May 23, 2022 08:36 UTC
  • Jumatatu tarehe 23 Mei 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 21 Shawwal 1443 Hijria sawa na tarehe 23 Mei 2022.

Miaka 1351 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, ardhi ya Andalusia huko Uhispania ya leo ilidhibitiwa na jeshi la Kiislamu lililoongozwa na Tariq bin Ziyad. Tariq ambaye alikuwa na wapiganaji karibu ya elfu 12, alivuka kwa boti mlango bahari ulioko kati ya Morocco na Uhispania ambao umepewa jina lake Tariq bin Ziad au "Gibraltar". Tariq bin Ziyad aliamuru kochomwa moto boti zote zilizotumiwa na wapiganaji wake kuvukia lango bahari na Gibralta ili kuwahamasisha zaidi kupigana na maadui. Katika kipindi cha karne 8 za utawala wao huko Andalusia, Waislamu walianzisha vituo mbalimbali vya utamaduni na taasisi za kiuchumi na kwa kipindi kirefu ardhi hiyo ilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu wa Kiislamu barani Ulaya.

Tariq bin Ziyad

Miaka 1089 iliyopita mwafaka na leo, alifariki dunia Ibn Habban, mtaalamu wa hadithi, elimu ya fiq'hi na mwanahistoria mashuhuri wa karne ya 14 Hijiria. Alipata elimu ya msingi kwa walimu mashuhuri wa zama zake na kisha akaelekea Neishabur kaskazini mwa mashariki mwa Iran, ambao katika kipindi hicho ulikuwa ni moja ya vituo muhimu vya kielimu. Ibn Habban anahesabika kuwa mtu mwenye nadharia muhimu katika elimu ya hadithi. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha"At-Thuqat" na Rawdhatul-Uqalaai wa Nazahatul-fudhalaai."

Katika siku kama ya leo miaka 404 iliyopita, sawa na 23 Mei 1618, kulianza vita vya kidini barani Ulaya vilivyoendelea kwa muda wa miaka 30. Katika vita hivyo, nchi za Ufaransa, Sweden na Denmark zilikuwa zikiwaunga mkono Waprotestanti, huku Uhispania na Ufalme wa Rome zikiwaunga mkono Wakatoliki. Vita hivyo vilifikia tamati mwaka 1648 baada ya kutiwa saini Mkataba wa Westaphalia.

Miaka 116 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Henrik Ibsen mwandishi wa tamthiliya wa nchini Norway. Alizaliwa mwaka 1828 na shauku na mapenzi ya Ibsen ya kuwa mwandishi wa tamthiliya ndiyo yaliyomsukuma kwenye taaluma hiyo. Mwandishi huyo wa Kinorway ameandika drama na tamthiliya nyingi. Moja kati ya tamthmliya zake mashuhuri ni ile iitwayo, An Enemy of the People yaani Adui wa Watu. 

Henrik Ibsen

Miaka 107 iliyopita katika siku kama ya leo, Italia ilijiingiza katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Kuingia Italia katika Vita vya Kwanza vya Dunia kulianza wakati nchi hiyo ilipoivamia Austria bila ya sababu yoyote isipokuwa tu kwa tamaa ya kujinufaisha kisiasa na kupanua utawala wake. Muda mchache baadaye, serikali ya Italia ilitangaza vita dhidi ya ufalme wa Othmania na hivyo kuufanya moto wa vita uwake kwa ukali zaidi. Hata hivyo, licha ya kupata ushindi kundi la nchi Waitifaki, Italia ikiwa moja yao, lakini nchi hiyo haikufaidika kivyovyote na vita hivyo. Matunda pekee iliyopata ni kuwaulisha raia wa Italia baada ya kuwaingia Waitaliano milioni tano na nusu katika vita hivyo. Kwa maneno mengine ni kuwa maamuzi na siasa za Italia katika Vita vya Kwanza vya Dunia zilifeli, kwani haikupata matunda yoyote ya maana kwa kujiingiza kwake kwenye vita hivyo. 

