Mar 17, 2022 22:26 UTC
  • Ijumaa tarehe 18 Machi 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 15 Shaaban inayosadifiana na tarehe 18 Machi mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1188 iliyopita alizaliwa Imam Mahdi (as) mwokozi wa ulimwengu katika mji wa Samarra Kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq. Yeye ni mwana mpendwa wa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa lakabu mashuhuri za Imam huyo wa Zama ni Mahdi, ambayo ina maana ya mtu aliyepewa hidaya na kuongozwa, na al Qaim, kwa maana ya atakayeanzisha mapambano. Imam Mahdi alipitisha miaka mitano ya kwanza ya uhai wake akiwa na baba yake mpendwa, Imam Askari (as). Alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu kama Imam baada ya kuuawa shahidi baba yake mtukufu na kisha akatoweka na kwenda ghaiba kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu. Kwa muda wa miaka 69 mtukufu huyo alikuwa akiwasiliana na kuwaongoza Waislamu kupitia wawakilishi wake maalumu. Baada ya hapo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Imam Mahdi alienda kwenye ghaiba kubwa na ya muda mrefu na atadhihiri tena ulimwenguni wakati mwafaka ambao Mwenyezi Mungu ataona unafaa. Atakapodhihiri duniani, ataujaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa baada ya kujaa dhulma na uonevu. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo huadhimishwa nchini Iran kama Siku ya Waliodhulumiwa Duniani.

Siku kama ya lao miaka 209 iliyopita, alizaliwa Christian Friedrich Hebbel mwanafasihi na mkosoaji mkubwa wa Ujerumani. Akiwa kijana mdogo na kutokana na kufariki dunia baba yake, alilazimika kufanya kazi katika kiwanda cha kuchapisha magazeti kwa lengo la kujidhaminia mahitaji yake. Hata hivyo baada ya kufanya tafiti kadhaa na kujiongezea maarifa, alianza kazi ya uandishi. Akiwa na umri wa miaka 20 Christian Hebbel alianza kusambaza Makala zake kwa ajili ya kuchapishwa katika magazeti ya fasihi ya mjini Hamburg, Ujerumani. Baada ya hapo alijiendeleza zaidi kielimu ambapo sambamba na kuendelea na masomo pia alikuwa akijihusisha na kazi za fasihi na kuandika michezo ya sinema mbalimbali ambapo pia katika uwanja huo ameacha athari katika uga wa fasihi na nadharia za ukosoaji. Hebbel alifariki dunia mwaka 1863 Miladia akiwa na umri wa miaka 50.

Christian Friedrich Hebbel

Miaka 164 iliyopita katika siku kama leo, alizaliwa mvumbuzi mashuhuri wa Kijerumani, Rudolf Diesel, ambaye alibuni injini ya diseli. Diesel alifanya utafiti na uhakiki mkubwa kuhusu injini za mitambo mbalimbali na akafanikiwa kuvumbua chombo ambacho kinaweza kuzalisha nishati kubwa zaidi bila ya kuhitaji umeme lakini kwa kutumia nishati ya kawaida na rahisi zaidi. Chombo hicho ambacho kilipewa jina lake mwenyewe la Diesel kilileta mabadiliko makubwa katika sekta ya viwanda na usafirishaji kwa kadiri kwamba licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia lakini injini za diseli zingalia zinatumika kwa kuwa ni zenye nguvu kubwa na zinazotumia nishati ndogo. Rudolf Diesel alifariki dunia mwaka 1913.

Rudolf Diesel

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, Mahatma Gandhi, kiongozi mpigania uhuru wa India aliyekuwa akifanya jitihada za kuiondoa nchi hiyo katika ukoloni wa Uingereza kwa njia ya amani alikamatwa na baadaye kuhukumiwa kifungo cha miaka 6 jela. Kutiwa mbaroni Gandhi kulizidisha hasira na chuki za wananchi wa India dhidi ya Waingereza na kutia nguvu azma yao ya kupambana kwa ajili ya kuikomboa nchi yao. Katika mapambano yake Gandhi alitumia mbinu iliyoitwa 'Satyagraha' ambayo inamaanisha kutafuta hakika na kweli. Mbinu hiyo isiyotumia mabavu na ghasia, ilikusudiwa kudhihirisha makosa ya adui na kumlazimisha abadili mwenendo wake.

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, hatimaye mapambano ya wananchi Waislamu wa Algeria yaliyoanzishwa kwa lengo la kuikomboa nchi hiyo na kukomesha uvamizi wa kikoloni wa Ufaransa yalipata ushindi baada ya miaka minane ya vita vikali. Watu milioni moja waliuawa katika vita hivyo. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa pili wa Evian, Ufaransa ilitambua uhuru wa Algeria na kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo. Hata  hivyo jeshi la siri la Ufaransa liliendeleza operesheni za kigaidi kwa muda nchini Algeria. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Algeria wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Yusuf bin Khada na baadaye nchi hiyo ikawa chini ya utawala wa Ahmad bin Bella.

Tags