Mar 20, 2022 02:41 UTC
  • Jumapili, 20 Machi, 2022

Leo ni Jumapili tarehe 17 Shaaban 1443 Hijria mwafaka na tarehe 20 Machi 2022.

Tarehe 20 Machi miaka 295 iliyopita, alifariki dunia Isaac Newton mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 84. Alizaliwa mwaka 1643 na kusoma katika Chuo Kikuu cha Cambridge. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy. ***

Isaac Newton

 

Katika siku kama ya leo miaka 82 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sheikh Hassanali Isfahani, arif, msomi na mwanazuoni aliyekuwa amebobea katika taaluma ya fiqhi. Alizaliwa mwaka 1279 Hijria huko Isfahan katikati mwa Iran na akaanza mapema mno kusoma elimu mbalimbali kama fiqhi, usul, mantiki na falsafa. Ayatullah Isfahani akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu, alielekea Najaf nchini Iraq na baadaye Mash’had, Iran na kubakia huko hadi mwisho wa umri wake. Ayatullah Isfahani alibobea pia katika elimu za hisabati, nujumu na tiba. Hata hivyo alikuwa mashuhuri zaidi katika baadhi ya elimu kama irfan na akhlaq. Umashuhuri mkubwa zaidi wa msomi huyo unatokana na uchamungu wake mkubwa na karama zake ambazo ni matokeo ya kujipinda katika ibada, kuitakasa nafsi na uchamungu mkubwa. Baadhi ya karama za Ayatullah Isfahani zimenukuliwa mwanaye katika kitabu alichokipa jina la "Alama za Wasio na Alama". *** 

Sheikh Hassanali Isfahani

 

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 29 Esfand 1329 Hijria Shamsia, baada ya vuta nikuvute na mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya mkoloni Mwingereza na utawala kibaraka wa mfalme hapa nchini, hatimaye wabunge wa Bunge la Taifa na lile la Seneti walipitisha muswada wa kutaifisha sekta ya mafuta nchini. Kupitishwa muswada huo ilikuwa hatua muhimu katika mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya mkoloni Mwingereza. Kufuatia kupasishwa sheria hiyo, Muswadiq aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Iran kwa kuungwa mkono wa wananchi na viongozi wa kidini hasa Ayatullah Kashani. ***

Kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran na kufanywa kuwa mali ya taifa

 

Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 20 Machi 1956, nchi ya Tunisia iliyoko katika eneo la kaskazini mwa Afrika ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Ijapokuwa harakati za ukombozi nchini humo zilianza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, lakini kutokea Vita vya Pili vya Dunia na kudhoofika Ufaransa kwenye vita hivyo, kuliandaa mazingira mazuri ya kujikomboa nchi hiyo. Baada ya kujipatia uhuru, Habib Bourguiba aliongoza nchi hiyo, kwa karibu miongo mitatu lakini kwa mabavu na ukandamizaji. Baada ya utawala wa Bourguiba, nchi hiyo ilitawaliwa na Zainul Abidin Ben Ali ambaye aliingia madarakani mwaka 1982. Kiongozi huyo naye alifuata mbinu na mwendo uleule wa Bourguiba wa kuwakandamiza wananchi na kupiga vita Uislamu, suala lililopelekea wananchi wa nchi hiyo kusimama kidete na kumng'oa madarakani mwezi Januari mwaka 2011. ***

Tunisia

 

Miaka 58 iliyopita katika siku kama ya leo, Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa hotuba na kuwataka wananchi wa Iran wasifanye sherehe za Nairuzi za mwaka mpya wa Kiirani wa 1342 ili kulalamikia hatua zisizo za kisheria za utawala wa kifalme wa Kipahlavi. Nairuzi ni sherehe za kitaifa za Wairani ambazo hufanywa kila mwanzoni mwa mwaka wa Kiirani. Katika kipindi chote cha mwaka 1341 Hijria Shamsia utawala wa kidikteta wa Shah ulichukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha misingi ya utawala wake na kwa ajili ya kuyaridhisha madola ya kigeni hususan Marekani. Imam Khomeini kwa uono mpana na kutazama mustakbali wa mambo akiwa pamoja na maulama wengine aliitangaza sikukuu ya Nairuzi kuwa mambolezo ya umma ili kubatilisha propaganda za utawala wa Kipahlavi za kuhalalisha hatua zake za hiana. Kwa muktadha huo, wananchi na viongozi wa kidini walifanya vikao vya maombolezo katika pembe mbalimbali za Iran. Ubunifu huu wa Imam Khomeini ulikuwa na taathira kubwa kiasi kwamba, katika siku ya pili ya sikukuu ya Nairuzi maafisa wa utawala wa Shah walishambulia mkusanyiko wa matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini) katika mji wa Qum waliokuwa wakifanya maombolezo na kuwauwa shahidi na kuwajeruhi baadhi yao. ***

 

Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, vikosi waitifaki wa Marekani na Uingereza waliishambulia kijeshi Iraq kwa kisingizio cha nchi hiyo kuzalisha silaha za mauaji ya umati. Hatua hiyo ilichukuliwa licha ya malalamiko makubwa ya walimwengu. Kufuatia vita hivyo vya umwagaji damu, zaidi ya makombora 1000 ya cruise, maelfu ya mabomu na makumi ya maelfu ya mizinga na mabomu ya vishada yalimiminiwa wananchi wasio na hatia wa Iraq. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wa Kiiraqi waliuawa katika vita hivyo. Aidha nyumba zisizo na idadi za Wairaqi, hospitali, taasisi za kiuchumi, kiutamaduni na misikiti ilibomolewa.

Tags