May 21, 2022 03:16 UTC
  • Jumamosi, 21, Mei 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 19 Mfunguo Mosi Shawwal 1443 Hijria mwafaka na tarehe 21 Mei 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 2238 iliyopita, yaani tarehe 21 Mei mwaka 216 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (as), jeshi la mtawala wa Carthage chini ya uongozi wa Hannibal, lilishindwa vibaya huko kaskazini mwa Italia. Hivyo vilikuwa vita vya pili baina ya utawala wa Carthage na Roma kwa anwani ya vita vya 'Punic.' Hannibal alishiriki vita hivyo kwa kutumia tembo na wapandaji tembo mahiri kabla ya kushindwa vibaya. ***

Hannibal,

 

Siku kama ya leo mmiaka 1009 yaani tarehe 19 Shawwal 434 iliyopita alizaliwa Abu Zakaria Yahya bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Mandeh ambaye alikuwa mwanahadithi, faqihi na mwanahistoria wa Kiirani. Alikuwa wa mwisho katika kizazi cha Ibn Mandeh na baada ya kupata elimu za zama zake alianza kufunza na kuandika vitabu. Mwanahistoria huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha Maisha ya Tabarani. ***

Abu Zakaria Yahya bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Mandeh

 

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, alizaliwa Andrei Sakharov, mwanafizikia mashuhuri wa Russia. Sakharov alihitimu taaluma ya fizikia katika chuo kikuu cha Moscow mwaka 1941 na kisha akaanza kufanya utafiti wa kina kuhusiana na nishati ya nyuklia. Alikuwa na nafsi muhimu katika utengenezaji wa bomu la hydrogen nchini Russia. Sakharov pia alikuwa muungaji mkono mkubwa wa harakati za kutokomeza silaha za nyuklia na ndio maana akatunukiwa zawadi ya amani ya Nobel hapo mwaka 1975. Miaka mitano baadaye Sakharov alibaidishiwa katika mji wa Gorky, mashariki mwa Moscow kutokana na upinzani wake dhidi ya siasa za utawala wa kikomonisti wa Russia. Hata hivyo ubaidishaji huo ulifikia kikomo mwaka 1986 baada ya Mikhail Sergeyevich Gorbachev kutwaa madaraka. Mwanzoni mwa mwaka 1989 Sakharov alichaguliwa kuwa mbunge katika bunge la Russia lakini akaaga dunia baadaye mwezi Disemba mwaka huohuo. ***

Andrei Sakharov

 

Katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, Rajiv Gandhi, Waziri Mkuu wa zamani wa India, aliuawa kigaidi. Rajiv Gandhi alikuwa mwanawe Indira Gandhi Waziri Mkuu wa zamani pia wa nchi hiyo. Alizaliwa tarehe 20 Agosti 1944 mjini Bombay na kulelewa katika nyumba ya babu yake Jawaharlal Nehru, Waziri Mkuu wa kwanza wa India. Rajiv Gandhi aliingia katika ulingo wa siasa baada ya kuaga dunia mdogo wake ambaye alikuwa akitayarishwa kumrithi kisiasa mama yake Indira Gandhi. Alichukua hatamu za kuiongoza India baada ya kuuliwa kigaidi mama yake hapo tarehe 31 Oktoba 1989. Rajiv Gandhi alikuwa na nia ya kushiriki katika uchaguzi mkuu wa bunge lakini aliuawa na magaidi tarehe 21 Mei 1991 akiwa na umri wa miaka 47 alipokuwa akifanya kampeni za uchaguzi huo huko kusini mwa India. ***

Rajiv Gandhi, Waziri Mkuu wa zamani wa India,

 

Miaka 24 iliyopita na katika siku kama ya leo, Jenerali Muhammad Suharto wa Indonesia alilazimika kujiuzulu baada ya kuitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa miaka 33. Aliingia madarakani mwaka 1965 baada ya kumpindua Ahmad Sukarno, mwanzilishi wa Indonesia huru ambaye alikuwa amechaguliwa na wananchi wa nchi hiyo. Uhuru wa kisiasa ulibanwa sana katika kipindi cha utawala wa Suharto. Hata hivyo nchi hiyo ilishuhudia maendeleo makubwa ya kiuchumi katika utawala wake katika miongo ya 80 na 90. Pamoja na hayo lakini mgogoro wa kiuchumi uliozikumba nchi za Asia Mashariki katika mwaka wa 1997 ulianzisha malalamiko na maandamano makubwa ya wanafunzi wa Indonesia na taratibu yakachukua mkondo wa kisiasa uliopelekea Suharto kuondolewa madarakani. Ufisadi wa kiuchumi uliofanywa na Suharto pamoja na familia yake ulichochea zaidi kuanguka kwa utawala wake, ambako kulitanguliwa na kujiuzulu kwake madarakani. ***

Jenerali MNuhammad Suharto

 

Miaka 27 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sheikh Muhammad Ghazali mwanazuoni na mwanamageuzi mkubwa wa Misri. Alizaliwa mwaka 1917 huko nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 10 tu, tayari Muhammad Ghazali alikuwa amehifadhi Qur'ani Tukufu yote. Muhammad Ghazali alihitimu Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 24. Fikra zake zilijengeka juu ya msingi wa mageuzi ya maarifa ya kidini, kukurubisha baina ya madhehebu za Kiislamu na kupinga fikra za kikaumu. Muhammad Ghazali aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 79 kwa mshtuko wa moyo na kuuzikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina. ***

Sheikh Muhammad Ghazali

 

Na siku kama ya leo miaka 16 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Mei 2006, nchi ya Montenegro ilijipatia uhuru wake kutoka Jamhuri ya Serbia baada ya kufanyika kura ya maoni. Kuanzia karne ya 16 hadi 19, Montenegro ilikuwa chini ya himaya ya utawala wa Othmaniya. Amma baada ya kusambaratika utawala wa Yugoslavia ya zamani, nchi hiyo ikaanza harakati za kujipatia uhuru wake, na ulipoanza mgogoro wa Kosovo mwishoni mwa muongo wa 1990, Montenegro ilikata uhusiano wake wa kisiasa na kiuchumi na Serbia na mgogoro wa pande hizo mbili ukazidi kupamba moto. ***

Montenegro