada ya kuichachafya Iraq katika mashindano ya Ubingwa wa Handiboli barani Asia mwaka huu 2022. Timu hiyo inayonolewa na Montoya Fernandez iliishukia jirani yake Iraq katika mechi hiyo iliyochezwa katika Ukumbi wa Spoti wa Wizara ya Michezo mjini Dammam, Saudi Arabia, kwa kuizaba magoli 28-25. Katika ya kitimutimu hicho cha wikendi, Iran ilikuwa imezitandika Australia, India na mwenyeji Saudi Arabia. Sasa ina kibarua cha kuzikabili timu nyingine za Kundi B, ambazo ni Kuwait na Bahrain Jumatatu na Jumatano mtawalia.

Timu ya taifa ya mpira wa mikono ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Kundi A linazijumuisha Saudi Arabia, Uzbekistan, Qatar Korea Kusini. Timu 18 zilipaswa kushiriki kwenye mashindano haya ya kieneo, lakini Thailand na Japan zikajiondoa. Timu tano zitakazofuzu kwenye mashindano hayo yanayomalizika Januari 31, zitajikatia tiketi kushiriki Mashindano ya Ubingwa wa Dunia kwa upande wa wanaume mwaka ujao 2023, ambapo Poland na Sweden zitashirikiana kuwa wenyeji wa michezo hiyo ya ulimwengu.

  AFCON; Raundi ya 16

Tuangazie sasa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) inayoendelea kurindima nchini Cameroon. Timu ya taifa ya soka ya Burkina Faso imetinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Afcon, baada ya kuishinda Gabon katika mchuano wa Jumapili. Mchuano huo uliishia kwa sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za ada na 30 za nyongeza, hivyo timu hizo zikalazimika kuingia kwenye mikwaju ya penati. Burkinabe imekuwa timu ya kwanza kutinga robo fainali ya michuano ya Afcon, kwa kuizaba Gabaon mabao 7-6 katika upigaji penati. Vijana wa Burkinabe sasa watavaana na Waarabu wa Tunisia, ambapo Jumapili walivuna ushindi wa aina yake, baada ya kuipepeta Nigeria bao 1 bila jibu mjini Garoua. Bao hilo la kipekee na la ushindi wa Tunisia lilitiwa kimyani na mchezai nguli Youssef Msakni.

Kombe la AFCON

 

Nigeria ilipoteza fursa kibao za kusawazisha mambo katika mchuano huo wa mchujo, sare ambayo angalau ingepelekea upigaji penati.  Hapo awali, mabingwa watetezi Algeria walitemwa katika kombe la mataifa ya Afrika kufuatia kichapo cha mabao 3 -1 dhidi ya Ivory Coast huko Douala. Algeria ilijikokota kwa tofauti ya magoli mawili katika kipindi cha mapumziko baada ya Ibrahim Sangare kupokea pasi safi kutoka kwa Franke Kessie na kulipachika goli wavuni. Nicolas Pepe anayeichezea Arsenal aliipatia Ivory Coast uongozi wa mabao 3-0 kabla ya nahodha wa Algeria Riyad Mahrez kupoteza penalti kwa kugonga mwamba. Sofiane Bendebka aliifungia Algeria bao la kufutia machozi dakika za mwisho na kuifanya sasa timu hiyo kuyaaga mashindano hayo kwa kuvuta mkia katika Kundi E. Huku hayo yakijiri, hatima ya Comoro ambayo iliibandua Ghana kwenye mashindano hayo katika mchuano uliowaacha wengi vinywa wazi, haijulikani. Hii ni kwa kuwa, huenda ikakumbwa na uhaba wa wachezaji katika mechi zake zijazo, kwa kuwa 12 miongoni mwao wamepatikana na maambukizi ya virus vya corona, wakiwemo walinda lango Ali Ahamada na Moyadh Ousseni. Shirikisho la Soka Afrika CAF halijawahi kuakhirisha mchuano wowote tangu mashindano haya yaanze Januari 9, licha ya timu kadhaa kuripoti kukumbwa na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.  Katika hatua nyingine, timu ya ya taifa ya soka ya Tanzania 'Taifa Stars' imeingia katika hatua ya makundi kwenye fainali za mataifa ya Afrika inayotarajiwa kufanyika 2023 nchini Ivory Coast. Tanzania na timu zingine 41 zitaingia moja kwa moja katika hatua ya makundi huku zikisubiri timu sita kutoka katika raundi ya awali na kuwa timu 48 ambazo zitakuwa katika makundi 12 (A-L). Stars imepata uhakika wa kuanzia hatua ya makundi baada ya kufanyika droo ya raundi ya awali huko Douala, Cameroon.

