Mar 23, 2022 02:45 UTC
  • Jumatano tarehe 23 Machi mwaka 2022

Leo ni Jumatato tarehe 20 Shaabani 1443 Hijria sawa na Machi 23 mwaka 2022.

Katika siku kama ya leo miaka 1058 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria na mtaalamu maarufu wa vitabu wa Kiislamu Ebn al Nadeem. Ibn Nadeem alipata umaarufu kutokana na kitabu cha "al Fehrest". Katika kitabu hicho Ibn Nadeem aliarifisha taaluma na elimu zote zilizokuwepo katika zama hizo na kutoa maelezo na wasifa wa wasomi mashuhuri wa elimu hizo. Kitabu hicho kinakusanya maelezo kamili kuhusu maulamaa na wasomi wa Kiislamu wa zamani hadi kufikia zama za Ibn Nadeem.

Siku kama ya leo miaka 370 iliyopita, yaani sawa tarehe 23 Machi mwaka 1652, yalianza shambulizi la manowari za kijeshi za Uingereza dhidi ya majeshi ya Uholanzi. Amri ya shambulizi hilo ilitolewa na Oliver Cromwell aliyekuwa dikteta wa wakati huo wa Uingereza. Akipata uungaji mkono wa Bunge la Uingereza, Cromwell alimpindua mfalme wa Uingereza na kisha kulivunja bunge la nchi hiyo. Inasemekana kuwa, lengo la kutekeleza shambulio hilo lilikuwa ni kulimaliza nguvu jeshi la Uholanzi ambalo lilikuwa na nguvu kubwa ya majini.

Oliver Cromwell

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, ilianzishwa harakati ya Ufashisti nchini Italia kwa uongozi wa Benito Mussolini. Ufashisti kwa ujumla ni utawala wa kidikteta wenye kufuata aidolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani, kukandamiza uhuru na kuzipotosha itikadi na fikra za wananchi. Hayo yalijiri baada ya Mussolini kunyakuwa wadhifa wa uwaziri mkuu nchini Italia mwaka 1922 na kuanza utawala wa kidikteta nchini humo. Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler, na kuandaa mazingira ya kuanzishwa Vita vya Pili vya Dunia.

Benito Mussolini

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, liliasisiwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani 'WMO'. Shirika hilo linafungamana na Umoja wa Mataifa na taasisi zote za hali ya hewa ulimwenguni hushirikiana na shirika hilo. Miongoni mwa malengo ya kuanzishwa shirika hilo ni kutoa msaada wa elimu ya hali ya hewa kwa wataalamu wa anga, mabaharia, wakulima na shughuli nyingine za kibinadamu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana siku ya leo yaani tarehe 23 Machi ikajulikana kuwa Siku ya Hali ya Hewa Duniani.

Na siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, sawa na tarehe 3 Farvardin 1384 Hijria Shamsia, alifariki dunia Allamah Sayyid Jalaluddin Ashtiyani, mwanafalsafa na mwanafikra wa Kiislamu baada ya kuugua kwa muda mrefu. Allamah Ashtiyani alizaliwa Ashtiyan katikati mwa Iran na kupata elimu ya msingi katika eneo hilo. Baadaye alielekea katika mji wa Qum na kupata elimu kwa wanachuoni wakubwa kama vile Imam Ruhullah Khomeini, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai. Baadaye alielekea katika mji mtakatifu wa Mash'had na kujishughulisha na kulea wanafunzi hadi mwisho wa uhai wake.

Allamah Sayyid Jalaluddin Ashtiyani

 

Tags