May 24, 2022 02:11 UTC
  • Jumanne tarehe 24 Mei 2022

Leo ni Jumanne tarehe 22 Shawwal 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 24 Mei 2022.

Katika siku kama ya leo miaka 292 iliyopita aliaga dunia Muhammad Hussein Khatunabadi aliyekuwa alimu na msomi mkubwa wa Kiirani. Alikuwa hodari katika fiqhi, fasihi na elimu ya Hadithi na alikusanya na kuandika Hadithi nyingi za Mtume (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo wa Kiislamu ni al Alwah al Samawiyyah. 

Ayatullah Muhammad Hussein Khatunabadi

Siku kama ya leo miaka 200 iliyopita, nchi ya Ecuador ilipata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania. Ecuador ni moja ya nchi za Amerika ya Kusini ambayo kupitia uongozi wa Simón Bolívar mwanamapinduzi maarufu wa Venezuela, ilifanikiwa kuwa huru na kujiunga na umoja wa Colombia Kubwa. Hata hivyo umoja huo ulisambaratika haraka na kufanya nchi wanachama wa umoja huo ikiwemo Ecuador kuasisi mfumo wa jamhuri.

Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, mji wa Khorramshahr wa Iran ulikombolewa na wapiganaji wa Kiislamu na ukaondoka katika uvamizi wa majeshi vamizi ya Iraq. Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane. Uvamizi dhidi ya mji huo ulijiri mwanzoni mwa vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran na Iraq. Siku hii inajulikana katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuwa, "Siku ya Muqawama na Ushindi". 

Katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, nchi ya Eritrea iliyoko kaskazini mashariki mwa bara la Afrika ilijitenga na Ethiopia na kujitangazia uhuru. Mwaka 1936 Miladia Italia iliikalia kwa mabavu Eritrea iliyokuwa ikihesabiwa katika zama hizo kuwa sehemu ya ardhi ya Ethiopia. Mwaka 1953, Italia iliirejeshea Ethiopia ardhi hiyo. Hata hivyo wananchi wengi wa nchi hiyo waliokuwa wakitaka uhuru walianzisha harakati za ukombozi dhidi ya serikali ya Ethiopia. Mwaka 1991, Harakati ya Ukombozi wa Eritrea ikisaidiana na wanamapinduzi wa Ethiopia walihitimisha utawala wa kidikteta wa Mfalme Mengistu Haile Mariam, na wakakubaliana kuanishwa mustakbali wa Eritrea mwaka 1993 kupitia kura ya maoni. Washiriki wengi wa kura hiyo ya maoni walipiga kura ya kutaka kujitawala Eritrea.

Bendera ya Eritrea

Miaka 21 iliyopita katika siku kama ya leo, vikosi vya utawala dhalimu wa Israel vililazimika kuondoka kwa madhila katika eneo la kusini mwa Lebanon baada ya kulikalia kwa mabavu eneo hilo kwa muda wa miaka 22. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na mapambano ya wananchi wa kusini mwa Lebanon. Mwaka 1982, majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yalishambulia Lebanon na kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut. Hata hivyo kutokana na wananchi hao kuathirika na mafunzo ya kutokubali dhulma hasa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, nchini Lebanon kulianzishwa harakati za mapambano ya Kiislamu dhidi ya majeshi vamizi ya utawala haramu wa Israel. Chama cha Hizbullah kilikuwa na nafasi muhimu na ya kuzingatiwa mno katika kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon toka katika makucha ya utawala dhalimu wa Israel.