Jan 29, 2022 02:55 UTC
  • Jumamosi, 29 Januari, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 26 Mfunguo Tisa Jamadithani 1443 Hijria mwafaka na tarehe 29 Januari 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita vita vya Dhatus Salasil vilimalizika kwa Waislamu kujipatia ushindi. Vita hivyo vilianza baada habari kusambaa kuwa kikundi cha washirikina kilitaka kushambulia mji wa Madina. Baada ya habari hiyo kumfikia Mtume Mtukufu (saw), aliwaamuru baadhi ya Waislamu waende kukabiliana na washirikina hao wakiongozwa na kamanda mmoja aliyetoka upande wa Muhajirina. Hata hivyo baada ya kujua uwezo mkubwa waliokuwa nao maadui, kundi hilo la Waislamu lilirejea. Mtume alimtuma kamanda mwingine lakini naye pia alirejea na ndipo Mtume Mtukufu (s.a.w) alipomteua Ali bin Abi Twalib (a.s) aongoze Waislamu katika mapigano hayo. Imam Ali (as) aliwashambulia maadui kwa umahiri mkubwa na kurejea Madina na ushindi. ***

Vita vya Dhatus Salasil

 

Miaka 617 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, Sheikh Jamaluddin Miqdad Hilli Asadi, fakihi na msomi wa Kiislamu aliaga dunia huko Najaf, moja ya miji ya Iraq. Hakuna taarifa kuhusiana na tarehe yake ya kuzaliwa, lakini lililo bayana ni kwamba, alikuwa mwenyeji wa mji wa Hillah Iraq. Alikuwa mashuhuri baina ya Maulamaa kwa jina la Fadhil Miqdad na alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Muhammad bin Makki. Fadhil Miqdad ameacha turathi na dafina kubwa ya vitabu na miongoni mwa vitabu vyake ni Adab al-Hajj na Ayat al-Ahkam.***

Sheikh Jamaluddin Miqdad Hilli Asadi

 

Katika siku kama hii ya leo miaka 96 iliyopita alizaliwa mjini Punjab, mashariki mwa Pakistan, Mohammad Abdus Salam, mwanafizikia mkubwa wa nchi hiyo. Alikuwa na juhudi kubwa kwenye masomo tangu akiwa kijana mdogo na akiwa na umri wa miaka 14 alijiunga na Chuo Kikuu cha mjini Punjab. Baada ya kupata shahada ya uzamili katika chuo kikuu hicho, Abdus Salam alijiunga na chuo kikuu cha Cambridge nchini Uingereza. Hatimaye akiwa katika chuo hicho, Abdus Salam alijiunga na taaluma ya fizikia ambapo mwaka 1951 alifanikiwa kupata tuzo ya Adams. Katika mwaka huo huo msomi huyo alirejea nchini kwake na kujishughulisha na kazi ya ukufunzi. Hata hivyo kukosekana kwa zana na vitendeakazi, kulimfanya arejee tena nchini Uingereza na baadaye kusafiri latika nchi nyingi za Ulaya ambapo aliongoza taasisi kadhaa za kielimu barani humo. Mohammad Abdus Salam, alifariki dunia mwaka 1996. ***

Mohammad Abdus Salam

 

Tarehe 29 Januari miaka 59 iliyopita alifariki dunia mshairi wa Kimarekani Robert Frost. Malenga huyo alizaliwa mwaka 1874. Kipaji chake kikubwa katika sanaa ya mashairi kilimuwezesha kuandika diwani yake ya kwanza ya mashairi akiwa na umri wa miaka 20. Frost aliipa diwani hiyo ya mashairi jina la "A Boy's Will". Malenga huyo mara kadhaa alitunukiwa tuzo ya usanii ya Pulitzer.***

Robert Frost.

 

Na siku kama ya leo miaka 43 iliyopita yaani tarehe 10 Bahman 1357 Hijria Shamsia, wahadhiri na matabaka mengine ya wananchi walitangaza mshikamamo wao na kuamua kuungana na viongozi wa kidini waliokuwa wamekusanyika katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran nchini Iran kuupinga utawala wa Shah. Katika hali ambayo idadi ya watu katika mkusanyiko ilikuwa ikiongezeka kila dakika, Shapour Bakhtiyar, Waziri Mkuu kibaraka wa utawala wa Shah alilazimika kukubali Imam Khomeini arejee nchini Iran kutoka uhamishoni nchini Ufaransa. Sambamba na hayo ndege za kijeshi za Marekani zilianza kuwaondoa raia wa nchi hiyo nchini Iran. ***

 

Tags