Jul 02, 2022 06:01 UTC
  • Jumamosi, 2 Julai, mwaka 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 2 Dhul Hijja 1443 Hijria Qamaria inayosadifiana na tarehe 2 Julai mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita mfumo wa kisultani ulifutwa huko Brazil katika mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji wa damu na badala yake ukaasisiwa mfumo wa jamhuri. Mfalme wa mwisho wa Brazil alikuwa Pedro II ambaye alifanya jitihada za kufanya mabadiliko nchini humo. Hatua za mfalme huyo hususan ile ya kuondoa biashara ya utumwa mwaka 1888, iliwakasirisha wamiliki wa ardhi waliokuwa wakiunga mkono mfumo wake wa kisultani. Pedro II alienguliwa madarakani bila ya mapambano yoyote na mfumo wa jamhuri ukaasisiwa nchini Brazil.

Pedri II

Miaka 97 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Patrice Lumumba mhandisi wa uhuru wa Kongo. Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa. Lumumba aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokita "Kongo, Nchi Yangu."

Patrice Lumumba

Tarehe Pili Julai miaka 61 iliyopita aliaga dunia mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway. Alizaliwa mwaka 1899 na kwa muda fulani alijishughulisha na uandishi huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway alianzisha mbinu ya kuandika riwaya na tungo fupi fupi na alikuwa akitumia lugha nyepesi na inayoeleweka. Mwaka 1954 mwandishi Ernest Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi. Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na For Whom The Bell Tolls".

Ernest Hemingway

Miaka 55 iliyopita katika siku kama hiyo sawa na Pili Dhu al-Hijjah ya pili 1388 Hijria Qamaria, Ayatollah "Seyyed Mohammad Mohaghegh Damad", msomi mkubwa wa chuo cha Kiislamu cha ya Qom, alifariki dunia. Seyed Mohammad Mohaghegh Damad, mwana wa Seyed Jafar Mousavi, alizaliwa mwaka 1325 Hijria Qamaria huko Ahmadabad, Ardakan, Yazd.

Alipoteza baba yake kabla ya kuzaliwa na kisha akampoteza mama yake akiwa na umri wa miaka sita. Licha ya matukio hayo ya kusikitisha, alianza elimu yake. Kisha akahamia Yazd na kukamilisha fasihi akiwa anasomeshwa na wahadhiri bingwa wa mji huo. Kisha, kwa ushauri wa mwalimu wake mpendwa, Sheikh Gholamreza Yazdi, alihamia Qom na kunufaika na masomo ya wasomi wakubwa wa chuo cha Kiislamu cha Qom Ayatullah Sheikh Abdul Karim Haeri Yazdi alivutiwa sana na kipaji cha Mohaghegh Damad na alitiwa moyo na mustakabali wa chuo cha Kiislamu cha Qom kutokana na uwepo wake. Hali hii ilimfanya amkubali kama mkwewe na kumpa jina la utani la "bwana harusi" yaani Damad kwa lugha ya Kifarsi.

Ayatollah Seyyed Mohammad Mohaghegh Damad

Alitilia maanani sana ufundishaji na alipokuwa kitandani katika siku za mwisho za maisha yake, alilia kwa sababu hakuweza kuhudhuria darasa. Baada ya siku 75 za kuugua, hatimaye  aliaga dunia kutokana na mshtuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 63 na akazikwa katika haram ya Imam Masoumeh (AS) mjini Qom.