Jul 04, 2022 04:12 UTC
  • Jumatatu tarehe 4 Julai 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 4 Dhulhija 1443 Hijria sawa na tarehe 4 Julai 2022.

Siku kama ya leo miaka 246 iliyopita, yaani tarehe 4 Julai mwaka 1776 wawakilishi wa majimbo 13 ya awali ya Marekani walisaini "Azimio la Uhuru" wa nchi hiyo katika mji wa Philadelphia. Ardhi ya Marekani kwa maelfu ya miaka ilikuwa makazi ya Wahindi Wekundu. Mwishoni mwa karne ya 15 wavumbuzi wa Ulaya waliwasili Marekani na nchi mbalimbali za Ulaya zikavamia na kukalia kwa mabavu kila eneo la nchi hiyo. Wazungu hao wa Ulaya waliandamana na mamilioni ya watumwa kutoka Afrika ambao walitumiwa katika kazi ngumu za mashambani na viwandani. 

Bendera ya Marekani

Miaka 76 iliyopita katika siku kama ya leo, visiwa vya Ufilipino vilijitangazia uhuru kutoka kwa Marekani. Fernando Magellan mvumbuzi wa Kireno pamoja na wenzake ndio waliokuwa Wazungu wa kwanza kutoka Ulaya kuwasili katika ardhi ya Ufilipino na hiyo ilikuwa mwaka 1521. Katika kipindi cha nusu karne baadaye, Uhispania ikawa imeidhibiti ardhi yote ya nchi hiyo. Mkoloni Muhispania alipora mali na utajiri wa Ufilipino kwa muda wa karne tatu.

Bendera ya Ufilipino

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita yaani 13 Tir mwaka 1350 Hijria Shamsiya alifariki dunia mwalimu mkubwa wa fasihi wa Iran, Dakta Muhammad Muin, baada ya kufanya juhudi kubwa za miaka mingi katika nyanja za utamaduni na mila za Kifarsi. Dakta Muin alizaliwa katika mji wa Rasht kaskazini mwa Iran. Alijifunza fasihi ya Kiarabu ujanani na baada ya kukamilisha masomo yake katika skuli ya Darul-Funun alielekea katika Chuo Kikuu cha Tehran na kujiunga na masomo katika kitengo cha fasihi na falsafa. Mwaka 1321 Hijria Shamsiya Ustadh Muin alianza kufanya kazi ya kufundisha na utafiti katika Chuo Kikuu cha Tehran akiwa mhitimu wa kwanza wa shahada ya udaktari wa lugha na fasihi ya Kifarsi.

Dakta Muhammad Muin

Na katika siku kama ya leo miaka 12 iliyopita,  Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah mmoja wa maulama mashuhuri na marja taqlidi wa Kiislamu alifariki dunia. Allama Fadhlullah alizaliwa mwaka 1935 katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq katika familia ya kidini yenye asili ya Lebanon. Sayyid Fadhlullah alianza kujifunza elimu ya dini katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Najaf, Iraq akiwa bado kijana mdogo. Alijishughulisha na uandishi wa makala na vitabu na alikuwa mshairi. Ayatullah Fadhlullah alikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah, na jambo hilo liliikasirisha sana Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zilifanya majaribio kadhaa ya kutaka kumuua. Ayatullah Muhammad Hussein Fadhlullah ameandika vitabu vingi vya thamani ikiwemo tafsiri ya Qur'ani ya "Min Wahyil Qur'an."

Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah

 

Tags