Vita vya Kwanza vya Dunia

Katika siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, alijiua Heinrich Himmler Mkuu wa zamani wa Shirika la Kijasusi na Usalama la Ujerumani ya Kinazi. Himmler alizaliwa mwaka 1900 na alipofikisha umri wa miaka 34 aliweza kupanda cheo na kuwa mkuu wa shirika hilo la kijasusi na usalama la Ujerumani (Gestapo). Heinrich Himmler anahesabiwa kuwa mmoja kati ya viongozi wauaji na wamwagaji damu ambaye aliongoza operesheni kadhaa za mateso na kuuwa watu nchini humo. Himmler alitiwa mbaroni baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya Nurenberg nchini Ujerumani, lakini kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo aliamua kujiua mwenyewe baada ya kunywa sumu.

Heinrich Himmler

Siku ya leo miaka 31 iliyopita pili Khordadi mwaka 1370 Hijria Shamsia Waislamu duniani walilalamikia vikali hatua ya utawala wa chama cha Baath cha Iraq ambao ulivunjia heshima maeneo matakatifu ya Kiislamu nchini humo. Baada ya wananchi Waislamu wa Iraq kuanzisha muamko kupinga jinai nyingi  za utawala wa Baath, Saddam Hussein dikteta wa wakati huo Iraq alitoa amri ya kuuawa bila huruma wananchi na kuhujumiwa maeneo matakatifu ya Kiislamu nchini humo. Kitendo hicho cha utawala wa baath kiliibua hasira za Waislamu hasa Waislamu wa madhehebu ya Shia ambao walifanya maandamano kupinga jinai hizo. Jinai hizo zilitendeka ukiwa umesalia muda mfupo kabla ya wananchi wa Iraq kupata ushindi dhidi ya Saddam. Katika kipindi hicho, Marekani na waitifaki wake walimsaidia Saddam kuua na kuwakandamiza wananchi. Hata baada ya wananchi kutafuta hifadhi katika maeneo matakatifu, Jeshi la Saddam liliwahujumu wakiwa katika maeneo hayo.Baada ya kupinduliwa utawala wa Saddam, kulipatikana makaburi mengi ya umati na hivyo kikabainika kiwango cha jinai za Saddam dhidi ya wananchi.

Shambulizi la utawala wa Baath dhidi ya maeneo matakatifu, Iraq

Miaka 11 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 2 Khordad mwaka 1390 Hijria Shamsia, Nasser Hijazi mchezaji na kocha mashuhuri wa soka nchini Iran aliaga dunia. Nasser Hijazi alizaliwa mwaka 1949 sawa na mwaka 1328 Hijria Shamsia mjini Tehran. Aliwahi kuwa golkipa wa Klabu ya Esteghlal na Timu ya Taifa ya Iran. Alijiunga na timu ya taifa ya Iran katika Kombe la Dunia la FIFA mwaka 1978 na alikuwa kipa nambari moja wa timu hiyo. Hijazi aliendelea kuwa kipa wa timu ya taifa ya Iran hadi mwaka 1980. Mnamo mwaka 1986 akiwa na umri wa miaka 36 alistaafu kama mchezaji na akaelekea nchini Bangladesh na kuwa kocha wa Klabu ya Mohammedan. Akiwa kocha wa Mohammedan timu hiyo iliweza kufanikiwa na kuwa kati ya vilabu bora nane vya bara Asia. Aliporejea Iran Hijazi alikuwa kocha mwenye mafanikio wa timu kama vile Bank Tejerat na Shahredari Kerman, Mashine Sazi Tarbiz, Zobahan na Sepahan Isfahan. Hali kadhalika alikuwa kocha wa timu za Nasaji Mazandaran, Esteghlal Tehran, Esteghlal Rasht na Esteghlal Ahvaz. Nasser Hijazi anatazamwa kama mmoja kati ya wachezaji mashuhuri na waliopendwa zaidi nchini Iran. Mwaka 1999 Shirikisho la Soka Asia lilimtambua kama kipa wa pili bora wa karne barani Asia. Mwaka 1988 aliugua na kulazwa hospitalini na hatimaye tarehe Pili Khordad akaaga dunia.

Nasser Hijazi