May 19, 2022 02:11 UTC
  • Alkhamisi, Mei 19, 2022

Leo ni Alkhamisi wezi 17 Mfunguo Mosi Shawwal 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 19 Mei mwaka 2022 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka Miaka 501 iliyopita, majeshi ya utawala wa kifalme wa Othmania yaliuteka mji muhimu wa Belgrade, uliokuwa mji mkuu wa Yugoslavia ya zamani. Mwishoni mwa karne ya 14 Miladia Utawala wa Othmania ulianza kusonga mbele katika eneo la Balkan na kuweza kulitawala karibu eneo lote hilo. Miaka 20 baadaye yaani mwaka 1541 utawala huo ulifanikiwa pia kuyadhibiti maeneo ya Hungary.

Siku kama ya leo miaka 260 iliyopita, alizaliwa katika familia masikini Johann Gottlieb Fichte mwanafalsafa wa Kijerumani. Johann alikuwa mmoja wa waasisi wakuu wa harakati ya kifalsafa iliyojulikana kama "German Idealism" ambayo ilitokana na maandiko ya kinadharia na kimaadili ya Immanuel Kant. Johann Gottlieb Fitche aliathiriwa sana kinadharia na mwanafalsafa mwenzake huyo na kumkabidhi moja ya athari zake muhimu katika taaluma ya falsafa. Johann Fitche ameandika vitabu vingi kama "Foundations of Nature Right, Mustakabali wa Binadamu na makala ya The Way Towards the Blessed Life.

Johann Gottlieb Fitche

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, alizaliwa Malcolm X, kiongozi wa harakati za kupigania uhuru ya Wamarekani wenye asili ya Afrika. Malcolm X alizaliwa katika familia masikini na akiwa na umri wa miaka minne, alishuhudia nyumba ya wazazi wake ikishambuliwa na kuteketezwa kwa moto na kundi la kibaguzi la Ku Klux Klan. Baadaye alijiunga na shule, hata hivyo hakuweza kukamilisha masomo yake kutokana na umasikini na aliacha shule akiwa na umri wa miaka 15; hivyo akalazimika kufanya kazi katika mgahawa mmoja na kutumbukia kwenye magenge ya utumiaji wa dawa za kulevya na unyang’anyi. Alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela akiwa na umri wa miaka 21. Akiwa jela alifahamiana na wafungwa wengi wenye asili ya Kiafrika waliotokana na familia za Kiislamu kama ambavyo pia alikuwa na mahusiano na Elijah Muhammad, kiongozi wa harakati ya siri ya Wamarekani weusi. Uhusiano wake na kiongozi huyo uliendelea hata baada ya Malcolm X kutoka jela. Baada ya hapo alianza kusoma na kufanya utafiti mkubwa kuhusiana na dini ya Uislamu na alifanikiwa kujenga misikiti miwili katika mji wa Detroit, Philadelphia nchini Marekani. Malcom X alipigwa risasi na kuuawa tarehe 21 Februari mwaka 1965 katika mji wa New York baada ya kushadidi harakati zake za kupigania haki za Waislamu na Wamarekani weusi. Mauaji ya mwanaharakati huyo Mwislamu wa Marekani, kama yalivyo mauaji mengi ya kisiasa ya Marekani, bado yangali yanagubikwa na wingu kubwa. Hata hivyo ushahidi unaonyesha kuwa, Malcom X aliuawa na maajenti wa shirika la usalama wa ndani ya Marekani FBI likishirikana na Shirika la Ujasusi la nchi hiyo, CIA.

Malcolm X

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, Thomas Edward Lawrence mwanasiasa na afisa wa ujasusi wa Uingereza alifariki dunia katika ajali ya gari. Lawrence alizaliwa mwaka 1888. Katika kipindi cha miaka ya kati ya 1910 na 1914, mwanasiasa huyo wa Uingereza alifanya kazi katika nchi za Iraq, Syria na Palestina akiwa mjumbe wa kamati ya masuala ya akiolojia (elimu mambo ya kale). Vilevile alikuwa mfanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza na mwaka 1916 aliteuliwa kuwa mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Uingereza nchini Misri. Thomas Edward Lawrence alikuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa njama ya Uingereza na Ufaransa ya kuzigawa nchi za Kiarabu na utawala wa Othmania (Ottoman Empire) na alichangia pakubwa kuwaweka madarakani wafalme Faisal huko Syria, Abdallah nchini Jordan na Mfalme Abdulaziz huko Saudi Arabia. Kwa sababu hiyo alijulikana kwa jina la Lawrence wa Uarabuni ( Lawrence of Arabia).

Thomas Edward Lawrence

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita yaani tarehe 19 Mei mwaka 1936, chombo cha rada kilitengenezwa na Sir Robert Watson-Watt, mtaalamu na mvumbuzi wa Kiingereza. Chombo hicho ambacho ni wenzo muhimu utumiwao na marubani kuonyesha vitu kwenye skrini au kugundulia na kutambulia mambo katika operesheni za kijeshi na zisizokuwa za kijeshi, kwa mara ya kwanza kiliwekwa katika viwanja vya ndege nchini Uingereza. Wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, rada ilihesabiwa kuwa wenzo muhimu wa kutoa tahadhari. Hii leo chombo cha rada kinatumiwa katika nyanja mbalimbali hasa katika safari za ndege, opresheni za kijeshi na kadhalika.

Sir Robert Watson-Watt

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, watu 90 wa familia ya Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim walitiwa mbaroni huko Iraq, na sita miongoni mwao wakanyongwa sikua kadhaa baadaye. Jinai hiyo ilikuwa ni mwendelezo wa utawa wa dikteta Saddam Hussein wa kukandamiza aina yoyote ile ya harakati ya kukabiliana na utawala wake. Muda mchache baada ya tukio hilo, watu wengine 10 wa familia hiyo ya Ayatullah Muhsin Hakim waliuawa na utawala wa Saddam. Ayatullahil Udhma Muhsin al Hakim alikuwa mmoja kati ya viongozi wakuu wa kidini nchini Iraq. Alifariki dunia mwaka 1348 Hijria Shamsia.

Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim

Na miaka 27 iliyopita katika siku kama ya leo, Allama Muhammad Taqi Shushtari aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 93 baada ya kuishi maisha yaliyojaa harakati ya kueneza elimu na maarifa. Muhammad Taqi Shushtari alizaliwa katika familia ya elimu na wanamapambano na alifanikiwa kukwea haraka daraja za kielimu. Aliondoka nchini Iran na kuelekea Iraq akiwa na umri wa miaka 32 akipinga marufuku ya vazi la hijabu iliyokuwa imetangazwa na Reza Shah mfalme wa wakati huo wa Iran. Miongoni mwa vitabu mashuhurti vya masomi huyo mkubwa wa Kiislamu ni Qamusur Rijal chenye juzuu 14, Nahjul Sabaghah, al Naj'a na Qadhaa Amirul Muuminin.

Allama Muhammad Taqi Shushtari