May 25, 2022 03:12 UTC
  • Jumatano tarehe 25 Mei 2022

Leo ni Jumatano tarehe 23 Shawwal 1443 Hijria sawa na tarehe 25 Mei mwaka 2022.

Siku kama ya leo, miaka 662 iliyopita, yaani tarehe 25 Mei mwaka 1360 kundi la mabaharia wa Kifraransa liligundua Ghuba ya Guinea. Ghuba ya Guinea iko magharaibi mwa bara la Afrika katika bahari ya Atlantiki. Baada ya muda kupita tangu kugunduliwa Ghuba ya Guinea, ushawishi wa Ufaransa ndani ya bara hilo ulianza, na taratibu ikaanza kuidhibiti ardhi iliyokuja kujulikana baadaye kama Guinea. Nchi ya Guinea iliendesha harakati za mapambano ya miaka mingi mpaka ikafanikiwa kupata uhuru wake mwaka 1958. Guinea ina eneo lenye ukubwa wa kilomitamraba zaidi 245,000 na imepakana na nchi za Senegal, Guinea Bissau, Mali, Ivory Coast, Liberia na Sierra Leone.

Katika siku kama ya leo miaka 331 iliyopita alifariki dunia Sayyid Neematulllah Jazairi aliyekuwa faqihi na mpokezi mkubwa wa hadithi wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 62. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, Hadithi, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu na alistahamili mashaka mengi katika njia ya kulingania sheria za dini ya Kiislamu. Sayyid Neematullah Jazairi ameandika vitabu kadhaa vya thamani kama Madinatul Hadith, Qiswasul Anbiyaa na Hidayatul Muuminin.

Sayyid Neematulllah Jazairi

Miaka 130 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 25 Mei mwaka 1892 alizaliwa Josip Broz Tito, kiongozi wa zamani wa Yugoslavia, huko katika eneo la Hrvatsko Zagorje, kaskazini mwa Zagreb, mji mkuu wa Croatia. Mnamo mwaka 1915, wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Tito alikamatwa katika medani ya vita dhidi ya Urusi; na baada ya kuachiwa huru aliungana na Wakomunisti kupamaba na utawala wa Tsar. Tito aliasisi harakati ya ukombozi wa taifa baada ya Ujerumani  kuishambulia Yugoslavia wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Mnamo mwaka 1943 alipewa hadhi ya Jemadari (Marshal), mwaka 1953 akawa Mkuu wa Baraza la Utendaji wa Shirikisho na Kamanda Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Yugoslavia na hatimaye mwaka 1974, Josip Tito akatangazwa kuwa rais wa milele wa nchi hiyo. Katika sera za nje, Tito aliilinda Yugosalvia na ushawishi wa Shirikisho la Kisovieti la Urusi (USSR), na kwa sababu hiyo akajitoa kwenye kambi ya nchi za Kikomunisti duniani. Jemadari Josip Tito aliaga dunia tarehe 4 Mei mwaka 1980 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Josip Broz Tito

Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 25 Mei mwaka 1963, Hati ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) ilisainiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 32 za bara hilo. Marais Gamal Abdel Nasser wa Misri, Kwame Nkrumah wa Ghana na Ahmed Sekou Toure wa Guinea walikuwa miongoni mwa waasisi wa jumuiya hiyo. Jumuiya ya OAU ilielekeza jitihada zake katika kuleta umoja kati ya nchi za Afrika, kutatua hitilafu kati ya nchi hizo, kutetea haki ya kujitawala ya nchi wanachama na ukombozi wa nchi nyingine za Kiafrika zilizokuwa zingali zinakoloniwa. Mnamo mwezi Julai mwaka 2002, viongozi wa nchi wanachama wa OAU walifanya kikao nchini Afrika Kusini na kuamua kubadilisha jina la jumuiya hiyo kutoka Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) na kuwa Umoja wa Afrika (AU) sambamba na kuanzisha taasisi kadhaa kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya umoja huo na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama. Hivi sasa Umoja wa Afrika una nchi 54 wanachama. Makao Makuu ya umoja huo yako Addis Ababa, Ethiopia na kikao cha viongozi wa nchi wanachama hufanyika kila mwaka katika moja ya nchi hizo.

Na tarehe 4 Khordad kwa mujibu wa kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya Hijria Shamsia imepewa jina la Siku ya Kusimama Kidete Dezful, ambao ni moja ya miji ya kusini mwa Iran. Sababu ya siku hii kupewa jina hilo ni muqawama na ungangari wa watu wa Dezful kukabiliana na hujuma na mashambulio ya makombora ya utawala wa Kibaathi wa Iraq wakati wa vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Wakati vilipoanza vita hivyo vya Kujihami Kutakatifu, mji wa Dezful ulishambuliwa kwa makombora zaidi ya 200 na kwa risasi zaidi ya elfu ishirini mpaka ukajulikana kwa jina la mji wa makombora. Pamoja na yote hayo wananchi katika mji wa Dezful waliendelea kuonyesha muqawama na uhimilivu kiasi kwamba hata katika mazingira hayo Sala ya Ijumaa iliendelea kusaliwa kila wiki kwa kuhudhuriwa na wananchi na wapiganaji waliokuwa kwenye medani za vita.

 

Tags