May 15, 2022 02:18 UTC
  • Jumapili tarehe  15 Mei 2022

Leo ni Jumapili tarehe 13 Shawwal 1443 Hijria sawa tarehe 15 Mei mwaka 2022.

Tarehe 25 Ordibehesht ni siku ya kumbukumbu ya Abul-Qassim Firdowsi mwanafalsafa na malenga mashuhuri wa Iran. Inasemekana kuwa Firdowsi alizaliwa mwaka 319 au 320 Hijria Shamsia katika mji wa Tus, kaskazini mashariki mwa Iran. Miongoni mwa athari muhimu za malenga huyo wa Kiirani ni kitabu alichokipa jina la "Shahnameh". Kitabu hicho kilichosheheni historia ya jadi na utamaduni wa Iran kabla ya ujio wa Uislamu, kimefasiriwa kwa lugha mbalimbali.

Abul-Qassim Firdowsi

Tarehe 15 Mei miaka 246 iliyopita katika siku kama hii ya leo ilitengenezwa meli ya kwanza yenye kutumia mvuke. Meli inayotumia nishati ya mvuke ilitengenezwa miaka 70 baada ya kuvumbuliwa nishati ya mvuke na mhandisi wa Kifaransa Denis Papin. Utumiaji wa nishati ya mvuke katika meli ulileta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri wa baharini. 

Miaka 163 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Pierre Curie msomi na mwanafizikia wa Ufaransa. Kipaji cha masomo ya hesabati na fizikia alichokuwa nacho kilianza kuonekana tokea ujana wake, na hatimaye kuibuka kuwa mtafiti mkubwa katika nyanja hizo. Mwaka 1898 mwanafizikia huyo wa Kifaransa alifanikiwa kugundua Radium akisaidiana na mkewe Bi. Marie Pierre. Pierre Curie aliaga dunia mwaka 1906.

Pierre Curie

Siku kama ya leo tarehe 15 Mei 1919 mji wa Izmir moja ya miji ya kihistoria na muhimu nchini Uturuki, ulitekwa na wanajeshi wa Mustafa Kamal Pasha, mwasisi wa Jamhuri ya Uturuki, baada ya kujiri mapigano yaliyopelekea kuuawa watu wengi. Mji wa Izmir uko magharibi mwa Uturuki, na harakati ya Warepublican ya Uturuki ilianziwa katika mji huo wa kihistoria. 

Izmir

Siku kama ya leo miaka 120 alifariki dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Twaha, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 83. Familia ya msomi huyo mkubwa inatokana na moja ya maulama mashuhuri wa Kiislamu. Sheikh Twaha alizaliwa mjini Najaf, Iraq na kupata elimu kwa mwanazuoni mashuhuri wa zama hizo yaani Sheikh Murtadha Answari, Sheikh Twaha alitabahari katika elimu ya fiq’hi, usulu fiq’hi, hadithi na tafsiri ya Qur’ani Tukufu.

Miaka 105 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, Mirza Muhamamad Taqi Shirazi Kiongozi wa Mapinduzi ya Iraq alitoa fatuwa ya jihadi dhidi ya mkoloni Muingereza. Baada ya Uingereza kutangaza vita dhidi ya utawala wa Othmania mwaka 1914 na kukaliwa kwa mabavu mji wa Basra, maulamaa wakubwa wa Najaf walitoa hukumu ya kukabiliana na mkoloni huyo. Miaka ya baadaye ilishuhudia kujitokeza makundi yaliyokuwa yakipinga uwepo wa Uingereza nchini Iraq.

Mirza Muhamamad Taqi Shirazi

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Borujerdi Marjaa Taqlidi aliaga dunia. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Borujerd nchini Iran. Sayyid Hussein Tabatabai Borujerdi alibobea katika elimu za fiqhi,  hadithi na tafsiri ya Qur'ani. Kipindi fulani alielekea mjini Najaf Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu na kubakia huko kwa miaka minane. Alikuwa na wanafunzi wengi ambao baadaye wakuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri. Miongoni mwa wanafunzi hao ni Shahid Murtadha Mutahhari, Sayyid Muhammad Hussein Beheshti, Ayatullah Jaafar Sobhani, Ayatullah Fazel Lankarani, Ayatullah Nasser Makarem Shirazi na wengine wengi.

Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Borujerdi

Miaka 82 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 15 Mei mwaka 1940, jeshi la Ujerumani liliivamia na kuikalia kwa mabavu nchi ya Uholanzi baada ya shambulio kubwa lililodumu kwa siku 5 katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani walianza kuzishambulia nchi za Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxemburg huko magharibi mwa Ujerumani tarehe 10 Mei na kufanikiwa kuzidhibiti nchi zote hizo. Uholanzi ilijipatia uhuru wake mwaka 1945.

Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza Mei 15 kuwa Siku ya Kimataifa ya Familia. Uamuzi huo ulichukuliwa kutokana na umuhimu wa familia na asasi hii tukufu ambayo inahesabiwa kuwa msingi mkuu wa jamii na lengo ni kuilinda familia na madhara ya nje na ya ndani na kuifanya iwe na mchango na nafasi bora zaidi. Asasi ya familia ilikuweko tangu wakati wa kudhihiri mwanadamu na imeendelea kuwa nguzo kuu ya jamii.  Mke na mume na watoto na wakati mwingine bibi na babu ni watu wanaounda familia hii. Familia ni mahala tulivu kwa wenza, sehemu ya kulea na kukuza watoto na ni mazingira yenye amani kwa ajili ya wanafamilia kuwa na mawasiliano salama.

 

Tags