Apr 04, 2022 02:43 UTC
  • Jumatatu tarehe 4 Aprili 2022

Leo ni Jumatatu tarehe Pili Ramadhani 1443 Hijria sawa na Aprtiili 4 mwaka 2022.

Katika siku kama ya leo miaka 1103 iliyopita alifariki dunia Abdur Rahman Zujaji Nahavandi aliyekuwa mwanafasihi, mtaalamu wa lugha na faqihi wa karne ya 4 Hijria katika mji wa Damascus. Alipata elimu kwa wanazuoni wakubwa na mashuhuri wa zama zake kama Ibn Dorayd na akafanikiwa kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa katika elimu hizo. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo wa Kiislamu ni "al Idhah".

Siku kama hii ya leo miaka 62 iliyopita Senegal inayopatikana magharibi mwa Afrika ilipata uhuru. Senegal ilikuwa chini ya ushawishi na ukoloni wa Wareno kuanzia karne ya 15 na kuanzia karne ya 17 pia Wafaransa nao walianza kuiba maliasili na utajiri wa nchi hiyo. Senegal iko katika pwani ya bahari ya Atlantic na inapakana na nchi za Mauritania, Mali, Guinea Bissau na Gambia.

Miaka 54 iliyopita katika siku kama ya leo Martin Luther King kiongozi aliyeongoza mapambano ya raia weusi wa Marekani aliuawa kwa kupigwa risasi na mtu mmoja au watu kadhaa wasiojulikana. Martin Luther alizaliwa mwaka 1929 katika mji wa Atlanta huko Marekani. Alipata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Boston na baadaye aliongoza harakati ya ukombozi ya Wamarekani weusi dhidi ya ubaguzi wa rangi waliokuwa wakifanyiwa raia weusi nchini Marekani. Katika kipindi hicho raia weusi wa Marekani waliasisi harakati ya nchi nzima ya kupinga ubaguzi wa rangi na vilevile katika kulalamikia sheria iliyokuwa ikiwatambua wazungu kama watu wa daraja ya juu huko Marekani. Kwa mujibu wa baadhi ya ushahidi ni kuwa shirika la ujasusi la Marekani CIA lilihusika katika mauaji hayo.

Martin Luther King

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita Zulfikar Ali Bhutto, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan alinyongwa. Bhutto ambaye alikuwa mwasisi wa Chama cha Wananchi (PPP) alikuwa Rais wa Pakistan mwaka 1971. Mwaka 1977 Jenerali Muhammad Dhiaul Haq alifanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Bhutto akimtuhumu kuwa amefanya mauaji na kuisaliti Pakistan. Hatimaye tarehe 4 Aprili mwaka 1979 Zulfiqar Ali Bhutto alinyongwa, licha ya viongozi wa baadhi ya nchi duniani kutaka asamehewe.

Zulfikar Ali Bhutto

 

Tags