Dondoo za Hapa na Pale

Nyota wa Mbio za Nyika za Dunia 2019 Hellen Obiri ameibuka mshindi wa mbio 8000 kwenye mashindano ya mbio za nyika za Northern Ireland jijini Belfast, Jumamosi. Obiri alipigiwa upatu kufanya vyema uwanjani Billy Neill Country Park. Mtimkaji huyo, ambaye ananuia kutetea mataji yake ya dunia nchini Amerika na Jumuiya ya Madola nchini Uingereza baadaye 2022 katika mbio za mita 5,000, hakusikitisha aliponyakua taji kwa dakika 26:44. Afisa huyo wa jeshi ni Mkenya wa nne kutwaa taji hilo baada ya Alice Aprot mwaka 2016, Caroline Chepkoech Kipkirui (2017) na Margaret Chelimo (2018). Duru hii ilivutia karibu wakimbiaji 600 wakiwemo Wakenya Vincent Keter na Kamar Etyang waliotimka katika mbio za kilomita 10 za wanaume.

 

Mbali na hayo, mchezaji maarufu wa mchezo wa tenisi kutoka Kuwait amepongezwa kwa hatua yake ya kujiondoa katika shindano moja la kimataifa baada ya kubainika kuwa alitakiwa ashindane na raia wa utawala haramu wa Israel. Muhammad Al Awadi alijiondoa katika Mashindano ya J4 Dubai ambayo yamefanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuanzia Januari 17 hadi 22. Wanaharakati katika mitandao ya kijamii wamempongeza Mkuwaiti huyo kwa kukataa kuwa sehemu ya sera za kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unazikoloni na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Mwandishi maarufu wa Kuwait Saadie Mufreh Al Awadi amempongza mchezji tenisi huyo kutokana na msimamo wake imara na kusema hatua yake hiyo ni fahari kwa nchi yake. Mwanaharakati Mpalestina Al Yasser Al Zaatrah ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: "Nabusu paji la uso wako, umetoa pigo kwa wavamizi." Naye mwandishi habari wa Misri Wael Kandil amesema kijana huyo Mkuwaiti mwenye umri wa miaka 14 ameamua kutocheza katika shindano hilo la kimataifa ili kutotia dosari historia katika maisha yake kwa kucheza na Mzayuni. Naye mbunge mwandamizi wa Kuwait Osama al Shaheen ametuma ujumbe katika Twitter na kuandika: "Salamu na sukrani kwa shujaa wa Kuwait Muhammad al Awadi kutokana na hatua yake ya kupinga uhusiano wa kawaida wa kimichezo na Wazayuni."

Muhammad Al Awadi

 

Kwengineko, watetezi wa haki za wanawake nchini Ufaransa wamepinga vikali mpango uliopasishwa hivi karibuni na Baraza la Seneti la nchi hiyo ya bara Ulaya unaopiga marufuku uvaaji wa vazi la staha na heshima la hijabu katika mashindano ya michezo. Watetezi wa haki za wanawake nchini Ufaransa wamesema kuwa, wanapinga vikali mpango huo ambao unawazuia wanawake Waislamu kuvaa vazi la stara ya mwanamke wa Kiislamu hijabu katika mashindano ya michezo. Wiki iliyopita, Baraza la Seneti la Ufaransa lilipiga kura na kupasisha sheria inayopiga marufuku uvaaji wa vazi la stara na heshima la hijabu katika mashindano ya michezo. Hatua hiyo ambayo ni muendelezo wa chuki dhidi ya Uislamu inatarajiwa kuzusha makelele na malalamiko mengi wakati mji mkuu wa Ufaransa Paris unatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Olimpiki mwaka 2024. Wajuzi wa mambo wanasema kuwa, endapo marufuku hiyo itajumuisha mashindano ya kimataifa ya michezo ya Olimpiki itakayofanyika mjini Parsi mwaka 2024 huenda yakayafanya mashindano hayo kukabiliwa na changamoto kubwa. Hii ni kutokana na kuwa, kama wanamichezo Waislamu watasusia mashindano hayo itakuwa pigo kubwa hasa kwa kuzingatia kuwa, katika mashindano ya Olimpiki ya Tokyo 2020 wanamichezo Waislamu walikuwa na nafasi na hisa kubwa ya medali katika mashindano hayo.

……………….….TAMATI….………….

 

Tags