May 13, 2022 02:22 UTC
  • Ijumaa tarehe 13 Mei 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 11 Shawwal 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 13 Mei mwaka 2022.

Tarehe 11 Shawwal miaka 1446 iliyopita Mtume Muhammad (S.A.W) alielekea katika mji wa Twaif karibu na Makka kwa lengo la kuwalingania Uislamu watu wa kabila la Thaqif. Safari hiyo ya Mtume mtukufu ilifanyika katika kipindi ambacho alikuwa ameondokewa na ami na mlezi wake kipenzi, Abu Twalib, jambo lililowafanya Maquraish wa Makka wazidishe maudhi na manyanyaso dhidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) na wafuasi wake. Hivyo ilitarajiwa kuwa, iwapo wakazi wa Twaif wangekubali Uislamu, mji huo ungeweza kuwa kituo na makazi salama kwa Waislamu waliokuwa wakidhulumiwa wa Makka. Hata hivyo viongozi wa kabila la Thaqif sio tu kwamba hawakumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja na risala ya Mtume Muhammad (S.A.W), bali pia baadhi ya watu wa kabila hilo walimfanyia maudhi, dhihaka na kumjeruhi Mtume Muhammad (saw).

Siku kama ya leo miaka 309 iliyopita alizaliwa mjini Paris, Alexis Cloude Clairaut mwanahesabati mashuhuri wa Ufaransa. Alikuwa na hamu kubwa na somo la hesabati ambapo akiwa na umri mdogo wa miaka 18 alifanikiwa kujiunga na Chuo cha Sayansi cha Ufaransa. Clairaut alipata umashuhuri mkubwa duniani kutokana na utafiti makini aliofanya katika nyanya tofauti za sayansi. Msomi huyo aliaga dunia mwaka 1765.

Alexis Cloude Clairaut

Katika siku kama ya leo miaka 115 iliyopita alizaliwa Bi Daphne du Maurier mwandishi wa riwaya, wasifu na thamthiliya wa Kiingereza. Maurier alizaliwa katika familia ya wanasanaa na iliyokuwa pia na wanafasihi. Ni kutokana na kukulia katika mazingira kama hayo, ndipo Bi Daphne du Maurier akafanikiwa kukuza kipaji chake katika uwanja wa uandishi. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni Scapegoat na Rebecca. Mwandishi huyo aliaga dunia mwaka 1889.

Daphne du Maurier

Na siku kama ya leo miaka 43 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsiya, mkataba wa kutoshtakiwa Wamarekani nchini Iran au Capitulation Accord ulifutwa nchini kufuatia mapambano yasiyosita ya wananchi Waislamu wa Iran, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Kiislamu na kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Kwa mujibu wa sheria za mkataba huo, raia wa Marekani aliyekuwa nchini Iran alikuwa na kinga kamili ya kisheria dhidi ya kufunguliwa mashtaka. Kwa kadiri kwamba hakuna taasisi au chombo chochote cha kisheria cha Iran kilichokuwa na mamlaka ya kumfungulia mashtaka na kumhukumu raia wa Marekani aliyekuweko Iran na kesi za raia hao wa Kimarekani zilipaswa kusikilizwa katika nchi yao.

 

Tags