May 16, 2022 02:27 UTC
  • Jumatatu tarehe 16 Mei mwaka 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 14 Shawwal 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 16 Mei mwaka 2022.

Katika siku kama ya leo miaka 870 iliyopita alifariki dunia Qutbuddin Rawandi, faqihi wa karne ya sita Hijria ambaye pia alikuwa mtaalamu wa Hadithi na teolojia ya Kiislamu. Kwa miaka mingi alipata elimu na maarifa kwa wasomi wakubwa wa zama zake na kubobea katika taaluma za fiq'hi, Hadithi na tafsiri ya Qur'ani. Msomi huyu mkubwa wa Kiislamu ameandika karibu vitabu 80 vikiwemo vya "Tafsirul Qur'an", "Risaalatul-Fuqahaa", "Tahafutul Falasifa", "Aayaatul-Ahkaam" na "Asbaabun-Nuzul."

Qutbuddin Rawandi

Siku kama ya leo miaka 520 iliyopita, ardhi ya Honduras inayopatikana leo huko Amerika Kusini iliunganishwa na makoloni ya Muhispania. Kabla ya hapo Honduras ilikuwa kituo cha utamaduni wa kaumu ya Maya. Hata hivyo baada ya Honduras kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Uhispania, kabila hilo liliangamizwa na kupotea. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia na kutokana na kuvurugika hali ya ndani ya Uhispania, Honduras kama ilivyokuwa kwa makoloni mengine, ilitumia fursa hiyo kuweza kujipatia uhuru wake. 

Tarehe 16 Mei miaka 234 iliyopita alizaliwa mjini Hamburg Friedrich Ruckert, malenga na mtaalamu wa masuala ya Mashariki wa Ujerumani. Alifanya juhudi ya kutafsiri mashairi ya lugha za Kifarsi, Kiarabu na Kichina kwa lugha ya Kijerumani. Kadhalika alijifunza fasihi na tamaduni za Mashariki mwa dunia na kuzitumia katika utunzi wa mashairi. Friedrich Ruckert  alikuwa mmoja wa malenga wa Kijerumani waliofasiri diwani ya mashairi ya Hafez (malenga mkubwa wa Kiirani) katika lugha ya Kijerumani. Miongoni mwa athari ya Friedrich Ruckert ni kitabu cha 'Spring of Love.'

Friedrich Ruckert

Katika siku kama hii ya leo miaka  106 iliyopita Ufaransa na Uingereza ziligawana milki zao katika Mashariki ya Kati na maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na utawala wa Dola ya Othmaniyya chini ya mkataba wa Sykes-Picot, ambao ulikuwa umetiwa saini wiki moja kabla. Kutiwa saini kwa mkataba wa kikoloni wa Sykes-Picot Agreement baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia kulitayarisha mazingira ya kisiasa ya kugawanywa ardhi ya Mashariki ya Kati na kusambaratisha dola la Othmaniyya. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi za Uingereza na Ufaransa ziligawana udhibiti wa nchi za Kiarabu ambazo zilizokuwa chini ya dola ya Othmaniyya. Kwa utaratibu huo, Iraq na Jordan ziliwekwa chini ya udhibiti wa Uingereza, Syria na Lebanon zikawa chini ya mamlaka ya Ufaransa. Maeneo ya kaskazini mwa Iraq na mashariki mwa Uturuki pia yalikabidhiwa kwa Urusi. Miongoni mwa matokeo mabaya sana ya makubaliano Sykes-Picot ni kuundwa kwa utawala wa kibaguzi wa Israel katika ardhi ya Palestina, jambo ambalo lilifanyika takriban miongo mitatu baada ya kutiwa saini makubaliano hayo.

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti lilianza kuondoka nchini Afghanistan. Baada ya Nur Muhammad Taraki kupinduliwa, serikali ya kwanza ya kikomunsti iliyokuwa ikipata himaya ya moja kwa moja ya Urusi ya zamani ilianzishwa nchini Afghanistan. Utawala wa Taraki uliondolewa madarakani mwanzoni mwa mwaka 1979 kupitia mapinduzi mengine yaliyoongozwa na Hafidhullah Amin mmoja wa watu wake wa karibu. Lakini Warusi hawakumpenda Hafidhullah ambaye alikuwa akitaka kujikurubisha kwa Marekani na kuanzisha uhusiano kati ya Afghanistan na Mashariki na vilevile Magharibi na hivyo wakaipindua serikali yake.

eshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti

Na siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, Jenerali Mobutu Sese Seko rais na dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zaire ya zamani, aliikimbia nchi hiyo baada ya vikosi vya majeshi ya waasi vilivyokuwa vikiongozwa na Laurent Kabila kukaribia mji wa Kinshasa. Mobutu alichukua madaraka ya nchi hiyo mnamo mwaka 1965 kupitia mapinduzi ya kijeshi na kisha kutawala kwa muda wa miaka 32. Licha ya kiongozi huyo kuwa dikteta asiye na huruma, lakini alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi hasa Marekani na Ufaransa. Kutokana na Congo DR kuwa katika eneo nyeti na muhimu kijiografia katikati mwa bara la Afrika na kuwa na utajiri mkubwa wa madini ikiwemo almasi, imekuwa ikizingatiwa sana na kumezewa mate na nchi za Magharibi. Siku moja baada ya Mobutu kuikimbia nchi hiyo, vikosi vya waasi viliuteka mji wa Kinshasa na kiongozi wao yaani Laurent Kabila, akashika hatamu za uongozi wa nchi. 

Jenerali Mobutu Sese Seko

 

Tags