Jul 03, 2022 02:12 UTC
  • Jumapili tarehe 3 Julai 2022

Leo ni Jumapili tarehe 3 Dhilhija 1443 Hijria sawa na Julai 3 mwaka 2022.

Katika siku kama ya leo miaka 118 iliyopita inayosadifiana na 3 Julai 1904, alifariki dunia Theodor Herzl, mwasisi wa harakati ya kimataifa ya Kizayuni. Herzl alizaliwa mwaka 1860 huko Bucharest mji mkuu wa Hungary na kisha kuelekea Austria. Mnamo mwaka 1897 aliunda Taasisi ya Kimataifa ya Kizayuni kwenye kongamano lililofanyika nchini Uswisi. Herzl alibuni mikakati ya kuasisiwa utawala ghasibu na wa Kizayuni wa Israel kwenye ardhi za Palestina, utawala ambao hadi leo unaendelea kufanya jinai kubwa na kusababisha maafa yasiyo na kifani dhidi ya raia madhlumu wa Palestina.

Theodor Herzl

Tarehe 12 Tir 1349 Hijria Shamsia, yaani miaka 52 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Allamah Abdul Hussein Amini, faqihi mkubwa na mwandishi hodari na mashuhuri wa Kiislamu. Kitabu cha kwanza cha mwanazuoni huo alikipa jina la Shuhadaul Fadhila. Hata hivyo kitabu mashuhuri na kikubwa zaidi cha Allamah Amini ni kile cha "al Ghadiir Fil Kitabi Wassunnah". Ndani ya kitabu hicho Allamah Amini amekosoa na kuchunguza vitabu vikubwa na marejeo vya Kiislamu 150 akithibitisha wilaya na haki ya Imam Ali bin Abi Twalib ya kuwa Khalifa na Imam wa Waislamu baada tu ya Mtume Muhammad (saw) kufariki dunia. Mwanazuoni huyo alisafiri kwa taabu katika nchi nyingi kama India, Uturuki, Syria, Misri na Iraq kwa ajili ya kukusanya ushahidi mbalimbali wa kihistoria alioutumia katika kitabu hicho.

Allamah Abdul Hussein Amini

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege la Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas, kusini mwa Iran na kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ilishambuliwa kwa makombora mawili ya jeshi la Marekani kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo. Shambulio hilo lilidhihirisha zaidi unyama wa serikali ya Marekani. Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa.

Ndege ya abiria ya Iran

Na Tarehe 3 Julai miaka 9 iliyopita rais wa zamani wa Misri kutoka harakati ya Ikhwanul Muslimin, Muhammad Morsi aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyoongozwa na jeshi la nchi hiyo. Mapinduzi hayo yaliongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Sisi. Morsi alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Misri baada ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011. Hata hivyo mwanasiasa huyo hakuweza kutatua matatizo ya kisiasa na kiuchumi ya muda mrefu ya nchi hiyo. Vilevile licha ya kwamba alihesabiwa kuwa katika safu za wanaharakati wa Kiislamu lakini alidumisha uhusiano wa karibu na utawala haramu wa Israel na akatangaza kutambua rasmi mkataba ya Camp David na utawala huo haramu. Vilevile alitekeleza siasa zisizo sahihi kuhusu baadhi ya nchi za Kiislamu na hatimaye akasalitiwa na nchi alizozitegemea ambazo ziliwaunga mkono na kuwasaidia wale waliomuondoa madarakani.

Muhammad Morsi