Jun 07, 2022 02:34 UTC
  • Jumanne, Juni 7, 2022

Leo ni Jumanne, mwezi 7 Mfunguo Pili Dhulqaad 1443 Hijria, sawa na tarehe 7 Juni 2022 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 727 iliyopita  alifariki dunia Ibn Baswis mtaalamu wa hati na kaligrafia. Alizaliwa mwaka 651 Hijiria katika mji wa Damascus na kwa muda wa miaka 50 alijishughulisha kufundisha hati yaani kaligrafia. Ibn Baswis aliandika hati kwa mitindo tofauti ya kupendeza na katika umri wake wa uzeeni aliandika nakala ya Qur'ani Tukufu kwa maji ya dhahabu na hati maridadi sana. Nakala hiyo ya Qur'ani na athari nyingine za Ibn Baswis bado ziko hadi leo. 

Ibn Baswis

 

Siku kama ya leo miaka 174 iliyopita Paul Gauguin, mchoraji mashuhuri wa Kifaransa alizaliwa mjini Paris. Alipata hamu ya uchoraji kutoka kwa mke wake ambaye alikuwa mwalimu wa uchoraji. Hatimaye aliamua kusafiri hadi katika kisiwa cha Tahiti kilichoko katika bahari ya Pacific ili kuendeleza sanaa hiyo. Akiwa katika kisiwa hicho alichora picha za kuvutia kuhusiana na mazingira na pia maisha ya watu wa kisiwa hicho hadi alipofariki dunia mwaka 1903.

Paul Gauguin

 

Siku kama hii ya leo miaka 143 iliyopita, yaani tarehe 7 Juni 1879 vilianza vita vilivyochukua muda wa miaka mitano kati ya nchi za Peru, Chile na Bolivia. Vita hivyo vilianza baada ya serikali ya Bolivia kutiliana saini na shirika moja la Chile na kisha kukiuka makubaliano ya mkataba huo. Suala hilo liliifanya Chile iishambulie kijeshi Bolivia. Hatimaye Chile ilijipatia ushindi kwenye vita hivyo na kutiliana saini makubaliano mapya na nchi za Bolivia na Peru. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, ufukwe wote wa Bolivia na sehemu ndogo ya ardhi ya Peru ilichukuliwa na Chile. 

 

Katika siku kama ya leo miaka 55 iliyopita na kufuatia kushindwa Waarabu katika vita na utawala haramu wa Israel, askari wa utawala huo waliingia katika mji wa kihistoria na kidini wa Baitul Muqaddas. Waislamu wanaupa utukufu maalumu mji huo kutokana na kuwa Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa ambacho ni kibla cha kwanza cha Waislamu unapatikana humo na pia kutokana na kuwa ni sehemu ambayo Mtume Mtukufu (saw) alipaa kuelekea mbinguni katika tukio la Mi'raaj kutokea hapo. Tangu utawala ghasibu wa Israel uzikalie kwa mabavu ardhi za Wapalestina,  umekuwa ukitekeleza njama hatari za kuuharibu msikiti huo na badala yake kujenga hapo hekalu bandia la Nabii Suleiman (as). Utawala huo vilevile unatekeleza siasa hatari ya kuvuruga muundo wa jamii asili ya wakazi wa mji wa Baitul Muqaddas kwa kuwafukuza Wapalestina katika ardhi zao na kujenga hapo vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi na Kizayuni. Walowezi hao wa Kizayuni wanafanya njama kubwa ya kufuta kabisa nembo na alama za Wapalestina na Waislamu katika mji huo mtukufu wa Baitul Muqaddas.

Maeneo matakatifu wa Palestina

 

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Juni 1980, ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia na kukiharibu kituo cha nyuklia cha Tamouz kilichoko karibu na Baghdad, mji mkuu wa Iraq. Licha ya shambulizi hilo kuharibu kikamilifu kituo hicho cha nyuklia na kuzikasirisha fikra za waliowengi duniani na vilevile kulaaniwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini hakuna hatua yoyote ya kivitendo ilizochukuliwa dhidi ya utawala wa Israel. Hivi sasa utawala huo ghasibu unamiliki zaidi ya vichwa 200 vya makombora ya nyuklia, na umekuwa ukikataa kuwaruhusu wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuikagua mitambo na vinu vyake vya nyuklia.

Kituo cha nyuklia cha Tamouz cha Iraq kilichoshambuiwa na Israel

 

Tags