Jun 02, 2022 11:40 UTC
  • Alkhamisi, 02 Juni, 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe Pili Mfunguo Pili Dhul Qaadah 1443 Hijria, sawa na tarehe Pili Juni 2022 Miladia

Miaka 1132 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe Pili Dhul Qaadah mwaka 311 Hijria aliaga dunia Abu Bakr Muhammad ibn Ishaq ibn Khuzaymah, Faqihi na Alimu mashuhuri wa Hadithi wa karne ya nne Hijria. Ibn Khuzaymah alizaliwa mwaka 223 Hijria katika mji wa Neyshabur nchini Iran, na tangu ujana wake alisafiri kwenda miji mbambali kwa ajili ya kusoma elimu tofauti za dini. Baadaye, alimu huyo aliandika vitabu kadhaa ambavyo vimesalia hadi leo. Athari muhimu zaidi ya Ibn Khuzaymah ni kitabu kiitwacho "Kitabu-Tawhid wa Ithbat S'ifati-Rab Azza Wa Jalla", kinachozungumzia itikadi za dini tukufu ya Uislamu. Ndani ya kitabu hicho amefafanua kwa kina itikadi na rai zake kuhusu tauhidi na upekee wa Mwenyezi Mungu na kubainisha sifa za Mwenyezi Mungu kulingana na aya za Qur'ani na Hadithi zilizopokewa na Ahlubaiti wa Mtume SAW.

Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita, yaani tarehe Pili Juni mwaka 1882 Miladia Giuseppe Garibaldi mzalendo mtajika wa Italia alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 74. Alipambana na kufanya juhudi kubwa zisizo na kifani kuziunganisha Italia ya Kaskazini na Kusini ili kupatikana Italia moja iliyoungana. Baada ya kuyakomboa maeneo kadhaa kutoka mikononi mwa watawala wanaojitegemea, aliongoza wapiganaji wake mara mbili kuushambulia mji wa Rome uliokuwa chini ya udhibiti wa Papa ili kutimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kuifanya Rome mji mkuu wa Italia. Hadi baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia Italia ilikuwa na mfumo wa utawala wa kifalme; na baada ya kuitishwa kura ya maoni tarehe Pili Juni 1946 mfumo wa utawala ulibadilishwa kuwa wa Jamhuri.

Giuseppe Garibaldi 

Miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadiifiana na tarehe Pili Juni 1970 Ayatullahil-Udhama Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa Chuo Kikuu cha kidini, Hawza cha Najaful-Ashraf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92. Baada ya kufariki dunia Ayatullah Bourujerdi, Ayatullah Hakim alijulikana kuwa mmoja wa viongozi wakubwa na wa juu wa kidini, yaani Marjaa-Taqlid, na Wairaqi wengi pamoja na Waislamu wengine wa Kishia wa nchi hiyo na maeneo jirani na Iraq walikuwa wakimfuata alimu huyo. Alisimama imara kupambana na harakati zote zilizoundwa kwa lengo la kuuhujumu Uislamu na hakuwa tayari kuzifumbia macho kwa namna yoyote ile. Fatwa mashuhuri ya Ayatullah Hakim ya kuutangaza Ukomunisti fikra ya Kilahidi ya kumkana Mwenyezi Mungu ilileta mageuzi makubwa nchini Iraq. Halikadhlika, ni yeye aliyetoa fatwa ya kuanzisha Jihadi dhidi ya Israel na ya kuyatia nguvu makundi yanayopambana na utawala huo wa Kizayuni. Kujenga na kuasisi maktaba mbalimbali, skuli, Husainiya, maeneo ya shughuli za kiutamaduni na kuandika vitabu kadhaa kikiwemo cha Mustamsiku Urwatil-Wuthqa, Nahjul-Fuqaaha, Sharhu-Tabsirah n.k ni miongoni mwa huduma kubwa zilizotolewa Marjaa Taqlidi huyo mkubwa kwa Hawza ya Najaf na Ulimwengu wa Ushia.

Ayatullahil-Udhma Sayyid Muhsin Hakim

Tarehe Pili Juni ni Siku ya Taifa ya Uingereza.

Nchi ya kisiwa ya Uingereza yenye eneo lenye ukubwa wa zaidi ya kilomitamraba 244,000 inapatikana upande wa Magharibi ya Ulaya na baina ya bahari za Atlantiki, Manche, bahari ya kaskazini na Bahari ya Ireland. Uingereza ina idadi ya watu wanaokaribia milioni 60. Mfumo wa utawala wa nchi hiyo ni wa kifalme, lakini mamlaka ya utendaji ya serikali yako mikononi mwa waziri mkuu. Akthari ya Waingereza ni wafuasi wa madhehebu ya Anglikana ambalo ni tawi la madhehebu ya Kikristo ya Protestanti. Uingereza imetokana na muungano wa Scotland, England, Wales na Ireland ya Kaskazini. Maeneo hayo kila moja lina mamlaka maalumu ya kujiendeshea mambo yake ya ndani. Tarehe Pili Juni, ambayo ni siku aliyozaliwa Malkia, inajulikana kuwa Siku ya Taifa ya Uingereza.

Na miaka tisa iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe Pili Juni 2013 alifariki dunia Ayatullah Sayyid Jalaluddin Taheri Imam wa kwanza wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Esfahan. Mwanazuoni huyo alizaliwa mwaka 1926 katika moja ya maeneo ya kale ya mji wa Esfahan. Alisomea taaluma za Elimu Jamii na alihitimu masomo yake pia katika taasisi ya Jumuiya ya Iran na Ufaransa na alikuwa amebobea katika lugha za Kiarabu na Kifaransa. Ayatullah Taheri alikuwa mmoja wa wanaharakati wakubwa waliopinga na kupambana na utawala wa Shah, Reza Pahlavi katika vuguvugu la Mapinduzi. Alikuwa Imam wa kwanza wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Esfahan kwa maana kwamba, hata kabla ya Mapinduzi, na kwa sisitizo la Imam Khomeini alisalisha Sala ya Ijumaa katika msikiti mkuu wa Hussein Abad. Sayyid Jalaluddin Taheri alikuwa pia mwalikishi wa Faqihi Mtawala Esfahan na mwakilishi wa mkoa huo katika Baraza la Wataalamu wa Kutunga Katiba na pia kwenye Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ana vitabu kadhaa alivyoandika na kuchapishwa kwa lugha ya Kiarabu.

Ayatullah Sayyid Jalaluddin Taheri

 

Tags