Jan 28, 2022 01:36 UTC
  • Ijumaa tarehe 28 Januari 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 25 Jamadithani 1443 Hijria sawa na 28 Januari 2022.

Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliendeleza utafiti wake wa masuala ya anga za mbali kwa kutuma kiumbe hai angani ikitumia roketi. Kiumbe huyo hai alikuwa tumbili ambaye alirejea ardhini salama katika utafiti huo. Majaribio hayo yaliyokuwa na mafanikio yaliwaonesha walimwengu mafanikio na maendeleo ya masuala ya anga ya Iran katika kipindi hicho cha vikwazo vizito vya kidhalimu vya Marekani na waitifaki wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Miaka 28 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Ayatullah Muhammad Ali Araki, mmoja wa marjaa wakubwa wa taqlidi wa Waislamu, akiwa na umri wa miaka 103. Mwanzuoni huyo wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Arak katikati mwa Iran na kujifunza elimu ya dini kwa maulamaa wakubwa hususan Ayatullahil Udhma Hairi. Ayatullah Muhammad Ali Araki alifundisha katika chuo kikuu cha kidini cha Qum kwa kipindi cha miaka 35 na kulea wanazuoni na wasomi hodari. Mwanazoni huyo mkubwa wa Kiislamu amezikwa katika Haram tukufu ya Maasuma (as) katika mji mtakatifu wa Qum.

Ayatullah Muhammad Ali Araki

Miaka 43 iliyopita katika siku kama hii ya leo, kundi kubwa la wanazuoni wa Kiislamu lilianzisha mgomo wa kuketi katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran baada ya Waziri Mkuu wa serikali ya wakati huo ya Shah, Shapoor Bakhtiyar, kumzuia Imam Khomeini kurejea nchini Iran akitokea uhamishoni. Wanazuoni hao walisema, sharti pekee la kusitisha mgomo huo ni kuruhusiwa Imam Khomeini kurejea nchini. Mgomo huo ulikuwa miongoni mwa matukio muhimu katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kwani kwa upande mmoja, serikali ya wakati huo ya Shah iliyokuwa ikiungwa mkono na Marekani, ilifanya jitihada kubwa za kumzuia Imam Khomeini asirejee nchini, na kwa upande mwingine ilikuwa ikifanya njama za kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi kwa kutoa ahadi na kutumia vitisho. Mgomo huo wa wanazuoni wa Kiislamu uliowashirikisha maulamaa mashuhuri kama Shahid Ayatullah Murtadha Mutahhari na Ayatullah Muhammad Beheshti, ulikifanya Chuo Kikuu cha Tehran kuwa kituo kikuu cha harakati za mapambano.

Mgomo wa wanazuoni wa Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Tehran

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita Shapoor Bakhtiyar, Waziri Mkuu kibaraka wa Shah wa Iran alitangaza kwamba ataelekea Paris, Ufaransa kwa shabaha ya kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu Imam Ruhullah Khomeini. Katika upande wa pili, Imam Khomeini alitangaza akiwa Paris kwamba, hamtambui Bakhtiyar kuwa ni Waziri Mkuu wa Iran, tofauti na uvumi uliokuwa ukienezwa wakati huo. Imam alisisitiza kuwa hatampokea wala kuzungumza na Waziri Mkuu wa Shah kabla hajajiuzulu. Siku hiyo hiyo wananchi wa Tehran walikusanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mehrabad kwa ajili ya kujiandaa zaidi na kutayarisha mipango ya kumpokea Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini (MA).

Shapoor Bakhtiyar

Miaka 134 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Husseini Shirazi alitoa fatuwa maarufu ya kuharamisha tumbaku ili kuzuia uporaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni wa Kiingereza katika nchi za Kiislamu. Fatuwa hiyo ilitolewa baada ya Mfalme Nasiruddin Shah wa Iran kutia saini mkataba wa kuipa kampuni moja ya utawala wa kikoloni wa Uingereza mamlaka ya kuuza na kununua tumbaku ya Iran kwa kipindi cha miaka 50. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa hiyo ya kuharamisha tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatua hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni. 

Ayatullah Mirza Shirazi