Mar 29, 2022 01:28 UTC
  • Jumanne tarehe 29 Machi mwaka 2022

Leo ni Jumanne tarehe 26 Shaabani 1443 Hijria sawa na 29 Machi mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1338 iliyopita, alifariki dunia, Yazid bin Abdul-Malik bin Marwan, khalifa dhalimu wa wakati huo. Yazid bin Abdul-Malik aliingia madarakani baada ya kufariki dunia Omar bin Abdul-Aziz hapo mwaka 101 Hijiria. Kiongozi huyo mbali na kufanya dhulma na ukandamizaji, hakuzingatia pia masuala ya Waislamu. Kwa kuzingatia kuwa alikuwa ni mtu wa karibu na ukoo wa Hajjaj Thaqafi, hivyo aliwapa umuhimu mkubwa watu wa ukoo huo.

Siku kama ya leo miaka 688 iliyopita, alifariki dunia Ibn Fasih, aliyekuwa faqihi, malenga na mtaalamu wa lugha ya Kiarabu, huko mjini Damascus, Syria. Baada ya kusoma elimu ya sheria za Kiislamu na lugha ya Kiarabu, alianza kujifunza elimu ya Hadithi na kuwa gwiji katika uwanja huo. Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa na kiwapa kikubwa cha kutunga mashairi. Ameandika vitabu mbalimbali kuhusu maudhui tofauti.

Siku kama ya leo miaka 449 iliyopita, yaani tarehe 29 Machi 1573 Mfalme Charles wa Tisa wa Ufaransa alitoa amri ya kihistoria iliyojulikana kama amri ya uhuru, ambayo ilikuwa kwa maslahi ya Wakristo wa madhehebu ya Protestanti. Kwa mujibu wa amri hiyo, Waprotestanti wa Ufaransa ambao walijipatia ushindi kwenye vita vya nne dhidi ya Wakatoliki wa nchi hiyo, walikuwa huru kufanya sherehe, ibada na misa zao nchini humo. Vita vya nne vya kidini kati ya Wakatoliki na Waprotestanti vilianza tarehe 16 Julai mwaka 1572 na vilikuwa maarufu kwa jina la Vita vya La Rochelle.

Mfalme Charles wa Tisa

Miaka 346 iliyopita katika siku kama ya leo vita baina Poland na Ufalme wa Othmania vilifikia tamati kwa ushindi wa Ufalme huo na kutekwa sehemu ya ardhi ya Ukraine iliyokuwa chini ya utawala wa Poland.

Siku kama ya leo miaka 250 iliyopita, alifariki dunia Emmanuel Swedenborg, aliyekuwa mwanafikra mkubwa na msomi wa Sweden. Swedenborg alizaliwa mwaka 1688 na baada ya kubobea kwenye taaluma ya hesabati, aliweza kuwa mhandisi mahiri nchini humo. Swedenborg hakutosheka na elimu hiyo na badala yake akaongeza juhudi kubwa na kutokea kuwa mtaalamu pia kwenye elimu ya falsafa na irfani. Msingi wa falsafa ya msomi huyo ulikuwa kujitenga na dunia ya kimaada na kuingia zaidi katika ulimwengu wa kimaanawi. Kwa msingi huo Swedenborg aliamini kuwa kadiri mwanadamu anavyosafisha roho yake ndivyo anavyomuelewa na kumjua zaidi Mwenyezi Mungu. Mtaalamu huyo aliandika vitabu zaidi ya 50 kwa ajili ya kuweka wazi falsafa yake.

Emmanuel Swedenborg

Katika siku kama hii ya leo miaka 120 iliyopita sawa na tarehe 29 Machi mwaka 1902 alizaliwa mwandishi wa Kifaransa kwa jina la Marcel Ayme. Katika masomo yake ya awali Ayme alisomea uhandisi hata hivyo kutokana na kupatwa na maradhi aliachana na taaluma hiyo. Baadaye alijishughulisha na uandishi wa magazeti na taratibu akaanza kujihusisha na uandishi wa riwaya ambapo alitokea kuwa mashuhuri katika uwanja huo. Marcel Ayme ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwake ni "Beautiful Image", na "The Green Mare".

Marcel Ayme

Siku kama ya leo miaka 22 ilioyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani. Alizaliwa mwaka 1303 Hijria Shamsia katika familia ya kidini katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baada ya masomo ya mwanzo alielekea Karbala nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Alifanya utafiti mkubwa kuhusu dini na madhehebu mbalimbali na kuwa gwiji katika taaluma hiyo. Wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Rouhani alikuwa bega kwa bega na wananchi wa Iran katika mapambano yao dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah wakiongozwa na hayati Imam Khomeini. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Firqatus Salafiyyah", "Buhuth Ma'a Ahlisunna Wassalafiyyah" na "Firaq wa Madhahibu Islamiyyah".

Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani

 

Tags