Mar 12, 2022 00:01 UTC
  • Jumamosi, 12 Machi, 2022

Leo ni Jumamosi mwezi 9 Shaaban 1443 Hijfria mwafaka na tarehe 12 Machi 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 962 iliyopita aliaga dunia Ibn Barraj mmoja wa mafaqihi na maulamaa mashuhuri wa Misri. Ibn Barraj alifahamika sana kwa jina la Trablosi kutokana na kuwa kwa muda fulani alikuwa na cheo cha kadhi katika mji wa Trablos yaani Tripoli huko kaskazini mwa Lebanon ya sasa. Msomi huyo wa Kiislamu alifunzwa na maulamaa kama vile Sayyid Murtadha na Sheikh Tusi. Ibn Barraj ni msomi mtajika wa Kiislamu ambaye fikra na mitazamo yake ilikuwa ikiheshimiwa na mafaqihi wakubwa wa zama hizo. ***

Ibn Barraj mmoja wa mafaqihi na maulamaa mashuhuri wa Misri. Ibn Barraj

 

Katika siku kama ya leo miaka 866 iliyopita inayosadifiana na tarehe 9 Shaaban mwaka 577 aliaga dunia Abul Barakat Abdul Rahman bin Muhammad mashuhuri kwa lakabu ya Ibn Anbari fakihi na mtaalamu wa lugha wa mjini Baghdad. Alihitimu masomo yake katika skuli mashuhuri ya Nidhamiya mjini Baghdad na kutokana na kufaulu vizuri masomo yake na maarifa mengi aliyokuwa nayo, alianza kufundisha katika skuli hiyo. Ibn Anbari ameandika vitabu na makala nyingi za kielimu. Kitabu cha al-Asrar al-Arabiyah ni moja ya athari mashuhuri ya alimu huyo. ***

Abul Barakat Abdul Rahman bin Muhammad mashuhuri kwa lakabu ya Ibn Anbari

 

Miaka 97 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Sun Yat-sen mwanamapinduzi na Rais wa Kwanza wa China. Sun Yat-sen anayejulikana kama baba wa taifa la China alizaliwa mwaka 1866 huko Nanlang China. Mwaka 1892 alijiunga na Chuo Kikuu na akiwa na umri wa miaka 26 alifanikiwa kupata shahada ya udaktari. Uwanja na mazingira ya Sun Yat-sen ya kuanzisha harakati zake za kisiasa yaliandaliwa baada ya Japan kuishambulia China mnamo mwaka 1894. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanzisha harakati zake dhidi ya mfumo wa kifalme wa Manchu. Baada ya harakati hiyo kushindwa alikimbilia nje ya nchi. Mwaka 1905 alirejea China na kuanzisha Muungano wa Wanamapinduzi wa China lengo likiwa ni kuleta demokrasia katika nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1911 utawala wa familia ya kifalme ya Manchu ulifikia tamati baada ya kupinduliwa. Tukio hilo lilipelekea kutangazwa mfumo wa Jamhuri nchini China na Sun Yat-sen alifanikiwa kushika hatamu za uongozi akiwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya China. ***

Sun Yat-sen

 

Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Machi 1930 ilianza harakati kubwa ya uasi iliyoongozwa na Mahatma Gandhi, kiongozi wa mapambano ya kupigania uhuru wa India. Harakati hiyo kubwa ambayo iliwashirikisha wazalendo na wapigania uhuru wa India, ilifanyika kwa shabaha ya kukabiliana na maamuzi mapya ya serikali ya kikoloni ya Uingereza kuhusu ongezeko la ushuru wa chumvi. Katika kukabiliana na sheria hiyo ya kidhalimu, Mahatma Gandhi na wenzake elfu 78 walianza kutayarisha chumvi kutoka maji ya baharini. Wakoloni wa Uingereza walikabiliana na harakati hiyo kwa kuwatia nguvuni makumi ya maelfu ya Wahindi na kuwatia korokoroni. Hali hiyo ilisababisha ghasia na vurugu katika idara za serikali. Mapambano hayo ya Mahatma Gandhi yaliilazimisha serikali ya kikoloni ya Uingereza kusalimu amri na kulegeza misimamo yake. ***

Mahatma Gandhi

 

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita sawa na tarehe 12 Machi 1968 nchi ndogo ya Mauritius iliyoko kusini mwa Afrika ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Waholanzi waliingia Mauritius katika karne ya 17 na wakafuatiwa na Wafaransa karne moja baadaye. Mwaka 1814 Waingereza walikivamia kisiwa cha Mauritius na kukiunganisha na makoloni yao. Kisiwa hicho kina ukubwa wa kilomita mraba elfu mbili hivi na jamii ya zaidi ya watu milioni moja. **

Bendera ya  Mauritius 

 

Na katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita yaani tarehe 21 Esfand 1363 Hijria Shamsia, Ayatullah Mahmoud Ansari Qomi, mmoja wa Maulamaa mashuhuri wa Tehran aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1300 katika mji mtakatifu wa Qom ulioko kusini mwa mji mkuu Tehran. Baba yake aliaga dunia wakati yeye akiwa na umri wa miak 10 na kaka zake kuchukua jukumu la kumlea ambapo ndi kipindi hicho pia alisoma masomo ya msingi ya Kiislamu. Baadaye alielekea Najaf Iraq na kunufaika na bahari ya elimu ya waalimu mahiri wa zama hizo. Ansari Qomi alifanikiwa kupata ijaza ya kunukuu hadithi pamoja na Ijtihadi kutoka kwa Maulamaa kadha wa Iran na Iraq. Mwanazuoni huyu ameacha pia athari ya vitabu muhimu hasa katika elimu ya fikihi, usul na tafsiri. ***

Ayatullah Mahmoud Ansari Qomi,

 

Tags